Saturday, February 23, 2019

TAARIFA KUHUSU KUSHIKILIWA KWA HALIMA MDEE NA MWENDELEZO WA MANYANYASO KWA WANACHADEMA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KUHUSU KUSHIKILIWA KWA HALIMA MDEE NA MWENDELEZO WA MANYANYASO KWA WANACHADEMA

Baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kumhoji, kumshikilia na kumnyima dhamana Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) Halima Mdee (Mb) Chama kimewaagiza wanasheria wake kuchukua hatua zaidi za kisheria haraka iwezekanavyo, ikiwemo kuandaa na kuwasilisha maombi ya _habeas corpus_ Mahakama Kuu ifikapo Jumatatu, Februari 25, 2019.

Aidha, kupitia taarifa hii, Chama kinalaani na kukemea vikali kitendo hicho cha polisi ambacho ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu, ikiwa ni mwendelezo wa vitendo vya jeshi hilo maeneo mbalimbali nchi nzima, kuwatendea wapenzi, wafuasi, wanachama na viongozi wa Chadema kinyume na taratibu za sheria za nchi.

Chama kinachukulia tukio hilo la leo kuwa ni kuendelea kuandamwa kwa wawakilishi wa Chadema wenye nafasi za kiserikali, wakiwemo wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na wabunge, wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao, likiwa limetokea siku chache baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' kuhojiwa na kushikiliwa na polisi kwa kutimiza wajibu wake, huku jeshi hilo likiwa halijawahi kutoa taarifa yoyote iwapo limewahi kuwaita, kuwahoji, kuwashikilia na kuwafikisha mahakamani viongozi wa CCM wakiwemo wabunge wa chama hicho wanaotoa kauli za kibaguzi, chuki na hata kumtishia maisha Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu.

Mapema leo asubuhi Mdee ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mbunge wa Kawe aliitikia wito kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, kufika Kituo cha Polisi Oyster bay kwa ajili ya mahojiano, ambapo amehojiwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi kwenye moja ya mikutano yake ya hadhara aliyofanya Jimbo la Kawe, ikiwa ni mwendelezo wa ratiba ya ziara za kuwatembelea, kuwasikiliza na kuwapatia mrejesho wapiga kura wake jimboni humo. 

Mbali ya kumshikilia Mdee chini ya ulinzi, polisi wameshikilia simu zake mbili na pia wamewataarifu wanasheria wake kuwa wataenda kufanya upekuzi nyumbani kwake wakati wowote kuanzia sasa. 

Chama kimeshangazwa na hatua hiyo ya kushikilia simu na kutaka kwenda kupekua nyumbani kwa mtuhumiwa anayetuhumiwa kufanya uchochezi kwenye mkutano wa hadhara, au ni mwendelezo ule ule kama ilivyokuwa kwa Mbunge Lissu kwenda kupimwa mkojo wakati anatuhumiwa kwa uchochezi? 

Pamoja na kuwaelekeza wanasheria kupitia Kurugenzi ya Katiba na Sheria ya Chama, kuwasilisha maombi hayo ya _habeas corpus_ kuiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kuwaita na kuwahoji polisi kwa kumshikilia Mdee na kumnyima dhamana, Chadema inavitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi kuacha kutekeleza majukumu yake bila kuzingatia Katiba na sheria za nchi. 

Haki ya kupata dhamana iko kwa mujibu wa sheria zetu. Haitolewi kwa utashi wa mtu wala mamlaka yoyote. Tunalikumbusha jeshi hilo kuwa kuminya na kunyima uhuru wa mtu kwa kumweka ndani ni uonevu usiokubalika, unaostahili kupingwa, kukemewa na kulaaniwa vikali na watu wote wapenda haki.

Imetolewa leo Jumamosi, Februari 23, 2019 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment