TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU KAULI TATA ZA RAIS JOHN MAGUFULI LEO KWA WAFANYAKAZI
Wananchi wengi waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya hotuba ya Rais John Magufuli leo kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari wakati akihutubia mkutano wa Jumuia ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (ALAT), wamesikitishwa, kama ambavyo sasa inaanza kuzoeleka na kuwa kawaida, na kauli zilizotolewa na Rais kwa taifa bila kupima athari kubwa na hasi katika utekelezaji wa sheria za nchi, uzingatiaji wa taratibu za uendeshaji nchi na misingi ya demokrasia na utawala bora.
Pamoja na wananchi kushangazwa na kauli nyingi zilizotolewa na Mhe. Rais Magufuli, chama tumeshangazwa zaidi na kiongozi huyo mkuu wa nchi kuamua kuonesha 'double standards' kwa kiwango cha juu, jambo ambalo ni litazidi kuzua maswali mengi, ikiwa ni pamoja na, je Rais anaujua vyema unyeti na uzito wa nafasi aliyonayo?
Katika mkutano huo Rais Magufuli amesikika akimsifia kwa uchapa kazi mtu anayeshikilia nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa, kiasi cha kwenda mbali na kusema kuwa yeye Rais hajali hata kama watu wanasema huyo Mkuu wa Mkoa hajasoma, kwani kwake (Rais) hata kama angekuwa hajui kusoma 'A', kukamata dawa za kulevya inatosha kuwa usomi.
Kauli hiyo pamoja na kutolewa kwa maneno machache, imekuwa na mwangwi hasi mkubwa katika maeneo tuliyotaja hapo juu; hadhi ya urais, utii wa sheria, uzingatiaji wa taratibu za kuendesha nchi na misingi ya demokrasia na utawala bora.
Kauli hiyo ambayo inaonekana imetolewa kama kujibu makombora ya tuhuma anazoelekezewa Mkuu wa Mkoa huyo kwa muda mrefu sasa bila kuwepo na ufafanuzi wowote, kuhusu utata wa elimu yake na majina anayotumia, imeibua mtanziko mkubwa katika masuala yafuatayo;
1. Uhalali wa agizo la Rais Magufuli kuwafukuza watumishi wa umma wanaodaiwa kuwa na vyeti feki
Itakumbukwa kuwa miezi ya awali mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alitangaza zoezi la kukagua vyeti vya watumishi wa umma, ambalo hatimae lilisababisha Rais kutoa agizo la kufukuzwa kazi kwa takriban watu 90,000 waliokuwa watumishi wa serikali, bila kufuata taratibu za sheria. Maumivu na machozi ya matokeo ya zoezi hilo hayajaisha wala kukauka miongoni wa waathirika na Watanzania wengi kwa jumla. Je Rais anajua kuwa kauli yake ya leo kuonesha kuwa 'vyeti' si suala muhimu, ameondoa uhalali wowote ule uwe wa kisheria au wa kisiasa wa agizo lake la kuwafukuza watumishi wale waliodaiwa kutokuwa na vyeti? Je anajua ametonesha vidonda ambavyo havijapona?
2. Uhalali wa kauli ya Rais Magufuli kuwa Serikali yake hailei 'vilaza'
Mnamo mwezi Juni mwaka huu, Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa Serikali yake haiwezi 'kulea' vilaza (kwa maana ya watu wasiokuwa na sifa stahili) akizungumzia sakata la wanafunzi vijana waliokuwa wamedahiliwa kusoma programu maalum ya ualimu katika Chuo Kikuu cha UDOM. Je Rais Magufuli anajua kuwa kauli yake ya leo inaonesha kuwa hakuwa na nia ya dhati kupinga 'vilaza' kwenye serikali yake? Na kwamba hakuwa mkweli kwa sababu wapo vilaza anaowatetea?
3. Kauli ya Rais Magufuli na shauri lililoko Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Baada ya madai ya utata wa majina anayotumia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama na elimu yake kutopatia majibu wala ufafanuzi, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, aliamua kufungua shauri mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili mamlaka hiyo ishughulikie suala hilo kwa kadri ya Sheria za nchi na kumaliza utata uliopo.
Lakini katika hali ya kushangaza leo, Rais Magufuli amenukuliwa akitoa kauli katika namna ambayo inamsafisha mkuu huyo wa mkoa na hivyo kuingilia shauri huku maoni yake yakielekea kuweka ushawishi na kuelekeza hukumu.
4. Rais kutoa kauli mbili zinazokinzana kuhusu haki ya kisheria ya nyongeza ya mishahara kwa watumishi
Wakati wa Sikukuu ya Mei Mosi, mwaka huu, Rais Magufuli alinukuliwa akikiri kuwa serikali yake haijatekeleza agizo la kisheria la kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wake. Akatoa ahadi kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2017/2018, wafanyakazi wataongezewa mishahara.
Katika hali ya kushangaza, leo Rais Magufuli katoa kauli inayokinzana na kauli ya Mei Mosi, ambapo amenukuliwa akisema kuwa hajapandisha mshahara wala hana mpango wa kupandisha mshahara kwa sababu bado anataka kuwaletea wananchi maendeleo.
Hitimisho
Ni wazi kuwa kauli hizi za Rais Magufuli, kama ilivyo kwa kauli zake zingine ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara, zinaendelea kujenga ombwe la kiuongozi ndani ya nchi na kuongeza maumivu na machungu badala ya kuleta faraja na matumaini.
Tutumie nafasi hii kuwapatia pole za dhati wafanyakazi wote nchini kwa kauli hii ya leo, ambayo inaweza kuvunja ari yao ya kazi na kuwakatisha tamaa. Tuwakumbushe tu kuwa mapambano ya wafanyakazi ni jambo endelevu na nyongeza ya mshahara ni haki yao kisheria. Haitolewi kwa hisani au mapenzi ya kiongozi yeyote yule.
Aidha, tunapenda kumkumbusha Rais Magufuli kuwa amekuwa akisikika akitumia maneno kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge, ni vyema akajua kuwa miongoni mwa wanyonge ni pamoja na wafanyakazi hao wanaoomba kuongezewa kima cha chini cha mshahara.
Imetolewa leo Jumanne, Oktoba 3, 2017 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment