Monday, February 18, 2019

Mahakama ya Rufaa kutoa uamuzi rufaa ya Jamhuri dhidi ya Mbowe na Matiko

Mahakama ya Rufani leo imeketi kusikiliza hoja za wakata rufaa (Jamhuri) na wakatiwa rufaa (utetezi) kwenye maombi ya rufaa namba 344  yaliyopo Mahakama Kuu kuhusu kufutiwa dhamana kwa washtakiwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Mb) na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama ya Rufaa kuamuru maombi hayo 344 yatupiliwe mbali na Mahakama Kuu kwa sababu hayaendani na kifungu cha 362 (1) cha Sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo.

Kwa upande wao Mawakili wa Wajibu Rufaa wamesisitiza kwamba Mwenendo na uamuzi wa Mahakama Kuu mbele ya Rumanyika J ulikuwa sahihi kisheria na haukuwa na dosari zozote. Wamesisitiza kwamba upande wa Jamhuri ulishirikishwa katika kila hatua, na kupewa fursa sawa ya kusikilizwa. Wamedai mahakamani hapo kuwa rufaa iliyokatwa na Serikali kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kutupilia mbali hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Serikali hazina mashiko kisheria na kuomba rufaa hiyo iliyoko mbele ya Mahakama ya Rufaa  itupiliwe mbali.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, upande wa Jamhuri (warufani) na upande wa utetezi (wakatiwa rufaa) Mgasha J kwa niaba ya jopo la majaji watatu, amesema Mahakama ya Rufaa itatoa uamuzi wake kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili katika tarehe itakayopangwa.

Mwenyekiti Mbowe (Mb) na Mbunge Matiko wamerudishwa mahabusu Segerea hadi kesi hiyo itakapoitwa tena mahakamani hapo wa ajili ya kutolewa uamuzi.

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment