CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Maswa, Simiyu, kimewashauri wafanyabiashara kufanya biashara kwa kuzingatia sheria badala ya kuwaogopa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ushauri huo ulitolewa mjini hapa mwishoni mwa wiki na mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbai, alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Maswa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mzadeco.
Kasulumbai alisema katika siku za hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kukikumbatia Chama cha Mapinduzi kwa kufanya kila kile ambacho wanaagizwa na viongozi wake wakihofia iwapo watapingana nacho biashara zao zitafungwa.
Alisema si kweli kwamba kila mfanyabiashara anapaswa kufuata maelekezo ya viongozi wa CCM kwa vile biashara wanazoziendesha zinalindwa na sheria za nchi na hazilindwi na CCM, hivyo hakuna sababu za msingi za wafanyabiashara kukaa wakinyenyekea kila mara hata pale wanapolazimishwa kutoa michango ya kuichangia CCM.
“Jamani ndugu zangu wafanyabiashara sioni sababu za ninyi kuendelea kuwakumbatia hawa viongozi wa CCM na chama chao, eleweni kuwa biashara zenu zinalindwa na sheria, na siyo CCM, hakuna sababu ya kuwaogopa viongozi wake, simameni katika sheria,” alisema Kasulumbai.
Kuhusu suala la ajira kwa vijana, mbunge huyo aliwataka vijana kujiunga katika vikundi na kujianzishia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali badala ya kukaa na kusubiri misaada wanayoahidiwa na serikali ya CCM.
Naye mbunge wa Meatu, Meshack Opulukwa, aliwataka wana CHADEMA katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kuhakikisha wanaongeza mshikamano ili kukiwezesha chama hicho kushika dola katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment