Tuesday, October 2, 2018
Hotuba ya mkutano wa mbunge Mch. Peter Msigwa kwa wanahabari ya tarehe 02/10/2018
Ndugu waandishi wa Habari, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kufika mahali hapa baada ya kupewa taarifa ya uwepo wa mkutano huu, tumewaiteni hapa ili tuweze kuuambia umma juu ya mambo machache yanayoendelea katika Mkoa wetu wa Iringa.
Awali ya yote niwape pole kwa usumbufu mliokutana nao wa kuzuiliwa na Mkurugenzi kupitia mambo wa Manispaa kuingia kwenye viwanja hivi vya manispaa Kuja kuripoti Mkutano huu.
Ndugu wanahabari Maelezo yangu yatajielekeza katika hoja zifuatazo;
1. Dhana ya Iringa Mpya iliyoanzishwa na mkuu wa mkoa
2. Matumizi mabaya ya Madaraka.
3 .Matumizi mabaya ya fedha.
Dhana ya Iringa Mpya iliyoanzishwa na mkuu wa mkoa
Ndugu wana habari, wote tunatambua kuwa kuna mabadriko ya kiuongozi katika Mkoa wa Iringa, hasa katika nafasi ya mkuu wa mkoa ambapo tulikuwa na Mkuu wa Mkoa Bi Amina masenza na sasa tuna mwingine.
Ambapo mkuu wa mkoa aliyepo amekuja na dhana hii iitwayo Iringa mpya, Ndugu wana habari hata hivyo dhana hii ina mapungufu mengi; lakini kabla ya kuendelea ndugu waandishi wa habari jiulizeni maswali yafuatayo;
Iringa mpya inafananaje? Inaonekanaje? Tunaweza kuiona kwenye Billboard, Inavyoonekana? Mosi Dhana hii sio shirikishi? Wadau wa kujenga iringa mpya ni kina nani? Ni CCM? RC? UVCCM? Mabalaza ya Madiwani? Wananchi wote? Kama ni wananchi wote wameshirikishwa? What it takes kuifanya Iringa mpya? Ni Appearance ya majengo au mabadriko ya watu? Nini maana halisi ya Iringa mpya? Ni vizuri mkapata majibu ya maswali haya.
Ndugu wana habari, Kwa mtazamo wangu sioni kitu kinachoitwa Iringa mpya, zaidi ya kujenga jina La mtu, kuharibu morali ya watumishi wa Umma,matumizi mabaya ya madaraka, kudharirisha watumishi wa umma hadharani, kujivisha uchungu bandia juu ya anayodhani ni matatizo ya wana Iringa.
Ndugu wana habari, kama Mkuu wa mkoa angekua na nia njema juu ya dhana yake ya Iringa mpya, naiita ni dhana kwa sababu ni kitu ambacho hakipo na hakitekelezeki, Angeitisha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ambayo ipo kwa mujibu wa sheria kifungu 1(8) ya sheria ya mikoa na Tawala za Mikoa na tawala za mikoa No 19 ya 1997, ambayo imetoa mamlaka ya uanzishwaji wa kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) sambamba na kifungu cha 8(2) kinachotaja wajumbe (RCC) miongoni mwao ni wabunge wanaowakilisha majimbo katika mkoa na wabunge wa viti maalumu hawa ni wawakilisha wa wananchi moja kwa moja.
Ndugu wanahabari tuna ushahidi wa kutosha kwamba hakuna mbunge hata mmoja aliyeshirikishwa wala kushiriki katika dhana hii ya Iringa mpya kwasababu sisi pamoja na utofauti wa itikadi zetu, tuna umoja wa wabunge wa mkoa wa Iringa. Napenda niwakumbushe vikao hivi kipindi cha Bi Amina Masenza tulikua tunashiriki, kwa sababu alikuwa anatushirikisha na alienda mbali zaidi na kuita vyama vya siasa vyenye usajiri wa kudumu mkoa wa Iringa, ila huyu ana ajenda zake binafsi sio zinazohusu Iringa.
Ndugu wanahabari lazima mjue kiongozi wa kweli hufurahi na kupongeza mafanikio ya wengine pasipo kuona gele, pamoja na kwamba mimi ni mbunge kwa tiketi ya Chadema, nimejipambanua wazi wazi kutambua mchango wa aliyekua mbunge wa Jimbo hili mama Mbega, Meya mstaafu mzee wetu Mwamwini na Mama Mazenza-RC, DC Kasesera, na wengine wengi waliopita, wana mchango mkubwa sana mpaka hapa Iringa ilipofika.
Sasa jiulizeni hiyo Iringa mpya ni kuamini kwamba waliokuwepo hakuna walichofanya isipokuwa huyu tu ndo kafanya mambo makubwa na mapya? je ni yepi hayo? Ni kuzisulubu Halmashauri na wafanya biashara kwa kuziongezea mzigo hasa mkuu wa Mkoa ana msafara wa Magari 25 haya ni matumizi yanayoathiri, kuchangia fedha ambazo hazikuwa kwenye bajeti? Hii ndo Iringa mpya?.
Ndugu waandishi wa habari tambueni kuwa, Kiongozi wa kweli hachukizwi na ushindani au upinzani bali huona ni changamoto na ni fursa pekee ya kujisahihisha na kujifunza ili kuelekea mahusiano bora na yenye faida kwa jamii. Kinyume kabisa na huyu bwana afanyavyo.
Matumizi mabaya ya Madaraka
Ndugu wana habari, kiongozi wa kweli hamiliki, hatawali wala hawi na amri juu ya watu bali hushauriana na kushirikiana na watu anao waongoza katika kuamua hatima yake na yao, hiki ni kinyume kwa mkuu wa mkoa huyu tuliye nae hii ni kutokana na matukio yafuatayo;
1.Aliagiza mtumishi wa manispaa ambaye ni Afisa maendeleo asimamishwe kazi, akamatwe na hataki kumuona kwenye mkoa wa Iringa, eti tu kwa sababu alishindwa kuwapa viziwi fedha, kwa sababu fedha hizo zilitumika kwenye ziara yake mkuu wa mkoa.
2.Akiwa kata ya nduli eneo la kigonzile, akiongea kwa simu na kaimu meneja wa Tanesco mkoa alisema “unaonaje nikikutia ndani kwa masaa kama mawili? RPC mtafute huyu na mweke ndani kuanzia saa sita hii mpaka saa nane na akitoka aje kwenye ziara yangu”.
3.Akiwa hospitali ya rufaa ya mkoa, alimwambia DMO “nilikua nasubiri uingie kwenye 18 zangu” hii inaonyesha kwamba mkuu wa mkoa anafanya kazi kwa chuki kupitia madaraka yake kwani huyu DMO alikua daktari pekee bingwa wa upasuaji katika hospitali, mpaka dakika hii wagomjwa wanaohitaji upasuaji wamerejeshwa makwao na wengine wanaendelea kutaabika hospitalini na majumbani kwa kukosa huduma, alimwambia asimuone Iringa, eti kisa hospitali ilikuwa inatoza TSH 12800/=, jiulizeni hivi fedha hii ina thamani kuliko wanaohitaji kufanyiwa upasuaji? Na je kumuondoa daktari huyu Bingwa ndio suluhisho la tatizo au ni kutengeneza tatizo zaidi?
Akiwa eneo la mlandege aliamuru Diwani wa viti maalumu wa Chadema awekwe mahabusu masaa48 na kutoa maneno ya kuudhi, kashfa na vitisho kwamba “usiniudhi mimi ni mtu hatari” kauli na matendo haya ni kinyume na mamlaka ya mkuu wa mkoa kama ilivyo ainishwa katika kifungu namba 7(1)-(3) cha sheria ya Tawala za Mikoa sheria No 19 ya 1997. Hivyo hapaswi kuishia kujua tu kuwa ana mamlaka ya kumweka mtu masaa48 isipokua awe na uwezo wa kufikri kosa lipi linafaa kwa kifungu hicho? Baada ya kumweka mtu masaa 48 yeye kama RC anapaswa kufanya nini? Kinyume na hapo ni matumiz mabaya ya madaraka.
Ndugu waandishi wa habari kiongozi wa kweli huwa na mtazamo wa kuwajali binadamu wote waishio ulimwenguni na hawi na mtazamo finyu usioona mbali katika mambo mbalimbali yanayo husu jamii na uongozi, kwani huwezi kufurahishwa mtumishi wa chini yako anapozomewa na wananchi halafu ukitegemea mtu huyo kesho amhudumie mwananchi aliyemcheka jana unapomtweza utu wake hadharani.
Matumizi mabaya ya fedha.
Gharama za misafara na matumizi ya ziara hizi ni makubwa kwa sababu kwanza, ana msafara wa magari mkubwa ambao unazidi hata misafara ya mawaziri, lakini pia kuna ulipanaji wa posho hata katika mazingira ambayo hayastahili kulipwa posho. Kwa Iringa mjini peke yake Mkuu wa Mkoa ametumia takribani sh 40 million fedha za halmashauri.
HITIMISHO
Kama mwakilishi wa wananchi naamini kwamba kuna umhimu wa ziara za kiutendaji kufanyika lakini hazipaswi kuwa za kisiasa, zenye kutafuta umaarufu binafsi na zisizo kuwa na tija zaidi ya kuumiza wananchi kupitia halmashauri zinazo gharamikia ziara hizo.
Mch. Peter Msigwa
Mb. Iringa Mjini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment