Wednesday, November 29, 2017

Lema: Mh Rais, kwenye Uchaguzi wa Madiwani tumeshuhudia nguvu ya dola, siamini kama ni Tanzania kwa Uchaguzi wa aina hii


Mh. Rais nakusalimu.

Uchaguzi wa marudio viti vya udiwani umekwisha, tumeshuudia nguvu ya dola kwa dhati kabisa nimeona kila kitu kilichotokea na bado siamini kama ni Tanzania kwa uchaguzi wa aina hii.

Mh. Rais, kuibiwa kura ni tofauti na kuporwa ushindi, huku kwetu Arusha huu sio wizi wa kura huu ni unyang,anyi wa kura, watu wameona na kushuudia ukatili wa ajabu wa Polisi na wasimamizi katika uchaguzi huu kwa kweli nimeumia sana kuliko wakati wote wa maisha yangu kwani ninatafakari ni wapi Nchi yangu inakwenda? Kwa namna hii wasiwasi mkubwa nilio nao ni maamuzi ya watu katika mioyo yao sioni kana kwamba watu hawa watalia tu bila kutafakari hatima yao, kwa namna nilivyoona ni dhahiri niseme kuwa Tanzania hakuna tena uchaguzi.

Matendo haya ya kwenye uchaguzi huu wa jana yameharibu fikra za watu wengi juu ya hatima ya Nchi yao na uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama vimetekeleza wajibu huu wa uporaji ushindi kwa nguvu zote. Kwa mfano, huko Meru na katika kata ya Muriet, wakala aliyekataa kutoka nje wakati wa zoezi la kuhesabu kura, kwa kweli alipata shida sana, wakala wetu kijana mdogo Edwin alipigwa vibaya na wasimamizi wa Tume alipokataa kutoka nje ya kituo cha kura baada ya kulazimishwa kutoka nje. Lakini pia nilishuhudia kwa macho yangu wakala wetu kijana Nuhu akitolewa kwenye kituo na askari kwa nguvu na kudhalilishwa sana, nilitamani nishuke nimsaidie lakini niliingiwa hofu kwani nilikuwa na taarifa mbaya zilizopangwa juu ya maisha yangu.

Mh. Rais, hekima inalia sana, mioyo ya watu wote walioshuhudia huu uchaguzi ni maoni yangu kuwa sasa bila shaka wanatafakari namna nyingine ya kupata viongozi wao, kwa vile ni dhahiri kuwa Uchaguzi hauna uhakika ya kutoa nafasi ya watu kuamua. Je, unafikiri ni nini itakuwa hatma ya Tanzania baadae?

Mh. Rais, kama huu ni mkakati wa kumaliza Upinzani, pengine mkakati huu unaweza kufanikiwa, lakini Nchi haiwezi kuwa salama hata kidogo. Hapa ndipo napata mashaka hivi kweli mtoto wangu na wajukuu zako wataishi vipi katika Taifa kama hili? Ni uhakika kwamba Polisi na hata Tume waliofanikisha zoezi hili miongoni mwao baada ya jana watakuwa miongoni mwa watu ambao wanatafakari sana kuhusu hatima ya Nchi yao.

Mh. Rais, CCM kushangilia ushindi huu ni fedheha na kejeli kubwa kwa Mungu, lakini kwa vile tulifundishwa tukiwa wadogo kuwa Mungu anaishi mbinguni basi bila shaka Mungu atakuwa anaanda safari ya kuja huku kwetu Tanzania hivi karibuni. Uchaguzi huu umeongeza chuki na uadui mkubwa sana miongoni mwa jamii. Mtu anawezaje kusema anaipenda Nchi yake na kuacha mambo kama haya yatokee?

Mh. Rais, nimekusikia mara nyingi ukimtaja Mungu kinywani mwako, kama kweli ni huyu Mungu wa kweli aliye umba mbingu na Nchi ni sahihi nikisema huyu Mungu hawezi kuruhusu wala kuvumilia mambo kama haya yafanyike. Watu wamepigwa, wamekatwa mapanga na fedhea mbali mbali, hakika damu itanena tu.

Mh. Rais, ninakuomba kuchukua tahadhari sana na watu wanaosema kila kitu ndio mzee, hawa ni maadui zako na Nchi yako. Huko Zimbabwe pia walikuwepo kwa Mugabe, lakini tumeshuhudia Watu wale wale walivyokuwa wa kwanza kusema Mugabe asulubiwe.

Mh. Rais, ninao uhakika kwamba kila jambo lina wakati wake, ni busara kila nyakati ikatumiwa kwa busara, kwani nyakati ni mbegu na maandiko yanasema “Mungu hadhihakiwi, apandacho Mtu ndicho avunacho”. Sasa uchaguzi huu umekwisha kwa namna hii watu wote wakiwemo vyombo vya ulinzi na usalama waliioshiriki ktk uchaguzi huu waeona ukatili mkubwa dhidi ya haki na maamuzi ya watu katika chaguzi.

Mh. Rais, nimalizie kwa kusisitiza kuwa, hiki kilichotokea katika uchaguzi huu wa marudio ni hatari kwa usalama wa Nchi, sitatajii kuamini kwamba nitaeleweka kwa ujumbe huu, sasa mpango wa kuondoa kwenye nafasi zao viongozi mbali mbali Nchini utaendelea kwa namna na njia yoyoye ile kwani wana uhakika kuwa wakirudi kwenye uchaguzi watatangazwa washindi.

Mh. Rais, hatuwezi kuvunjika moyo hata kidogo na siku zote tunaimarika kutokana na matatizo na changamoto, tunayo fursa sasa ya kufikiri kwa dhati ni nini hatima ya Tanzania na uchaguzi. Bila shaka sasa wananchi tutaanza kudai Katiba huru kwa nguvu zote na haya ndio madai yetu ya msingi kwa wakati huu kuliko jambo lolote, najua sasa Watanzania watakuwa tiyari, bila Katiba na Tume huru Tanzania hakuna Tume ya uchaguzi bali kuna tume ya uporaji wa uchaguzi.

Mh. Rais, tafadhali naomba utafakari maneno haya aliyosema mfalme Sulemani kutoka katika kitabu cha Mithali. "Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu"

Mungu akubariki sana.
ONLY TIME WILL TELL.

Godbless J Lema (MB)

No comments:

Post a Comment