Monday, October 8, 2018

TUNDU LISSU AZUNGUMZIA KUHUSU MJADALA WA HAMA HAMA YA WABUNGE NA MADIWANI


Huu mjadala wa hama hama ya Wabunge wa CHADEMA ni muhimu sana. Unahitaji kujadiliwa kwa tahadhari na kwa umakini, vitu ambavyo ni adimu katikati yann kelele na vumbi kubwa vilivyotokana na hama hama hii. 

Napendekeza kutafakari mambo yafuatayo ya kufikirisha katika kujaribu kuelewa maana halisi ya hii hama hama:

(1) Kuhama kwa viongozi wa kisiasa kutokana na migogoro na tofauti za kisiasa ndani ya vyama vya siasa sio jambo geni katika historia ya vyama vingi nchi yetu. Hata hivyo, kuhama kwa Wabunge na Madiwani wa upinzani kwenda CCM ni jambo geni. 

(a) Kati ya 1995, CHADEMA ilipopata Wabunge wake wa kwanza (walikuwa wanne), na 2015 ilipopata  Wabunge 35 wa majimbo na 37 wa Viti Maalum, hakuna Mbunge au diwani hata mmoja aliyejiuzulu ubunge na kujiunga na CCM kwa sababu yoyote ile. 

(b) Katika kipindi hicho cha '95 - '15, Wabunge na Madiwani walioondoka CHADEMA na vyama vingine vya upinzani na kuhamia CCM:

(i) ama walifukuzwa kwenye vyama vyao (mfano madiwani 5 wa CHADEMA Arusha, akina Danhi Makanga na Teddy Kasela Bantu wa UDP, n.k.), 

(ii) ama walipoteza ubunge wao mahakamani (mfano Makongoro Nyerere, Dr. Lamwai, Kifu Gullamhussein Kifu wa NCCR-Mageuzi, n.k.) 

(iii) au walisubiri washindwe ubunge ndio wakahamia CCM (mfano Dr. Amani Walid Kabourou, Saidi Arfi wa CHADEMA na wengineo wengi)

(c) Katika kipindi hicho hicho, waliokuwa wanahama chama wakiwa wabunge na kujiunga na vyama vingine walikuwa wanaCCM (mfano Freddie Mpendazoe).

(2) Katika kipindi hicho chote, licha ya matatizo mengi, hakukuwa na ukandamizaji wa haki za kisiasa na haki za binadamu kwa ujumla kama ilivyo sasa.

(a) Vyama vya siasa vilikuwa vinaendesha mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa. 

(i) Leo shughuli za kawaida za kisiasa, kama mikutano ya hadhara, maandamano na hata vikao au semina za ndani,  zimepigwa marufuku kabisa.

(b) Viongozi wa vyama vya upinzani hawakuwa walengwa wa moja kwa moja wa ukandamizaji unaoendeshwa na vyombo vya usalama. 

(i) Leo karibu viongozi wote wa CHADEMA wa ngazi za juu, wakiwemo Wabunge wengi, na wa ngazi za kati na hata za chini wanakabiliwa na kesi za jinai mahakamani. 

(ii) Wengi wa wale ambao bado hawana kesi angalau wameonja mahabusu au kipigo cha polisi kwa kufanya shughuli za kawaida za kisiasa zinazoruhusiwa na sheria zetu. 

(iii) Wapo viongozi wameuawa kinyama lakini mauaji yao hayajachunguzwa wala hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika. 

(iv) Wengine wamejeruhiwa vibaya katika mazingira hayo hayo ya kulenga kuwaua au kuwadhuru viongozi wa upinzani. 

(c) Haki, hadhi na heshima ya Bunge na Wabunge wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge au katika shughuli za kibunge, zilikuwa zinaheshimiwa. Leo kuwa Mbunge, au diwani au hata Mwenyekiti wa Kijiji au Mtaa wa upinzani, hasa wa CHADEMA, ni adha kubwa.

(i) Leo Wabunge wa upinzani wanapigwa na kudhalilishwa na askari wenye sare za polisi ndani ya Ukumbi wa Bunge. 

(ii) Wakitoka nje ya Bunge Wabunge wa upinzani wanatekwa nyara na mapolisi na kusafirishwa usiku kupelekwa Dar Es Salaam au Arusha au Morogoro au kwingineko. 

(iii) Leo Wabunge wa upinzani wanakamatwa na kuwekwa mahabusu na baadae kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa kushiriki kwenye mikutano ya hadhara kwenye majimbo yasiyokuwa yao, ambalo halijawahi kuwa kosa la jinai katika nchi yetu.  

(3) Ambao wanajiuzulu ubunge na udiwani na kuhamia CCM ni wanaCHADEMA wa aina gani hasa???

(a) Wabunge wote wa CHADEMA ambao wamejiuzulu ubunge na kuhamia CCM ni wanaCHADEMA na Wabunge wapya. 

(i) Baadhi, kama Dr. Mollel wa Siha na ole Kalanga wa Monduli, waliingia CHADEMA na bungeni kutokana na wimbi la Lowassa la '15.

(ii) Baadhi, kama Waitara,  Ryoba na ole Millya, wana muda mrefu CHADEMA lakini ni Wabunge wapya.

(iii) Ubunge wa upinzani wanaoujua hawa waliohama, ni ubunge wa upinzani wa Tanzania ya Magufuli na Bunge la Spika Ndugai, i.e. ubunge wa adha na mateso, sio ubunge wa heshima wa Bunge la Spika Sitta na Spika Makinda.

(b) Wabunge wenye historia ndefu kwenye CHADEMA au bungeni hawajajiuzulu hata mmoja. 

(i) Tofauti na waliohama, hawa wana historia na uzoefu wa mapambano kisiasa ya upinzani nje na ndani ya Bunge. 

(ii) Tofauti na waliohama, hawa wana historia na uzoefu wa kutiwa misukosuko mbali mbali na Serikali ya CCM kabla na baada ya kuwa wabunge.

(4) Mazingira ya kuhama hama yakoje??? Swali hili ni muhimu kwa sababu ya ubishani mkubwa uliopo kuhusu madai ya matumizi ya rushwa ili kuwarubuni wanaohama. 

(a) Kila aliyehama amerudishwa na CCM kama mgombea wa nafasi ile ile aliyoiacha kwa kujiuzulu, bila hata kufuata utaratibu wa kawaida wa kichama wa kufanya vikao vya uteuzi, n.k. 

(b) Viongozi wa CCM na Serikali yake, kuanzia Rais Magufuli mwenyewe na wa chini yake, wametangaza hadharani kwamba kila atakayejiuzulu ubunge au udiwani atarudishwa kugombea nafasi ile ile kwa kupitia CCM na atatangazwa mshindi kwa nguvu. Hata bila ushahidi wa malipo ya fedha, ahadi hizi ni rushwa kwa tafsiri ya rushwa ya sheria za nchi yetu. 

(c) Kila aliyejiuzulu ubunge au udiwani na kuhamia CCM amefanya hivyo ili 'kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo'!!! 

(i) Hata bila kuhoji ukweli wa sababu yenyewe, inawezekanaje hiyo ndio iwe sababu ya kila mmoja anayejiuzulu na kuhamia CCM???

(ii) Hata bila kuuliza maswali juu ya uhalali wa sababu hiyo, kwa nini wanaojiuzulu sasa wanarudishwa kugombea nafasi zile zile walizoziachia??? 

(iii) Kwani kujiuzulu ubunge au udiwani wa CHADEMA na baadae kugombea nafasi zile zile kwa CCM ni njia pekee ya kumuunga mkono Magufuli??? Kumbuka, John Shibuda wa CHADEMA na John Cheyo wa UDP walikuwa wakiunga mkono jitihada za Rais Kikwete lakini hawakuwahi kujiuzulu ubunge au uanachama wa vyama vyao.

(iv) Hivi inakuwaje wanaounga mkono jitihada za Rais Magufuli ni wanaCHADEMA peke yao??? Vipi akina Lyatonga Mrema, au Profesa Lipumba, au Dovutwa na wengineo wa vyama vingine??? Au ndio kusema hawa hawana madhara yoyote kwa CCM hata wakibaki kwenye vyama vyao???

(v) Hivi inakuwaje wanaounga mkono jitihada za Rais Magufuli ni Wabunge na Madiwani wa Majimbo na Kata peke yake??? 

Inawezekanaje Rais Magufuli asiungwe mkono na Wabunge na Madiwani wa Viti Maalum ambao ndio wengi zaidi bungeni??? 

Au ndio kusema kujiuzulu kwa Wabunge na Madiwani wa Viti Maalum hakuna faida yoyote kwa CCM kwa sababu hakupunguzi idadi ya Wabunge na Madiwani wa upinzani???

(vi) Katibu Mwenezi wa CCM, Polepole, amesema kwamba mwisho wa 'kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo' ni December, '18. Kwa nini zuio hilo la CCM linalingana ama kukaribiana na zuio la kikatiba na kisheria kwa chaguzi za marudio??? Je, hii ni bahati mbaya tu au kuna njama iliyofichwa kwenye hii ratiba ya CCM na ratiba iliyowekwa na Katiba na Sheria za Uchaguzi???

(c) Kila aliyehama 'ameshinda' uchaguzi katika mazingira ya matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi na mfumo wa usimamizi wa uchaguzi wenye upendeleo wa wazi wazi kwa CCM. Matokeo yote ya chaguzi za marudio za hivi karibuni ni matokeo ya kupika kati ya wasimamizi wa uchaguzi wanaCCM na vyombo vya usalama vya Serikali ya CCM. Hata Katibu Mkuu wa CCM Dr. Bashiru Ali amethibitisha hili in so many words. 

(5) Je, tatizo ni Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe??? Hili nalo limeleta mjadala mkubwa. 

(a) Wote waliojiuzulu ubunge na udiwani wa CHADEMA na kujiunga na CCM na wapambe wao wamedai tatizo ni Mwenyekiti Mbowe.

(i) Hata hivyo, waliingia CHADEMA na kuchaguliwa Wabunge au madiwani kwa kupitishwa na vikao vya Chama vilivyoongozwa na Mwenyekiti Mbowe huyo huyo. Baniani mbaya ila kiatu chake dawa!!! 

(ii) Mwenyekiti Mbowe hajawahi kuwa kiongozi wa CHADEMA mzuri kwa CCM tangu angalau '05 alipogombea Urais hadi leo hii. Baadhi ya dhambi zake ni pamoja na kuwa Mchagga, mkwe wa Mzee Mtei, Mkaskazini, Mkristo na, sasa, mng'ang'ania madaraka. 

(iii) Licha ya 'madhambi' haya makubwa, Mwenyekiti Mbowe ni kiongozi wa upinzani mwenye mafanikio makubwa katika historia ya vyama vingi vya siasa nchini kwetu. 

(b) Mwenyekiti Mbowe amelipia mafanikio yake katika siasa za upinzani za Tanzania kwa gharama kubwa sana.

(i) Biashara zake, iwe ni Bilicanas, au uchapishaji magazeti au mashamba ya kilimo, zimeharibiwa na Serikali ya Magufuli ili kulipiza kisasi kwa sababu ya mafanikio yake ya kisiasa.

(ii) Mwenyekiti Mbowe amekamatwa na kushtakiwa kwa jinai kwa sababu za kisiasa kuliko pengine kiongozi mwingine mkuu wa Chama cha siasa katika Tanzania. 

(c) Katika viongozi wote Wakuu wa upinzani katika historia ya Tanzania, ni Mwenyekiti Mbowe, na pengine Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF, ambaye amebaki na msimamo thabiti wa kisiasa licha ya mateso makubwa ambayo amepitishwa. 

(6) Kujiuzulu kwa Wabunge na Madiwani wa upinzani, hasa CHADEMA, katika mazingira haya kuna madhara kwa CHADEMA na kwa siasa za upinzani kwa ujumla. Je, ni madhara gani hayo na ni makubwa kiasi gani kwa CHADEMA na kwa siasa za upinzani???

(a) Ni wazi wapo viongozi, wanachama, wafuasi na wananchi waliokatishwa, na watakaokatishwa, tamaa na matukio haya. Je, ni wengi kiasi gani???

(b) Kama hama hama hii ina madhara makubwa kwa upinzani kama inavyoelezwa na baadhi yetu, ni kwa nini kuna matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi na kila aina ya ubabe na hila kwenye chaguzi za marudio???

(c) Kama 'upinzani unakufa' kama inavyoelezwa, kwa nini Serikali ya Magufuli inaendelea kukataza uhuru wa vyama vya siasa vya upinzani kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria zetu??? Kwa nini bado kuna makatazo ya Bunge Live??? Kwa nini kuna ukandamizaji wa vyombo vya habari na uhuru wa maoni???  

(d) Kama hama hama hii ina madhara makubwa kwa upinzani, kwa nini bado wananchi wetu wanahudhuria kwa maelfu katika mikutano ya hadhara michache inayoruhusiwa wakati wa kampeni za chaguzi za marudio???

Haya ni baadhi ya masuala yanayohitaji kujadiliwa kama sehemu ya mjadala wa hama hama ya Wabunge na Madiwani wa upinzani. Nawataka radhi kwa kuwasubirisha muda mrefu.

No comments:

Post a Comment