Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, ametoa tamko la Musoma, likiwataka Watanzania wote wapenda nchi yao, kujiandaa kwa maandamano makubwa na mgomo wa wananchi yatakayofanyika Machi 25, 2013, nchi nzima, kushinikiza uwajibikaji (kujiuzulu au kufukuzwa kazi) kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo, kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.
"Yatakuwa maandamano makubwa ya kuisimamisha nchi...tunataka siku hiyo mama ntilie wawe barabarani, watoto waliofeli na wazazi wao wawe barabarani, bodaboda wawe barabarani, wamachinga wawe barabarani, walimu wawe barabarani, wanafunzi walioko shuleni na vyuoni wawe barabarani, askari watuunge mkono.
"Wazalendo wote watuunge mkono, Machi 25, 2013, Watanzania wawaoneshe watawala kuwa sauti ya wananchi ni kubwa na muhimu kuliko waziri mmoja na naibu wake...tunataka kitu kidogo tu, waziri na naibu wake wajiuzulu, tunataka wawajibike kwa matokeo mabaya ambayo yametuingiza kwenye kitabu cha maajabu ya dunia..., wanaume na wanawake siku hiyo hakuna mtu kubaki ndani.
"Tutaisimamisha nchi katika majiji manne, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha...nanyi wa Musoma mnataka kulianzisha hapa? Haya Mbunge Nyerere wananchi wako nao wamesema watalianzisha hapa hapa, hawataki kuja Mwanza, kwa hiyo wa Butiama watashuka Musoma, wa Tarime watashuka hapa, wa Serengeti, Bunda na Mwibara, watashuka hapa, yataanzia wapi na kuelekea wapi, mtaambiwa hatua za baadae. Wananchi mjiandae Machi 25, maandamano na mgomo mkubwa," alisema Mbowe.
Kamati ya Ngwilizi
Mwenyekiti Mbowe pia ametoa kauli na msimamo wa CHADEMA juu ya kuwepo kwa wito wa kile kinachoitwa kuwa ni Kamati ya Kudumu ya Kinga, Haki na Maadili ya Bunge chini ya uenyekiti wa Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (Kamati ya Ngwilizi) kuwaita wabunge wa CHADEMA kutokana na kile kinachodaiwa kuwa vurugu zilizotokea bungeni siku ya Februari 4, 2013.
Msimamo wa CHADEMA ni kwamba, wawakilishi hao wa wananchi hawatakwenda kuhojiwa kwenye hiyo Kamati ya Ngwilizi, kwa sababu za msingi zifuatazo; kamati hiyo haipo, kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za bunge, kamati zote za bunge zilimaliza muda wake siku bunge lilipoahirishwa, Februari 8, 2013, baada ya mkutano wa 10 ambao ni nusu ya uhai wa bunge.
"Kwa mujibu wa kanuni ya bunge 113 kifungu kidogo cha 7 kinazungumzia ukomo wa uhai wa kamati za bunge ambao ni wakati wa Mkutano wa 10 wa bunge, yaani nusu ya uhai wa bunge. Hivyo kamati zote, ikiwemo hii ya Ngwilizi, zilishamaliza muda wake. Kanuni ya 113 kifungu cha 10, kinazungumzia position ya Mwenyekiti wa kamati na ukomo wake, Ngwilizi hana mamlaka tena, maana uenyekiti wake ulikwisha kuanzia Februari 8, 2010..."
"Hivyo wawakilishi hao wa wananchi walioitwa, hawatakwenda, kuhojiwa, kama wanataka kutufukuza ubunge kwa maslahi ya CCM wajaribu waone...hawa ni wawakilishi wa watu, si suala la wabunge wa CHADEMA! Kama inafikia hatua wao wanaweza kufanyiwa vyovyote tu watu wanavyotaka, je mwananchi wa kawaida atapata wapi ya kuzungumza," amesema Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesisitiza kuwa CHADEMA inashangaa kuona wabunge wake leo wanaitwa kuhojiwa na Kamati ya Ngwilizi, kwa suala la vurugu za bungeni, Februari 4, 2013, wakati kamati hiyo hiyo ilishalishughulikia suala hilo hilo na ikatoa hukumu bila kuwasikiliza.
"Leo ndiyo wamekumbuka kuhahalisha utaratibu mbovu na haramu waliotumia kushughulikia suala hilo...walitunga tuhuma, wakaendesha mashtaka, wakatoa hukumu na wakataja hata wakosaji kuwa ni Lissu, Mnyika, Gekul na Nassar, wakaitangazia dunia nzima, watanzania wote na nchi nzima ikaambiwa kuwa hawa ndiyo wakosaji...wakafanya hivyo bila kuwaita na kuwasikiliza hata siku moja, sasa ndiyo wameona umuhimu wa kuwaita, kwa utaratibu upi? Wanataka kusikiliza kitu gani wakati walishaamua na wakosaji wanajulikana?
"Wanasahau kuwa kamati hiyo ni sawa na mahakama ya bunge, inapokaa ni sawa na mahakama, sasa kwa taratibu za mahakama, ikishashughulikia suala moja, haiwezi tena kukaa kushughulikia suala hilo hilo ambalo tayari imeshalitolea uamuzi. Tatu wito huu unakiuka katiba ya nchi na sheria...," alisema Mbowe mbele ya mkutano huo wa hadhara uliohudhuria na maelfu ya wananchi wa Musoma na vitongoji vyake.
Mbunge Vincent Nyerere azuiwa kwenda Kamati ya Bunge
Wananchi wa Musoma waliohudhuria mkutano huo wa hadhara kwa kauli moja wamemzuia Mbunge wao Vincent Nyerere kuitikia wito wa kuhojiwa na kile kinachoitwa kuwa ni Kamati ya Ngwilizi, wakisema kuwa hiyo ni kinyume na misingi ya demokraia na uendeshaji wa shughuli za bunge.
Wananchi hao walifikia uamuzi huo baada ya kuhojiwa na Mwenyekiti Mbowe, iwapo katika mazingira hayo (aliyoyaelezea mapema) iwapo wako tayari mbunge wao aitikie wito huo ambao umefikishwa kwake kwa barua ya kipolisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, nao wakasema 'asiende asiende...hatutaki aende.
No comments:
Post a Comment