Saturday, September 9, 2017

TAMKO LA ZADIA KUHUSU KUSHAMBULIWA KWA MH. TUNDU LISSU.

TAMKO LA ZADIA KUHUSU KUSHAMBULIWA KWA MH. TUNDU LISSU.

Jumuiya ya Diaspora ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA) imepokea, kushtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kushambuliwa kwa mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Mh. Tundu Antipas Lissu kwa kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwake akitokea katika vikao vya bunge huko mjini Dodoma, Tanzania.

Kama jumuiya tunalaani vikali shambulio hili lenye kuashiria uharamia mkubwa na linaloweza kupelekea kutia doa sura ya taifa letu ulimwenguni kote kama linavyojulikana kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu.

Shambulio hili limewasikitisha na kuhuzunisha watu wengi wa rika na taaluma mbali mbali na kila mpenda amani, haki, na usawa ulimwenguni kote kwani ni shambulio la kiharamia lililodhamiria kumaliza uhai wa Mh. Tundu Lissu.
Shambulio kama hili limezoeleka kusikika katika nchi jirani na za mbali lakini sasa limeshatokea nyumbani kwetu na limepelekea kuleta mtafaruku mkubwa na kutia wasiwasi watu wengi hususan wanasiasa kutoka upande wa upinzani na kuanza kuhofia maisha yao na familia zao.

Ni matarajio yetu kwamba serikali na vyombo vyetu vya dola vitafanya kila juhudi iwezekanayo na kutumia rasilimali zetu tulizonazo katika kufanya uchunguzi wa kina, kuwatafuta, kuwatia hatiani, na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wahusika wote waliotenda shambulio hili la kiharamia.

Aidha, tunawanasihi wanajumuiya wote na wapenda amani wote popote pale walipo kuwa watulivu, kujiepusha na dhihaka na kukejeli na ikiwezakana kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika kufanikisha uchunguzi wa shambulio hili utakaopelekea kukamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria kwa maharamia hao waliotenda shambulio hili.

Mwisho, tunachukua nafasi hii kumuombea Mh. Tundu Lissu kwa Mwenyezi Mungu, amjaalie kupona haraka na kurudi katika hali yake ya afya na uzima ili aweze kurudi katika kufanya shughuli zake za kawaida pamoja na harakati za kutetea haki na usawa kwa jamii ya Watanzania. Pia tunawaombea amani na utulivu wa moyo na akili wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki zake wote na kila alieguswa na tukio hili.

Ahsanteni,
Uongozi wa ZADIA.

No comments:

Post a Comment