Wednesday, October 25, 2017

TAARIFA KUTOKA CHADEMA MKOA WA ILALA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
OFISI YA MKOA WA ILALA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI​


Ndugu waandishi wa habari na wananchi mliohudhuria mkutano huu wa Waandishi wa Habari ulioandaliwa na CHADEMA Mkoa wa Ilala, habari zenu za asubuhi. Kwanza niwashukuru kwa kuitikia wito wetu wa kuhudhuria Mkutano huo.

Sababu ya kuwaita ndugu waandishi wa habari ni kutoa taarifa ya maamuzi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Ilala wa kwenda Mahakamani kusimamisha kufanyika kwa Uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Ilala uliopangwa kufanyika tarehe 12/11/2017.

Tumeamua kuchukua hatua hii ngumu kwa sababu za msingi, kwani tumeona kwamba Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Ilala anataka kufanya hujuma za makusudi kwa kupanga Ratiba ya Matukio ya Uchaguzi ambayo siyo rafiki, iliyoficha nia mbaya na ambayo inakwenda kinyume kabisa na Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2014, Kanuni ambazo zimetungwa chini ya Kifungu Na. 87A ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura 288. Na kwa uzoefu wetu, hujuma kama hizi za vyombo na watu wa dola kama wasimamizi wa uchaguzi, hufanywa kuumiza vyama vya upinzani, hususan CHADEMA.

Tutaeleza hapa chini matukio yaliyojitokeza toka Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi) wa Manispaa ya Ilala alipotoa Ratiba ya Matukio ya Uchaguzi huo mdogo.

1. Tarehe 16/09/2017, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Ilala aliita Kikao cha wadau kuhusu kusudio la kufanya uchaguzi na ratiba ya uchaguzi. Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, ratiba ya matukio ya Uchaguzi mdogo mwaka 2017 ilitolewa na kujadiliwa.

2. Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wa CHADEMA walitoa dukuduku zao kuhusu tarehe za baadhi ya matukio ya uchaguzi huo, zikiwemo tarehe za kubandika orodha ya awali ya wapiga kura, pingamizi kwa kwa waliojiandikisha kupiga kura na kutoa maamuzi ya pingamizi hizo. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, matukio yote hayo yalipewa siku mbili tu, ambazo wawakilishi wa CHADEMA katika kikao hicho cha wadau waliona ni chache mno kwa mujibu wa Kanuni na uhalisia, na wakaomba zirekebishwe. Hata hivyo Msimamizi wa Uchaguzi alipuuzia hoja hizo.

3. Baada ya kupitia tena Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2014, na kuthibitisha hoja za wawakilishi wetu kwenye kikao cha wadau tajwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Ilala, kiliandika barua tarehe 09/10/2017 yenye Kumb. Na. CDM/ILALA/MANISPAA/2017/01, kikiitaka Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya marekebisho ya haraka ya kasoro zilizopo kwenye ratiba ya matukio ya uchaguzi na kujulisha wadau wote wa Uchaguzi mapema iwezekanavyo. Kasoro hizo ni kama ifuatavyo:-

a) Kwa mujibu wa Ratiba hiyo, Uandikishaji wa wapiga kura ulipangwa kufanyika kwa siku saba (7) kuanzia tarehe 15/10/2017 hadi tarehe 22/10/2017, na baadaye kurekebishwa kwamba uandikishaji utaanza tarehe 22/10/2017 hadi 29/10/2017. Hata hivyo, kwa mujibu wa Ratiba hiyo, orodha ya awali ya wapiga kura itabandikwa tarehe 06/11/2017 (siku 6 tu kabla ya Uchaguzi)! Kwanza, CHADEMA tukataka kujua kwa nini Orodha hii ya awali ya wapiga kura ikamilike tarehe 22/10/2017, lakini ichukue siku 15 kuibandika (06/11/2017). Hata baadaye walipobadilisha kuonyesha kwamba uandikishaji utakamilika tarehe 29, bado itachukua siku 8 kabla ya kubandika orodha ya awali. Pili, na muhimu, hatua hii ya kuchelewesha kubandika orodha ya awali ya wapiga kura inasababisha kukiukwa kwa baadhi ya vifungu vya Kanuni za Uchaguzi huu kutokana na kutokuwepo kwa muda wa kutosha, kama inavyoelezwa hapa chini.

b) Kifungu cha 9(7) cha Kanuni kinatamka ifuatavyo: Mkazi yeyote wa Mtaa au vyama vya siasa vitakuwa na haki ya kukagua katika muda wa siku kumi tangu tarehe Orodha ya wapiga kura ilipobandikwa mahali pa Matangazo ya Uchaguzi ili kutoa maoni juu ya usahihi wa Orodha hiyo na anaweza kuomba

i. Orodha irekebishwe kwa kuongeza jina lake au jina la mkazi; au

ii. Orodha irekebishwe kwa kufuta jina lililoorodheshwa kwa vile aliyeorodheshwa hana sifa ya kupiga kura katika kila Mtaa husika.

c) Kifungu cha 9(8) kinaeleza: Pingamizi dhidi ya mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura litawasilishwa kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ambaye atalitolea uamuzi na kurekebisha Orodha ya wapiga kura iliyotangazwa katika muda wa siku tano kuanzia tarehe ya kuwasilishwa pingamizi hilo.

d) Kifungu cha 9(9) kinaeleza: Mtu yeyote au chama cha siasa ambacho hakitaridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kitawasilisha rufaa kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ataishughulikia rufaa hiyo katika muda wa siku tano baada ya kupokea rufaa hiyo.

4. Kwa maelezo hayo juu, CHADEMA ilimjulisha Msimamizi wa Uchaguzi kwamba mchakato ulioelekezwa na vifungu vya 9(7), 9(8) na 9(9) ya Kanuni za Uchaguzi unahitaji siku ishirini (20) toka tarehe ya kubandika Orodha ya awali ya wapiga kura hadi maamuzi ya rufaa ya Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu Orodha hiyo ya wapiga kura, na siyo siku mbili (2) kama Ratiba yake inavyoonyesha.

5. Katika barua yetu hiyo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala (Msimamizi wa Uchaguzi) tulisisitiza kwamba ni lazima muda wa kutosha utolewe kwa wapiga kura na vyama vya siasa kukagua Orodha ya Wapiga Kura na kuweka pingamizi na kuwapa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi na baadaye Msimamizi wa Uchaguzi muda wa kupitia pingamizi na kutoa maamuzi kwa mujibu wa Kifungu cha 9(7), 9(8) na 9(9) za Kanuni za Uchaguzi huo. Ili kwenda na muda, tuliomba Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi ifanye marekebisho haya mara moja.

6. Lakini licha ya tarehe hizo za kubandika orodha ya awali ya wapiga kura, CHADEMA tuliona kasoro nyingine katika ratiba ya tarehe ya kurejesha fomu za wagombea na tarehe ya uteuzi. Kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (1) Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti na ujumbe wa Kamati ya Mtaa siku zisizopungua ishirini kabla tarehe ya Uchaguzi. Kifungu cha 13 (2) kinasema kwamba Siku ya uteuzi, wagombea watawasilisha fomu za uteuzi kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kabla ya saa kumi kamili jioni baada ya hapo fomu hazitapokelewa ili kuruhusu kufanyika kwa uteuzi wa wagombea kutokana na fomu zilizowasilishwa. Na kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (3) Saa ya uteuzi itakuwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na dakika kumi na tano jioni siku ya uteuzi. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, uteuzi unafanyika siku ile ile ya mwisho ya kurejesha fomu. Lakini kwa mujibu wa ratiba ya matukio iliyotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi tarehe ya mwisho kurejesha fomu za wagombea ni 21/10/2017, wakati tarehe ya Uteuzi ni 23/10/2017. CHADEMA tunajiuliza kwanini Msimamizi wa Uchaguzi akae na fomu kwa siku mbili baada ya siku ya mwisho ya kurejesha fomu hadi siku ya uteuzi, kinyume na Kifungu 13 (2) cha Kanuni za mwaka 2014?

7. Hata hivyo hadi jana tarehe 16/10/2017 (siku 7 baada ya barua yetu tajwa), Msimamizi wa Uchaguzi ameshindwa kufanya marekebisho kwenye ratiba kama tulivyoomba na ilivyo kwenye Kanuni.

8. Wakati Msimamizi wa Uchaguzi akishindwa kutujibu au kufanya marekebisho ya ratiba, tarehe 11/10/2017 aliandika barua kwa wadau kutangaza kwamba fomu za kugombea uongozi kwenye uchaguzi huo zitaanza kutolewa na kurudishwa kuanzia jana tarehe 16/10/2017 jana hadi tarehe 21/10/2017, kabla ya kufanya marekebisho ya msingi kwenye ratiba ambayo CHADEMA tuliomba na tunaona ni ya msingi sana ili mchakato wa uchaguzi ufuate sheria za nchi.

9. Kutokana na kasoro hizo muhimu, CHADEMA tunadhani kuna njama za kutaka kuhujumu Uchaguzi huu kupitia Ratiba ya Uchaguzi isiyo rafiki na isiyozingatia Kanuni za Uchaguzi, na kwa kuwa Msimamizi wa Uchaguzi ameshindwa kujibu malalamiko yetu au kurekebisha ratiba hiyo, jana tarehe 16/10/2017 tumemwandikia barua yenye Kumb. CDM/ILALA/MANISPAA/2017/02, tukimweleza kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Ilala, tumeamua yafuatayo:-

a) CHADEMA hatuwaruhusu wagombea wetu kurudisha fomu za kugombea katika zoezi lililoanza jana tarehe 16/10/2017 hadi 21/10/2017, na badala yake,

b) CHADEMA itakwenda Mahakamani kusimamisha Uchaguzi huu mdogo usifanyike katika Manispaa ya Ilala kama ilivyotangazwa kwenye Ratiba yake hiyo, na kwamba Ofisi yetu tayari imeelekeza Wanasheria wetu wachukue hatua za kusimamisha Uchaguzi huu Mahakamani kama malalamiko yetu hayatafanyiwa kazi na kurekebishwa kufikia kesho tarehe 18/10/2017.

MWISHO: Ndugu waandishi wa habari, hizo ndizo sababu zilizoifanya CHADEMA kuamua kwenda Mahakamani kusimamisha Uchaguzi wa tarehe 12/11/2017, na tulitaka waandishi wa habari pia mzijue na kuwataarifu wananchi wa Tanzania, wananchi wa Manispaa ya Ilala, na hususan wanachi wanaotakiwa kufanya uchaguzi huo kwenye mitaa 13.

Asanteni sana!

Imetolewa kwa niaba ya CHADEMA Mkoa wa Ilala, na

Dr. Milton Makongoro Mahanga

MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA ILALA

No comments:

Post a Comment