Friday, April 7, 2017

TAARIFA KWA UMMA YA KULAANI NA KUPINGA VIKALI VITENDO NA MANENO YA SPIKA WA BUNGE MHE. JOB NDUGAI JUU YA KILICHOFANYIKA UCHAGUZI WA EALA.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)




TAARIFA KWA UMMA YA KULAANI NA KUPINGA VIKALI VITENDO NA MANENO YA SPIKA WA BUNGE MHE. JOB NDUGAI JUU YA KILICHOFANYIKA UCHAGUZI WA EALA.

Siku ya tarehe 04.04.2017 kulifanyika uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambapo kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi huo kama lilivyochapishwa kwenye gazeti la serikali lilionyesha kuwa vyama vilivyokuwa na haki ya kuweka na kupata viti vilikuwa vitatu;

Vyama hivyo ni CCM (6), CHADEMA (2) na CUF (1) na hii ni kutokana na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ibara ya 50 ikisomwa pamoja na Kanuni za uchaguzi wa Bunge la EALA pamoja na Kanuni za Bunge la Jamhuri ya Muungano kama zitakavyoainishwa kwenye taarifa hii.

Kabla ya kufafanua misingi hiyo ya kikanuni inayosimamia uchaguzi wa EALA na kile kilichotokea Aprili 4, ni vyema kuweka wazi kuwa tunalaani na kupinga vikali kauli zilizotolewa na Spika wa Bunge Job Ndugai kwani zinapotosha, ni za kuudhi na zinalengo la kuligawa taifa katika misingi ya udini, maeneo (ukabila) na jinsi.

Tunapinga kwa nguvu zote kitendo hiki na vingine vya namna hiyo, vinavyolenga kutaka kuligawa taifa letu na tunawataka Watanzania wenye nia njema na nchi yetu kutafakari madhara ya kauli za Spika Ndugia na kuzikemea kwa nguvu zote.

Tunalaani na kupinga Maeneo yafuatayo;

1. Kwa kauli yake ya jana kuwa ni lazima CHADEMA izingatie mikoa katika kuwasilisha upya majina ya wagombea wa nafasi 2 za EALA ni sawa na kusema kuwa ameamua au ametengeneza vigezo vingine nje na Mkataba wa Afrika Mashariki, Sheria ya Uchaguzi wa Afrika Mashariki na Kanuni za Bunge.

Aidha anaposema kuwa tunatakiwa kuzingatia Mikoa anasahau kuwa CHADEMA ina viti 2 tu kati ya viti 9 na ambavyo kwa vyovyote vile wagombea wanaweza kupatikana kutokana sehemu yeyote ndani ya nchi yetu 2 na sio vinginevyo. Lakini pia kama kauli hiyo hatari ya Spika Ndugai ingelikuwa ni mojawapo ya kigezo, bado CHADEMA isingetoa watu zaidi ya mikoa miwili na hili tumelitekeleza kwa kuwasilisha majina ya Ezekia Dibogo Wenje (Mkoa wa Mara) na Lauwrence Kego Masha (Mkoa wa Mwanza).

2. Kuhusu majina ya CHADEMA kutakiwa kuzingatia jinsia; CHADEMA ina haki ya kupata nafasi mbili kati ya 9 kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge. Swali ni je, 1/3 ya viti viwili ingepatikanaje ili kukidhi jinsia? Au anapindisha kanuni kuwa kwa CHADEMA nafasi zinatakiwa sasa kugawiwa kwa misingi ya 50/50 ? Ila kwa vyama vingine hilo sharti halipo? Tunaamini Spika Ndugai anafanya mchezo huu wa kukiuka kanuni kwa makusudi kwa sababu, anajua kabisa kama Chama tunaweza hata kupeleka wanawake kwa asilimia 100 kwani kumbukumbu zilizopo tayari zinaonesha kuwa CHADEMA imekuwa ikitoa fursa sawa kwa jinsi zote hata ndani ya Bunge analoliongoza ushahidi upo wazi namna ambavyo CHADEMA ina asilimia kubwa ya wabunge wanawake kuliko hata chama chake cha CCM. Imani ambayo tunayo siku zote si katika EALA pekee
bali katika nafasi mbalimbali.

Aidha ieleweke pia wazi kuwa kigezo cha uwiano wa jinsia kinapimwa baada ya uchaguzi wa nafasi zote 9 kukamilika na si wakati wa mchakato na hiyo ndiyo 'spirit' ya kifungu cha 4(4) cha Sheria ya Afrika ya Mashariki.

3. Ieleweke pia kuwa Spika wa Bunge hatoi viti vya Ubunge wa Afrika Mashariki kama zawadi au kwa hisani yake binafsi. Viti vinatolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge kwa kuzingatia uwiano wa uwakilishi Bungeni na ndio maana mwaka 2012 CCM ilikuwa na viti 7 lakini mwaka huu wa 2017 ina viti 6. Hii maana yake ni kuwa uwakilishi wa CCM ndani ya Bunge umepungua baada ya uchaguzi mkuu wa 2015. Hivyo Spika kusema kuwa yeye ndio amewapa viti viwili CHADEMA ni kauli ya kuudhi na ya kupotosha umma kwani kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika Mashariki na Kanuni za Bunge CHADEMA ina haki ya uwakilishi katika EALA na si kutokana na huruma au mapenzi ya Spika au matakwa binafsi ya mtu mwingine yeyote.

4. Kuhusu CHADEMA kuweka wagombea wawili na kuwa na haki ya kupata viti viwili; utaratibu wa uchaguzi wa EALA unatakiwa kusimamiwa na taratibu za Bunge, ili mtu awe Mbunge wa EALA ni lazima akidhi vigezo vya kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa maana hiyo sheria za uchaguzi wa nchi pia zinatumika. Kama hivyo ndivyo, kupita bila kupingwa ni sehemu ya uchaguzi. Na historia inaonesha kuwa wakati wa kuwachagua wawakilishi wa Bunge la SADC, PAP na CPA ndani ya bunge letu, kila Chama kilileta viti kwa idadi kamili na wakapita bila kupingwa. Kitu gani kinafanya EALA iwe tofauti? Kulikuwa na ajenda gani ya siri kwenye hili? Spika wa Bunge ana maslahi gani kwenye hili kiasi kinachomfanya anatumia nguvu kubwa katika kupindisha kanuni za Bunge? Sheria zetu za uchaguzi zinatambua mgombea kupita bila kupingwa anatumia sheria ipi au kanuni ipi kwenye hili la EALA?

Aidha kwenye suala la dini tunamtaka Spika Ndugai tutambue kuwa nchi yetu haina udini na hata sheria ya vyama vya siasa inakataza uwepo wa vyama vya kidini, hivyo kwa Spika kusikika akipandikiza mbegu hii kama kigezo cha kuwapata wawakilishi wetu Bunge la EALA anapandikiza mbegu mbaya sana kwa Taifa letu.

Au Spika Ndugai anataka Watanzania waanze kuulizana kati ya aliowatangaza kuwa wameshinda 7 ni wangapi kati yao wa imani moja? Kama amesahau apitie upya aliowataja kuwa ndio wawakilishi wetu EALA halafu ndio aje kutushauri kama anafanya haya kwa nia njema na si kwa lengo la propaganda na kupandikiza chuki katika taifa, ambazo chama chake CCM kimekuwa kikizitumia muda mrefu kinapoishiwa hoja zenye ushawishi na mashiko kwa umma.

Tunalaani vikali Spika wa Bunge kukiuka kanuni za Bunge zifuatazo ;

1. Kanuni ya 5(3) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge ambayo inaeleza kuwa chama chenye haki "kinaweza" kuweka wagombea watatu katika kila kundi la wagombea wa uchaguzi wa Afrika ya Mashariki. Kuilazimisha CHADEMA kuweka wagombea zaidi ya wawili kwenye nafasi zake mbili ni kinyume cha kanuni na ndio maana katika kila kundi CCM nao hawakuweka wagombea watatu badala yake wakaweka wawili.

2. Spika alikiuka Kanuni ya 9(1) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge kumruhusu mgombea Thomas Malima Mgombea wa CUF kujitoa ndani ya ukumbi wa Bunge akijieleza kinyume cha Kanuni kwa sababu kanuni zinataka mgombea ajitoe kwa barua na taarifa kwa Katibu wa Bunge na nakala kwa Katibu Mkuu wa Chama chake si baada ya saa kumi ya siku moja baada ya uteuzi, kanuni ambayo mgombea huyu hakutimiza matakwa yake na Spika alikaa kimya hata baada ya kukumbushwa na wabunge wetu.

HITIMISHO

Ni lengo la CHADEMA kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na wawakilishi kwenye EALA wenye weledi na uwezo wa kujenga hoja kusimamia maslahi ya nchi yetu. Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya uwakilishi kutoka Tanzania ambao ulichangiwa na Maspika waliopita kwa kutozingatia matakwa ya ibara ya 50 ya Mkataba wa Afrika Mashariki pamoja na masharti ya Kanuni ya 12 na Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari 2017. Hii ilifanya nchi kuwa na uwakilishi hafifu kwa sababu ya ushabiki wa kisiasa

Tungependa kumkumbusha Spika Ndugai kuwa sisi CHADEMA tunaitazama EALA kama sehemu ambayo inatakiwa kama Taifa tupeleke wawakilishi wenye uwezo na uzalendo kwa Taifa letu kwa ajili ya kusimamia na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na sio vyama vyetu.

Afrika Mashariki sio fursa ya ulaji bali ni wajibu kwa Taifa letu. Tupeleke wawakilishi wenye uwezo wa kutuwakilisha. Turejeshe heshima ya Taifa letu. TANZANIA KWANZA.

Imetolewa leo Aprili 7, 2017 na;

John Mrema

Mkurugenzi wa Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje - CHADEMA .

No comments:

Post a Comment