Wednesday, October 25, 2017

SERIKALI YA RAIS MAGUFULI HAINA MAMLAKA YA ‘UHAKIMU’ KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI


SERIKALI YA RAIS MAGUFULI HAINA MAMLAKA YA ‘UHAKIMU’ KUFUNGIA VYOMBO VYA HABARI
Uamuzi wa Serikali ya Rais John Magufuli wa kulifungia gazeti la kila siku la Tanzania Daima, kinyume cha sheria za nchi, ni mwendelezo wa vitisho na mashambulizi dhidi ya uhuru wa habari na vyombo vya habari, hali ambayo ikiachwa iendelee bila kukemewa na kupingwa itazidisha sintofahamu kubwa inayoendelea nchini kuhusu kupuuzwa kwa taratibu za kuongoza nchi.

Nikiwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, yenye wajibu mkubwa wa kuwa mlezi na msimamizi mwenye sura rafiki wa tasnia hii nyeti, natumia fursa hii kusema yafuatayo; 

1. Kulaani na kupinga vikali hatua hiyo ya Serikali kuendeleza tabia iliyo kinyume kabisa na misingi ya utoaji haki, yaani kuwa mlalamikaji, kukamata, kufungua mashtaka, kuendesha mashtaka na kuwa hakimu/jaji wa kesi yake mwenyewe. Hii pia haikubaliki katika misingi ya utawala bora unaozingatia sheria.

2. Serikali imetumia vibaya na kimakosa Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016, kulifungia Gazeti la Tanzania Daima. Kifungu cha 54(1) cha Sheria hiyo kilichotumiwa na Serikali ya Rais Magufuli kuadhibu chombo hicho cha habari, hakitoi mamlaka YOYOTE kwa Serikali kuchukua hatua iliyochukua jana. Kutokana na msingi huu, Serikali ifikirie upya uamuzi huo na iubatilishe mara moja na kuvifungulia vyombo vingine ambavyo vimefungiwa.

3. Kitendo cha Serikali kutumia vibaya na kimakosa sheria hiyo, kinadhihirisha kuwa uamuzi huo umesukumwa na chuki na nia ovu dhidi ya gazeti hilo.

4. Aidha, hatua hiyo ambayo iko kinyume na sheria hiyo iliyotumika, ambayo imechukuliwa siku moja tu baada ya Rais Magufuli kusikika akitoa maelekezo akiwa Ikulu, imetulazimisha kuamini kuwa hatua za kufungia vyombo vya habari tangu Rais Maguli aingie madarakani, zinachukuliwa ili kufurahisha utashi, matamanio na matakwa binafsi ya Rais Magufuli.

Hitimisho
Ni vyema Rais Magufuli aache mwenendo wake na Serikali yake wa kutisha, kushambulia na kudhibiti vyombo vya habari, waandishi wa habari na uhuru wa habari kwa ujumla, kwa kila jambo ambalo liko kinyume na matendo, kauli, matamanio, matakwa, fikra, mawazo na maoni yake.

Tunatoa wito kwa wadau wa habari ambao ni Watanzania wote kusimama kidete, wapaze sauti kwa njia zozote kutetea uhuru wa habari nchini na kupinga vikali kauli na vitendo vya Rais wetu dhidi ya vyombo vya habari, hasa kuvifungia, jambo ambalo linaathiri waandishi wa habari wote katika chombo husika, wafanyakazi wengine na familia zao.

Kwa sababu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inayotumiwa kufungia vyombo vya habari haitoi mamlaka hayo kwa Serikali, tunasisitiza tena kuitaka Serikali ivifungulie vyombo vyote vya habari vilivyofungiwa hadi sasa, ikiwa ni pamoja na magazeti ya Mseto, Mawio, Mwanahalisi, Raia Mwema na Tanzania Daima.

Joseph Mbilinyi (Mb)
Waziri Kivuli Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Oktoba 25, 2017
Dodoma, Bungeni

No comments:

Post a Comment