NAIBU Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Mtatiro Julius, amesema kuwa chama hicho kikifanikiwa kushika dola kitahakikisha kinashirikiana na watu safi akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza katika kipindi cha ‘Tuongee Asubuhi’ kinachorushwa na televisheni ya Star tv, Mtatiro alisema chama hicho kipo tayari kuhakikisha wanakuwa na lengo moja la kuijenga nchi kwa kushirikiana na viongozi waadilifu.
Mtatiro, alisema chama hicho kimejiwekea malengo na kipo tayari kuongoza dola pamoja na kushirikisha watu safi ambao watakuwa wakisimamia vema utekelezaji na kuwaletea Watanzania maendeleo.
Alisema ni muhimu Watanzania wakapata dira ya taifa itakayowaongoza na kuonesha wanapotaka kuelekea.
Kuhusu vyama vya upinzani kuwa chanzo cha kuvuruga amani, Mtatiro, alisema vyama hivyo havifanyi kazi ya kushawishi Watanzania waharibu amani ya nchi na kama wapo wanaofanya hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua.
Alisema kuwa amani iliyopo inalindwa na Watanzania wenyewe, hasa kupitia viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhubiri suala hilo.
“Sio kweli CCM inalinda amani ya nchi…amani iliyopo inalindwa na Watanzania na kila kiongozi anayesimama kuhubiri jambo hilo,” alisema.
Alisema kuwa iwapo vyombo vya dola vinashindwa kuwachukulia hatua wale wanaoonekana kuvuruga amani basi vyombo hivyo vitakuwa vimeshindwa kufanya kazi.
Mtatiro alisema kuwa uzalendo umepotea miongoni mwa Watanzania kutokana na ufisadi unaofanywa na wale walioshika dola.
“Hivi kweli unaweza kuwahubiria Watanzania wawe wazalendo wakati wanaona matendo yanayofanywa na viongozi wao…waziri anakuwa na nyumba ya sh bilioni sita unafikiri watakuelewa kukizungumza uzalendo?” alihoji.
Alisema kuwa uzalendo unaenda na vitendo, hivyo ili kuurudisha ni muhimu viongozi waliopo madarakani wakaanza kujitafakari upya.
Kuhusu makundi, Mtatiro alisema kuwa yapo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sio katika vyama vya upinzani kwa kuwa wamekuwa wakijitahidi kuyaondoa.
No comments:
Post a Comment