Friday, October 6, 2017

UCHAGUZI WA UMOJA WA MADIWANI CHADEMA TAIFA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI- UCHAGUZI WA UMOJA WA MADIWANI CHADEMA TAIFA

Tunatoa taarifa kuwa muda wa kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uenyekiti, ukatibu, mnadhimu, mweka hazina na mratibu wa mawasiliano na uhusiano wa Umoja wa Madiwani wa CHADEMA Taifa, umeongezwa hadi tarehe 30 Oktoba, 2017.
Fomu zinapatikana kwenye ofisi zote za Kanda za Chama , Mikoa na Wilaya. Wenye sifa ya kugombea nafasi hii ni Madiwani wote wa kuchaguliwa na Viti Maalum isipokuwa Mameya na Wenyeviti wa Halimashauri pamoja na Manaibu na Makamu wao hawatakuwa na sifa za kugombea nafasi hii.

Fomu zote zinatakiwa kufika Makao Makuu ya Kanda ifikapo saa 10.00 jioni ya tarehe 30 Oktoba, mwaka huu.
Kwa wale wote ambao walishachukua na kurejesha fomu hawatatakiwa kujaza fomu upya.

Kwa ajili ya kuweka uratibu mzuri baina ya madiwani na chama katika utendaji wa kila siku, Chama kupitia Katiba yake, kiliweka nafasi ya madiwani kuwakilishwa moja kwa moja katika vikao vya maamuzi kuanzia ngazi za chini hadi ngazi ya taifa.

Umoja huu umeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama ibara ya 9.5.6; "Kutakuwa na Umoja wa Madiwani wa CHADEMA nchini ambao utakuwa na Uongozi, vikao na kuendeshwa kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Baraza Kuu la Chama."

Kwa mujibu wa Katiba hiyo, ibara ya 7.7.14 (O), Mwenyekiti na Katibu wa Umoja huu watakuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama.
Utaratibu huu unawawezesha madiwani wa chama kuwa na uwakilishi wa moja kwa moja na sauti zao kusikika kwenye vyombo vya maamuzi vya Chama kupitia kwa viongozi waliochaguliwa na madiwani wenyewe.

Tunawatakia Maandalizi mema wale wote wenye nia ya kugombea nafasi hizo.

Imetolewa leo tarehe 05 Octoba, 2017 ;
John Mrema
Mkurugenzi Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje - CHADEMA


No comments:

Post a Comment