Friday, October 6, 2017

NYONGEZA YA MISHAHARA KWA WATUMISHI SIO HISANI YA RAIS!

Mnamo Septemba 5, mwaka huu, akijibu swali namba 3486, nililouliza bungeni kwa niaba ya watumishi wote nchini, hususani wale ninaowawakilisha mkoani Mwanza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, alikiri mbele ya umma masuala kadhaa ambayo ni vyema yakaendelea kuwa katika kumbukumbu sahihi kwenye mjadala unaoendelea nchini sasa kuhusu madai ya ongezeko la mshahara kwa watumishi nchini.

1. Alikiri kuwa Serikali haiajiri (bila shaka pamoja na ongezeko la stahili za waajiriwa hao) kwa utashi wa Rais.

2. Serikali imeshatenga bajeti, kupitia mwaka wa fedha wa 2017/18 (kwa ajili ya kutekeleza takwa la kisheria) kuongeza mishahara kwa watumishi nchini.

Katika swali langu la msingi niliitaka Serikali kutoa kauli kwa watumishi wa umma waliokuwa wameajiriwa tayari na kusainishwa mikataba ya ajira serikalini kabla Rais John Magufuli hajatoa kauli ghafla kusitisha ajira serikalini kupisha kile kilichoitwa zoezi la ukaguzi wa vyeti hewa.

Aidha niliitaka Serikali itoe kauli iwapo inatambua kuwa watu hao tayari walikuwa ni watumishi na mchakato wa kuwaingiza kwenye payroll ulishaanza lakini ukasitishwa ghafla na sasa wako mtaani na hawajui hatma yao.

Katika majibu yake kwa swali hilo la msingi, Serikali ilisema kuwa watumishi hao waliosimamishwa mwezi Mei, walisharejeshwa kazini, wanaendelea na majukumu yao, kulipwa mishahara yao na ikasema kuwa wanatambulika kama watumishi serikalini. Pengine majibu ya serikali kwa maswali ya nyongeza ndiyo yaliibua mkanganyiko mkubwa zaidi na yanaweza kuhusika zaidi katika mjadala huu unaoendelea sasa;

Katika maswali mawili ya nyongeza, nilitaka Serikali lini itaondoa dhana zinazoanza kujengeka nchini (kuhusu ajira) kuwa;

(i)hadi sasa imeshindwa kuajiri kwa sababu haina hela

(ii) serikali inaajiri kwa utashi wa Rais badala ya mahitaji yaliyopo pamoja na matakwa ya kisheria.

Swali la pili la nyongeza lilitaka Serikali ieleze kwanini haipandishi madaraja (mishahara) ya watumishi kama sheria zinavyoelekeza.

Ilikuwa wazi kuwa Serikali haikuwa imejipanga kwa mazuri ya uhakika. Lakini kupitia waziri husika ambaye kwa kiasi fulani alipata shida kujibu maswali hayo, Serikali ikatoa kauli bungeni kukanusha kuwepo kwa zile dhana mbili nilizozitaja hapo juu, lakini pia ikatoa kauli kuwa imeshapanga bajeti ya nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma nchini.

Wananchi, hasa watumishi wanaoamini kuwa uwajibikaji wa pamoja wa kiserikali, waliichukulia kauli ile ya serikali ndani ya bunge kuwa mathubuti, ikisubiri utekelezaji tu. Kumbe haikuwa hivyo! Kauli za juzi za Rais Magufuli wakati akifungua mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (ALAT), kwamba hatapandisha wala hana mpango wa kupandisha mishahara ya watumishi nchini, si tu kwamba zimesababisha mkanganyiko mkubwa wa kauli zake mwenyewe zinazokinzana akizitoa kwa nyakati tofauti katika jambo hilo hilo, lakini pia zimepeperusha mbali matumaini kidogo yaliyoanza kurejea kwa watumishi baada ya majibu yaliyotolewa bungeni.

Inastaajabisha na kusikitisha! Kupitia taarifa hii kwa vyombo vya habari na umma wa Watanzania, kwa dhima ile ile, kwa niaba ya watumishi wote nchini, hususani wale wa Mkoa wa Mwanza ambao ninawajibika kuwawakilisha na kuwasemea, napenda kusema;

1. Kauli hiyo ya juzi ni ishara ya mambo mengi ikiwa ni pamoja na;

(i) Dharau kwa mhimili wa Bunge, dharau kwa watumishi nchini, dharau kwa wananchi.

2. Kwamba nyongeza ya mishahara kwa watumishi inatolewa kwa hisani au kadri rais anavyojisikia.

3. Kauli ya serikali iliyotolewa bungeni haikuwa kweli. Kutokana na hayo, naomba kutoa wito kama ifuatavyo;

1. Wito kwa watumishi wote wa mkoani Mwanza wakishirikiana na wenzao wengine nchi nzima, kupitia vyama na jumuia zao mbalimbali, kusimama kidete kupinga kauli na ulaghai wa serikali kuhusu stahili zao. Watetee haki zao, hasa hii ya nyongeza ya mshahara, bila kuogopa!Mapambano ya kupigania haki za wafanyakazi duniani kote ni sehemu ya mapambano ya kitabaka.

2. Ni muhimu serikali yetu, kama ilivyo sehemu zingine duniani, itumie lugha ya kistaarabu na staha hasa kupitia njia za majadiliano ya mezani kufikia mwafaka katika kutatua matatizo ya wafanyakazi na kada zingine katika jamii.

3. Wananchi na makundi mengine katika jamii kusimama pamoja na wafanyakazi dhidi ya unyanyasaji huo ambao ni kinyume na sheria zetu, kwa sababu sasa inazidi kudhihirika kuwa hakuna kundi liko salama au litabaki salama kwenye mikono ya utawala usiozingatia Katiba na kukiuka sheria za nchi. Kwa sababu inaonekana kauli iliyotolewa bungeni kuhusu nyongeza ya mishahara haikuwa kauli inayotokana na mipango au uwajibikaji wa pamoja wa serikali yetu, basi mambo matatu yafuatayo yafanyike;

1. Bunge letu liitake serikali iwajibike bungeni kuhusu kauli (commitment) hiyo ambayo sasa ni dhahiri kuwa haikuwa ya kweli.

2. Waziri Angela aone umuhimu wa kuwajibika, kwa ama kutoa kauli isiyokuwa ya kweli bungeni au kwa sababu kauli yake hiyo (iwapo ilikuwa ya kweli) imekanushwa hadharani tena na mkuu wake wa kazi. Kanuni ya msingi ya utawala bora inamuondolea uhalali wa kuendelea kuwa sehemu ya timu ya serikali.

3. Kama waziri husika alitoa kauli hiyo bila kuwa imetokana na uwajibikaji wa pamoja katika Baraza la Mawaziri au mipango ya serikali, basi Rais amfukuze kazi waziri huyo mara moja kwa kutoa kauli isiyokuwa ya kweli tena bungeni.

Susanne Maselle Makene Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mwanza

No comments:

Post a Comment