Tuesday, March 12, 2013

Nyerere kupeleka bungeni vilio vya wana-Tarime


MBUNGE wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere, amewahakikishia wananchi kutoka vijiji saba vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara, uliopo katika Jimbo la Tarime kuwawasilishia matatizo yao katika vikao vya Bunge.
Amesema atambana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini, juu ya changamoto zilizopo kwa wananchi hao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Sabasaba mjini Tarime, alipopatiwa nafasi na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wakati wa ziara ya kuimarisha chama na uzinduzi wa majimbo ya chama, Nyerere alisema amefikia hatua hiyo baada ya kuyapokea malalamiko mengi ya wananchi hao.



Awali wananchi hao kutoka vijiji vya Nyakunguru, Kewanja, Nyamwaga, Matongo, Nyangoto, Kerende na Genkuru, walimuelezea mbunge huyo juu ya kero ya kuporwa ardhi yao na makazi yao kwa kufidiwa kiasi kidogo na wengine kukosa kabisa na kufunguliwa mashitaka kutokana na kuendelea kuishi maeneo yao.
Nyerere aliwaondoa wasiwasi wao kuwa mbali ya kuyachukua malalamiko yao dhidi ya Kampuni ya African Barrick na kuyafikisha bungeni, pia aliwaambia kuwa atakuwa anawasilisha matatizo mengine yanayozihusu wizara nyingine kuyasemea moja kwa moja na kwa njia ya hoja binafsi, ili kuibana serikali kuyashughulikia kikamilifu.
Katika hatua nyingine, wanachama na wadau wa CHADEMA, wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, kuondoa uongozi wa kamati tendaji ya chama hicho wilayani hapa kwa ajili ya kukiweka chama hicho vema.

No comments:

Post a Comment