Thursday, January 3, 2013

Mbowe: Msinilishe maneno


ASEMA HAKUMTANGAZA DK. SLAA MGOMBEA URAIS 2015
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema baadhi ya vyombo vya habari vimemlisha maneno, na hivyo kupotosha kauli yake aliyoitoa katika mkutano wa hadhara jimboni Karatu hivi karibuni.
Alisema kuwa upotoshaji huo umeibua mjadala kwa baadhi ya wanasiasa na vyombo kadhaa vya habari wakijaribu kupotosha kuwa ndani ya chama hakuna demokrasia.
Mbowe alifafanua kauli yake jana wakati akizungumza na Tanzania Daima na kueleza kile alichokisema katika mkutano wake huo ili kuondoa upotoshaji unaoendelea.
Alisema kuwa chimbuko la kauli yake lilikuwa ni baada ya kusikia watu wakisema kuwa kuna makundi ndani ya chama ambayo yanawaunga mkono yeye, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Kabwe yakiwataka wagombee urais 2015.
“Nilichokisema ni kwamba hakuna makundi katika chama, ila kuna mitazamo tofauti katika mambo mbalimbali jambo ambalo ni la kawaida sana,” alisema.
Mbowe alifafanua kuwa, aliwaambia wananchi kuwa hawana makundi, bali wana utofauti wa mtazamo na kwamba hakuna ugomvi kati yake na Dk. Slaa kwa sababu ya urais 2015.
“Nilisema sigombei, hivyo hatugombanii vyeo, tunaheshimiana na tunaelewana. Niliongeza kuwa 2010 sikugombea, tulimtuma Dk. Slaa na alitosha katika nafasi ile na hakuna anayebisha kuwa hakutosha maana alitupatia wabunge wengi.
“Niliwaambia kuwa mimi ni mwenyekiti, nitasimamia kanuni na taratibu za kuwapata wagombea wazuri, tangu rais, wabunge na madiwani, na nikasema ni vema tukawatambua wagombea mapema kwani hatutakubali wale wanaojiunga mwishoni kutoka CCM kwani tumegundua ni mamuluki.
“Hao wananilisha maneno kwa kunitolea kauli tofauti na niliyoisema kulingana na malengo yao,” alisema.
Mbowe alisema kuwa anaomba Watanzania waelewe kuwa yeye ni mwenyekiti wa chama na anaelewa umuhimu wa vikao na kuheshimu uamuzi wa vikao hivyo.
“CHADEMA si mali ya Mbowe, ni mali ya wanachama, hivyo siwezi kupinga suala la uamuzi wa pamoja ambao mimi mwenyewe ndio nawashauri wengine,” alisema.
Alisema kuwa yeye ni mmojawapo wa waasisi, na amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu zaidi ya miaka 20 sasa, na kwamba anajua maana na umuhimu wa kufanya kazi kama timu, lakini akaomba kuwa tafsiri za watu binafsi au baadhi ya vyombo vya habari zisipotoshe alichokisema.
Pinda akana
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amekana kumhonga Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Said Arfi, akisema kuwa hajawahi kutoa wala kupokea rushwa maishani mwake.
Pinda alikuwa akikanusha tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) mikoa ya Rukwa na Katavi, Laulent Mangweshi, kuwa alimhonga Arfi ili amsaidie apite bila kupingwa kwenye jimbo lake la Mlele katika uchaguzi wa 2010.
Akihutubia wananchi wa Mkoa wa Katavi kwenye sherehe za kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha 2013 zilizofanyika wilayani Mpanda, Pinda alisema ni vizuri CHADEMA wakakaa na kumaliza tofauti zao mkoani humo bila kuzushiana mambo yasiyo na msingi.
“Nimesikia kwenye mkutano wa mashauriano wa CHADEMA wa mikoa ya Rukwa na Katavi ulifanyika Desemba 16 mwaka jana, Mwenyekiti wa BAVICHA wa mikoa hiyo, alishutumu Arfi kuwa alihongwa fedha na mimi ili nipite bila mpinzani,” alisema.
Alisema yeye hakumhonga Arfi na hata hawezi kufanya hivyo kwani katika maisha yake hajawahi kutoa wala kupokea rushwa.
Pinda alisema kuwa yeye na Arfi wamekuwa na ukaribu kutokana na shughuli zao za ubunge ambapo wamekuwa wakishirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mpanda na Mkoa wa Katavi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment