Thursday, April 6, 2017

HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI (KUB), MHESHIMIWA FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018


Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
________________________________

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbunge mwenzetu Mhe. Dkt. Elly Macha (CHADEMA Viti Maalum) kilichotokea tarehe 30 Machi, 2017 huko nchini Uingereza alikokuwa matibabuni. 


2. Mheshimiwa Spika, marehemu alikuwa kielelezo cha mtu jasiri, mwenye kujiamini na aliyekuwa mstari wa mbele kivitendo kujiendeleza na kuwapigania wengine; tena wasio na ulemavu licha ya yeye mwenyewe kuwa na ulemavu. 


3. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri, Taifa kwa ujumla limempoteza mpiganaji madhubuti aliyeamini na kusimamia misingi ya haki na aliyependa kuona haki ikitamalaki na kutendeka katika makundi yote ya jamii.


4. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Ofisi ya Katibu wa Bunge na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza chini ya Balozi, Dr. Asha Rose Migiro kwa namna ambavyo mmekuwa wa msaada kwa njia mbalimbali kwa marehemu na Familia yake tangu wakati wa kuugua kwake hadi sasa wakati juhudi na mipango ikiendelea ya kuurejesha nchini kwa mazishi mwili wa marehemu Dr. Elly Macha.


5. Mheshimiwa Spika, tunatoa pole nyingi kwa wote walioguswa na msiba huu, na tunaiombea roho ya Marehemu mahali pema peponi. AMINA.


6. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kinilinda na kuniimarisha katika kuitenda kazi yake kwa njia ya siasa. Ni dhahiri, siasa sasa si salama tena kuifanya nchini mwetu kwani matukio kadhaa yanayotukumba wanasiasa na viongozi wa upinzani siyo ya kawaida na hayaakisi utamaduni wetu tuliouzoea kama Taifa.


7. Mheshimiwa Spika, kwa nchi na viongozi wanaoheshimu Demokrasia, huviona vyama vya siasa vya upinzani kama vyombo muhimu vya kuwasaidia katika kupata mawazo mbadala yaani “Free Consultancy”. Hujipima mafanikio yao kwa kuchambua kwa makini maoni ya wapinzani na kujirekebisha pale inapobidi.


8. Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja na nusu wa utawala wa awamu hii tumeshuhudia manyanyaso na uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wetu kuuwawa au kupotea. Mfano aliyekuwa Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Geita Mhe. Alphonce Mawazo aliyeuwawa mchana kweupe na watu wakishuhudia na waliohusika wanajulikana. Msaidizi wangu Ben Rabiu Saanane kupotea baada ya kupokea vitisho kadhaa vyenye asili ya kisiasa na hadi sasa vyombo vya dola havijatoa maelezo ya kina ya Ben kapelekwa wapi!! 


9. Mheshimiwa Spika, wabunge wetu nao hawajawa salama hata kidogo. Tumeshuhudia mbunge wetu Mhe. Peter Lijualikali kufungwa kwa uonevu mkubwa, Mbunge wetu mwingine Mhe. Godbless Lema kunyimwa dhamana kwa zaidi ya miezi minne kwa shtaka lenye dhamana na wengine wengi nikiwamo mimi mwenyewe na Mhe Tundu Lissu kukamatwa mara kwa mara na vyombo vya dola na kufunguliwa mashtaka mbalimbali yasiyo na nia njema wala afya kwa ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu.


10. Mheshimiwa Spika, tunaamini mapito haya mazito ya kisiasa katika nchi yetu yanalenga kujaribu kufifisha ndoto ya Taifa - ndoto ya kuwa taifa huru linalosimamia misingi ya haki za binadamu, uhuru wa maoni ya kila raia, demokrasia ya kweli, - ndoto ya kuwa taifa linaloheshimu katiba ya nchi na ndoto ya kuwa taifa lenye uchumi unaomnufaisha kila mwananchi. 


11. Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa upande wetu, na hila hizo za baadhi ya wenye mamlaka hazijatuondoa kwenye lengo kubwa la kuwavusha wananchi wa Tanzania kuifikia ndoto hiyo ya Taifa; na kwa sababu hiyo tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila jambo.




*UKIUKWAJI WA DEMOKRASIA NA UTAWALA WA SHERIA*


12. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ya Tanzania imesifika duniani kote kwa tunu zake za amani, umoja na mshikamano kutokana na waasisi wa taifa hili kuheshimu na kuenzi misingi ya utawala wa sheria demokrasia na uhuru wa kupata habari.


13. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ni kwamba: “Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo”.


14. Mheshimiwa Spika, ibara ya 18 ya Katiba imeweka msingi wa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kusema kwamba: “Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii” 

15. Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani, zimeonekana dalili za wazi za Serikali hiyo kuvunja Katiba ya Nchi kwa kutupilia mbali misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa kupata habari jambo ambalo linaweza kuitumbukiza nchi yetu kwenye Dola la ki- dikteta.

16. MheshimiwaSpika, matukio mahsusi ya ukandamizaji wa haki na demokrasia yaliyofanywa na serikali kinyume cha katiba na sheria za nchi ni pamoja na haya yafuatayo.

i. *Kupiga Marufuku Mikutano ya Vyama vya Siasa:* 

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waziri Mkuu na hatimaye Rais, imetangaza kwamba ni marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuipa Serikali nafasi ya kufanya kazi. Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba kama ilivyonukuliwa hapo awali. Aidha, katazo la mikutano ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya siasa ya 1992 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa.

ii. *Kupiga Marufuku Urushwaji wa moja kwa moja (live coverage) wa Mijadala ya Bunge:*

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ilipiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge kupitia televisheni ya taifa na vyombo vingine vya habari. Katazo hilo ni kinyume na ibara ya 18 ya Katiba ambayo inatoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi. Aidha, kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda hivi karibuni cha kuvamia kituo cha habari cha Clouds akiwa na polisi wenye silaha za moto kwa malengo ya kushinikiza kituo hicho kurusha habari anazozitaka yeye sio tu kimekandamiza uhuru wa vyombo vya habari bali pia kimenajisi tasnia ya habari nchini.

iii. *Kudhibiti Wabunge wa Upinzani wawapo Bungeni:*

Mheshimiwa Spika, yamekuwapo matukio kadhaa yanayoashiria kutaka kuwadhibiti Wabunge wa Upinzani Bungeni kwa lengo la kuwanyamazisha wasiikosoe Serikali. Jambo hili limefanyika kwa namna mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea kesi Wabunge wa Upinzani na kuwapeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambapo hukumu ya kuwaadhibu inakuwa imeshaandaliwa. Kwa hila hizo, wabunge wa Upinzani wamekuwa wakipewa adhabu za kufungiwa kuhudhuria kuanzia vikao kumi hadi mikutano miwili ya Bunge bila hata ya kusikilizwa jambo ambalo ni kinyume kabisa cha Kanuni za Bunge. Aidha, mara kadhaa wabunge wa Upinzani wamekamatwa kwa udhalili mkubwa na kusafirishwa umbali mrefu wanapokuwa wanahudhuria vikao vya Bunge.

iv. *Kuingilia Mhimili wa Mahakama:*

Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM kupitia Rais, kwa nyakati tofauti imeonekana kujaribu kuingilia uhuru wa Mahakama jambo ambalo ni hatari kwa utoaji wa haki nchini. Katika hotuba yake, wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria duniani Rais alinukuliwa akisema kwamba Mahakama iwahukumu haraka haraka watu waliokwepa kodi halafu atatumia asilimia fulani ya fedha ambazo zitakuwa zimepatikana kutokana na faini za wale walioshindwa kesi kuwapa Mahakama ili wafanye kazi vizuri ya kuendelea kuwahukumu na kuwafunga wakwepa kodi. Kauli kama hiyo inaweza kusababisha watuhumiwa wasisikilizwe na kutendewa haki. Aidha, kutoa ahadi ya kuipa Mahakama fedha ili ifanye kazi ya kuwahukumu wakwepa kodi wenye mgogoro na Serikali inatoa taswira ya rushwa.

v. *Kupuuza Utawala wa Sheria:* 

Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Juni, 2016; wakati wa uzinduzi wa siku ya usalama wa raia, Rais alinukuliwa akiwaruhusu polisi kuwaua majambazi bila kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Aidha aliuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi kuwapandisha cheo watakao wauwa majambazi badala ya kuwashtaki mahakamani. Tafsiri ndogo ya Kauli ya Rais ni kwamba utawala wa sheria uwekwe kando na polisi sasa au wananchi wajichukulie sheria mkononi. Jambo hili litaiingiza nchi kwenye machafuko kwa kuwa utashi wa polisi sasa ndio utakaokuwa wa mwisho na wa kuaminika kuliko Mahakama. Watu wengi watauwawa kwa kisingizio kuwa ni majambazi kutokana na chuki binafsi tu na polisi. Nani ataamua haki katika mazingira hayo?


vi. *Uonevu unaofanywa na Vyombo vya Dola dhidi ya Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba:* 

Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Zanzibar waliukataa utawala wa CCM kupitia sanduku la kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Serikali ya Muungano ikishirikiana na SMZ wakafanya hila kuupora ushindi wa Wazanzibari kwa kuufuta uchaguzi ule bila sababu za msingi na kuitisha uchaguzi mwingine haramu ambao ulisusiwa na Chama cha Wananchi - CUF, kilichokuwa kimeshinda uchaguzi uliofutwa. Kutokana na tukio hilo, Serikali ya Muungano ikishirikiana na SMZ imeamuru vyombo vya dola vikiwemo Jeshi la Polisi, JWTZ na Usalama wa Taifa kuwaadhibu wananchi wa Zanzibar hususan wanaounga mkono Chama cha Wananchi – CUF kwa kuwavamia nyakati za usiku na kuwakamata, kuwapiga, kuwafungulia mashtaka bandia na kupora mali zao ikiwemo mifugo. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu unaopaswa kulaaniwa na watu wote.

*MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA TAIFA*

17. Mheshimiwa Spika, kilio cha hitaji la Katiba Mpya ya Nchi yetu kilianza kusikika Tangu Mfumo wa Siasa ya Vyama vingi uanze hapa nchini miaka ishirini na tano iliyopita. Haina shaka kwamba vyama vya upinzani ndivyo vilivyoanza kutoridhishwa na mfumo wa uchaguzi, madaraka makubwa ya Rais, na mfumo mzima wa utawala na uendeshaji wa Serikali mambo yaliyoanzisha ajenda ya madai ya Katiba Mpya.

18. Mheshimiwa Spika, baada ya mapambano hayo ya kudai katiba mpya, hatimaye Serikali ilianzisha mchakato wa Katiba Mpya. Mchakato huo ulianza kwa Bunge kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 mnamo mwezi Novemba, 2011 na baadaye kufanyiwa marekebisho mwaka 2012 na 2013. Aidha, Bunge lilitunga Sheria ya Kura ya Maoni mwaka 2013. Katika kipindi hicho hicho, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilifanya kazi kubwa ya kukusanya na kuyachambua maoni ya wananchi hadi kupata Rasimu ya kwanza ya Katiba mnamo tarehe 3 Juni, 2013. 

19. Mheshimiwa Spika, rasimu hiyo ilipelekwa kwa wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya maoni zaidi na hatimaye baada ya kuzingatia maoni ya wananchi ikatengenezwa rasimu ya pili ya Katiba ambayo ilikabidhiwa katika Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa ili kupata Rasimu ya Katiba Pendekezwa.

20. Mheshimiwa Spika, yaliyotokea katika Bunge Maalum la Katiba yalikuwa ni fedheha na aibu kubwa kwa Taifa kwani Chama Cha Mapinduzi kwa kutumia wingi wa wajumbe wake katika Bunge hilo kiliuteka mchakato ule na kuyafuta kwa makusudi maoni ya wananchi yaliyokuwamo katika rasimu iliyowasilishwa katika Bunge Maalum na kuingiza sura na vifungu vipya kwa maslahi yao wenyewe.

21. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa vyama vya Upinzani katika ushirikiano wa UKAWA, tuliondoka katika Bunge Maalum kwa kuwa hatukupenda kushiriki kunajisi mchakato wa kupata Katiba Mpya. Tangu vyama vya Upinzani tujitoe katika mchakato huo haramu, mchakato wa Katiba Mpya umekwama na mpaka sasa hakuna mwelekeo wowote kuhusu suala hilo.

22. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Tanzania bado wanahitaji mabadiliko makubwa ya kimuundo na kimfumo katika uendeshaji wa Serikali – mabadiliko ambayo msingi wake ni Katiba Mpya; 
Na kwa kuwa Mgombea wa Urais kupitia CCM aliwaahidi wananchi kuleta mabadiliko hayo na kuongeza kuwa hatawaangusha;
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutekeleza ahadi hiyo kwa kurejesha tena mchakato wa Katiba Mpya. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa mchakato wa Katiba Mpya urudishwe nyuma katika ngazi ya Bunge Maalum ili kujadili maoni ya wananchi katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba bila kuathiri maudhui ya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.

Inaendelea.......






*HALI YA UCHUMI KATIKA TAIFA*

*Hali ngumu ya maisha*

23. Mheshimiwa Spika, uchumi ndio msingi wa maisha ya binadamu. Hitilafu yoyote inayotokea katika ukuaji wa uchumi inakuwa na athari ya moja kwa moja kwa maisha ya mwananchi.

24. Mheshimiwa Spika, tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikijigamba kuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ikilinganishwa na serikali za awamu zilizotangulia, lakini kumekuwa na kilio kikuu kwa upande wa wananchi kuhusu hali ya maisha kuendelea kuwa ngumu kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu.

25. Mheshimiwa Spika, kilio hiki cha wananchi kinamaanisha kwamba ukuaji wa uchumi unaohubiriwa na Serikali haujawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa nchi hii. Wanazuoni wa uchumi wanasema kwamba “Growth is inclusive when it takes place in the sectors in which the poor work (e.g. agriculture); occurs in places where the poor live (e.g. undeveloped areas with few resources); uses the factors of production that the poor possess (e.g. unskilled labour); and reduces the prices of consumption items that the poor consume (e.g. food, fuel and clothing).” 

26. Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo; unatokea katika maeneo ambayo watu masikini wanaishi kwa mfano maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali; unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo kwa mfano nguvukazi isiyo ya kitaalamu; na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.

27. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ukipima hali ya Tanzania utaona kwamba uchumi wetu sio shirikishi kwa kuwa ukuaji wake hautokei katika sekta ambazo watu masikini wan
afanya kazi au maeneo ambayo watu masikini wanaishi. Aidha, ukuaji wa uchumi wetu hautumii nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo na pia ukuaji huo haujapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia.

*Kukosekana Mkakati wa kuinua uchumi vijijini*

28. Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa makini vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Tano, utagundua Serikali haina mkakati wowote madhubuti wa kuinua uchumi wa wananchi waishio vijijini. (Rural Economy). Uchumi wa Vijijini unagusa kilimo, uvuvi na ufugaji na sekta hizi ndizo zenye uwezo mkubwa wa kuajiri watu na kupunguza umaskini. Tukumbuke asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea sekta hizi.

29. Mheshimiwa Spika, duniani kote, hakuna nchi iliyowahi kufanikiwa kuingia kwenye uchumi wa viwanda kabla ya kupitia mageuzi ya Kilimo. Nchi zote za Asia ambazo tunapenda kuiga economic model zao ziliendeleza kwanza kilimo na bado pamoja na kuingia kwenye uchumi wa viwanda, bado idadi kubwa ya watu wao wanaendelea na sekta hizi za rural economy.

30. Mheshimiwa Spika, kilicho dhahiri ni kuwa serikali ya awamu ya Tano haikujiandaa na sera hii na inakurupuka kufanya mambo mbalimbali bila kuwa na mpango mathubuti wenye matokeo yanayopimika yaani “Integrated rural development plan”. Kwa miaka ya karibuni mchango wa Sekta ya kilimo unazidi kushuka na sasa ni pungufu ya 2.5% ya GDP.

31. Mheshimiwa Spika, Sekta hizi za kilimo, Ufugaji na Uvuvi zilipewa asilimia 2.22 tu ya fedha zilizoidhinishwa kwa shughuli za maendeleo ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.2 kati ya bilioni 200.5 zilizowekwa na bajeti ilhali zaidi ya bilioni 128 zimetumika kama malipo ya awali kununulia ndege za Air Tanzania, bila hata ya kuwepo Business Plan. Kwa Serikali hii, ndege zinazohudumia wananchi wasiozidi 10,000 ni muhimu na kipaumbele kuliko sekta inayogusa zaidi ya 70% ya wananchi wake.

*Hali ya Uwekezaji*

32. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tovuti ya Economic Freedom (Tanzania Economy: Population, GDP, Inflation, Business, Trade, FDI, Corruption) inayoonesha vigezo vya uhuru wa kuwekeza katika sekta za uchumi, Tanzania ipo katika rangi nyekundu kwenye kigezo cha Uhuru wa kiuchumi ikishika nafasi ya 105, kati ya 180. Ikumbukwe kwamba uhuru wa kiuchumi ni kigezo kikubwa cha kimataifa cha kupima mwenendo wa uchumi. Nafasi ambayo Tanzania imeshika ni kiashiria kibaya kwamba uchumi wetu upo katika hatari ya kuporomoka vibaya.

33. Mheshimiwa Spika, uchambuzi uliofanywa na wataalamu wa uchumi inaonesha kwamba kwamba; uchumi wa Tanzania upo hatarini kuporomoka kutokana na mambo yafuatayo:

i. *Hali ya kisiasa ya nchi:* 
Mheshimiwa Spika, Tanzania bado iko katika hali tete ya kisiasa kufuatia uchaguzi wa 2015, ambapo suala la Zanzibar bado halijatatuliwa na kuendelea kukiukwa kwa misingi ya kidemokrasia, kubinywa kwa uhuru wa siasa za vyama vingi na uhuru wa vyombo vya habari. Jambo hili limeathairi uhuru wa kiuchumi na limewatia hofu wafanya biashara wa ndani na nje hivyo kupunguza kasi ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

ii. *Ustawi wa Jamii na Utawala Bora:*
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ya ‘Human Development Indicator’; bado Tanzania inashika nafasi ya chini katika vigezo vya kimataifa vya ustawi wa jamii na utawala bora. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania inashika nafasi ya 151 kati ya 187. Aidha, kigezo cha ustawi kijinsia kinaishusha Tanzania kwenda kwenye nafasi ya chini zaidi yaani 129 kati ya nchi 159 - yaani ni wa ishirini kutoka mkiani. (http://hdr.undp.org/sites/all/themes/hdr_theme/country-notes/TZA.pdf ukurasa wa 6)

iii. *Katiba ya Nchi:*
Mheshimiwa Spika, kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya ya Wananchi kumesababisha kuwa na hali ya ‘Constitutional Uncertainty’ jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaliona kuwa na tishio au ‘threat’ kiuchumi. Hii ni kwa sababu nchi inapokuwa katika mkwamo wa kupata katiba inayoridhiwa na wananchi huweza kusababisha machafuko ya kisiasa (Political instability) na jambo hili huwatia hofu sana wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa jambo ambalo huwafanya kuzuia mitaji yao mikubwa kwenda katika nchi yenye hali kama hiyo. Hili nalo limetuathiri kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana kuna malalamiko miongoni mwa wananchi kwamba mzunguko wa fedha ni mdogo.
iv. *Mahusiano yasiyotabirika kati ya Serikali na Sekta Binafsi:*

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Formal Sector Employment and Earnings Survery ya 2015, ni kwamba 1/3 ya mapato ya kodi yanatokana na watumishi (waajiriwa) ambapo sekta binafsi ina waajiriwa 1,432,985 na sekta ya umma waajiriwa 708,366. Aidha, takriban 2/3 ya makusanyo ya TRA yanatoka katika sekta binafsi. Kwa takwimu hizo ni kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika mapato ya Serikali na hivyo katika uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Spika, licha ya umuhimu huo wa sekta binafsi katia uchumi wa nchi yetu, Serikali imekuwa ikiweka mazingira magumu kwa sekta hii kukua. Sekta binafsi imekuwa ikilalamika kuwa mfumo wetu wa kodi sio rafiki kuikuza Sekta binafsi, pili mazingira ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha sio rafiki kwa biashara hasa zinazoanzishwa, kwani serikali inashindana na sekta binafsi katika kukopa kwenye taasisi za fedha. Haya mazingira yanapunguza kasi ya uanzishwaji wa biashara mpya kwani watu wanaogopa kuingia kwenye sekta binafsi.



v. *Tishio la kuanguka kwa uchumi wa nchi:*
Mheshimiwa Spika, tayari Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeionya Tanzania kuwa uchumi wake uko hatarini kuporomoka kutokana na kubana matumizi kulikopitiliza, kushuka kwa idadi ya mikopo, utekelezaji hafifu wa uwekezaji wa umma na kutotabirika kwa sera za serikali kuhusu sekta binafsi. 

*Mheshimiwa Spika, IMF wanasema hivi kuhusu uchumi wa Tanzania: "There are risks that could adversely affect economic growth going forward, arising from the currently tight stance of macroeconomic policies, the slow pace of credit growth that may become protracted, slow implementation of public investment, and private sector uncertainty about the government's new economic strategies” *

Mheshimiwa Spika, IMF wanapendekeza sera za fedha zilegezwe ili kuondoa tatizo la mzunguko mdogo wa fedha unaotokana na kubana matumizi pamoja na kuisadia sekta binafsi kupata mikopo."Monetary policy should be eased to address the tight liquidity situation and support credit to the private sector” Hii ni pamoja na kulipa wakandarasi mbalimbali wanaoidai Serikali kwani deni la ndani sasa linakaribia Trilioni 5.

Mheshimiwa Spika, angalizo hili la IMF limechangiwa na wabobezi wa Uchumi akiwemo Profesa Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anayesema, nanukuu: "…In fact right now, you could say we are in the stage of a recession and if we don't take heed of the IMF advice and act, the country may enter the stage of depression, which is worse”


Mheshimiwa Spika, ushauri unaotolewa na mchumi huyu ni kwamba tutekeleze ushauri wa IMF - tusipotekeleza ushauri wa IMF, ni kwamba nchi itaingia kwenye anguko kuu la uchumi – economic depression.

vi. *Kutokuheshimu Mikataba na Uchumi kuendeshwa kwa kauli za Rais*

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa kuhakikisha rasilimali za nchi zinainufaisha nchi yetu, ni muhimu kwa viongozi wetu kutambua “sensitivity” ya Multinational Corporations inapokuja kwenye suala la kubadilisha au kutokuheshimu mikataba.


Mheshimiwa Spika, pale ambapo Serikali inaona kuna mambo hayako sawa itake mazungumzo ya kurejea mikataba kabla ya kutoa makatazo hadharani kama ilivyokuwa kwa katazo la kupeleka “mchanga wa Dhahabu” nje ya nchi kwa uchenjuaji linalohusu Kampuni ya Acacia inayochimba dhahabu nchini. Mambo haya yanahitaji muda na mipango na kamwe kukurupuka kutakuja kulisababishia Taifa hili ulipaji wa fidia kubwa sana na kibaya zaidi kuua kabisa imani ya wawekezaji wakubwa hususan wa kimataifa.


34. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia kipengele hiki cha uchumi kwa kusema kwamba, serikali isijifiche kwenye kivuli cha tarakimu kwamba uchumi wetu unakuwa kwa asilimia saba na kujidanganya kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi duniani ilhali bado wananchi wake ni masikini wa kutupwa. Kwa mujibu taarifa ya Benki ya Dunia, Watanzania zaidi ya milioni 12 ni masikini wa kutupwa kwani wanaishi chini ya mstari wa kiwango cha umaskini (below poverty line). Hii ni dalili mbaya kwani inaashiria kwamba hakuna uhusiano katika ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7 na kuboreka kwa maisha ya wananchi. Kwa maneno mengine ukuaji wa uchumi si shirikishi kama nilivyoeleza hapo awali na kwa maana hiyo unagusa kwa kiwango kidogo sana maisha ya mwananchi wa kawaida. 

*Deni la Taifa na Athari zake kwa maendeleo ya Taifa*

35. Mheshimiwa Spika, madeni ya Taifa hadi Desemba 2016 yamefikia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 20.7 yakiwemo ya ndani na nje ikiwa ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii. Kiwango hiki ni takriban shilingi za Kitanzania 46.66 trilion. Kasi ya kukua kwa deni hili inazidi kushika kasi kutokana na riba na adhabu mbalimbali zitokanazo na kuchelewa kulipa kwa wakati madeni yetu. Aidha kuongezeka huku kunachangiwa na Serikali kuendelea kukopa hususan kwenye vyanzo vya kibiashara ambapo riba zake ni kubwa.

36. Mheshimiwa Spika, deni la nje sasa hivi linaigharimu serikali karibu nusu ya makusanyo yake yatokanayo na kodi. Ukichanganya na mishahara, karibu asilimia 70 ya mapato ya ndani yanatumika kulipia deni la nje na mishahara ya watumishi mbalimbali wa Serikali.

37. Mheshimiwa Spika, mara kadhaa watu wengi wametahadharisha kuhusu athari za kukopa kuliko uwezo wetu na Serikali imejitetea kwamba deni la nchi ni stahimilivu. Pamoja na ustahimilivu huo, sasa athari zake zinaanza kuwa na athari kubwa katika kutekeleza bajeti na hivyo mipango ya serikali ikiwepo miradi mbalimbali ya maendeleo.

*NAFASI YA TANZANIA KATIKA JUMUIYA YA KIMATAIFA*

38. Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilijijengea heshima kubwa katika medani za kimataifa hasa kwenye masuala ya kupigania uhuru wa nchi nyingine barani Afrika, pamoja na kutetea nchi ambazo zilikuwa zinaonewa na mataifa mengine duniani.

39. Mheshimiwa Spika, Ushirikiano wa kimataifa kwa nchi inayoendelea kama Tanzania ni jambo la msingi sana kwani kuna mambo mengi ambayo tunahitaji kujifunza kutoka kwa mataifa mengine ili kuweza kuasili mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia, kiuchumi na kiutandawazi yanayoendelea kutokea kila siku duniani. 

40. Mheshimiwa Spika, Licha ya umuhimu huo, serikali ya awamu ya tano imeonekana kufifisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mengine kwa kudhibiti safari za nje kwa kisingizio cha kubana matumizi. Ikumbukwe kwamba kudhibiti safari za nje kusiko kwa kimkakati ni kuliingiza taifa kwenye giza nene kwani safari hizo zilikuwa ni lango la fursa za biashara ya kimatafa (international trade) ambayo ndiyo msingi wa diplomasia ya ki-uchumi.

41. Mheshimiwa Spika, Ushirikiano wa kimataifa unaimarishwa pale ambapo wakuu wa nchi mbalimbali wanapokutana kujadili masuala mbalimbali kuhusu mustakabali wa nchi zao na namna ya kusaidiana kukabiliana na changamoto mbalimbali. Ni jambo la kustaajabisha kuona Rais wa nchi yetu akiwa na mwamko mdogo wa kushiriki mikutano ya kimataifa kwa ajili ya kukuza ushirikano na mataifa mengine. Kitendo cha Rais kushindwa kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) mwaka jana kimeiweka Tanzania nyuma katika uhusiano wa kimataifa.

42. Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutambua kuwa Rais amekuwa akituma wawakilishi katika mikutano ya kimataifa, lakini viko vikao au mikutano ya kimkakati (strategic meetings) ambayo ni lazima Rais wa nchi kushiriki.

43. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Rais kuacha kukwepa kuhudhuria mikutano ya kimataifa na ya kikanda ambayo ni muhimu kwa ajili ya kujenga mustakabali wa diplomasia ya uchumi pamoja na uhusiano wa kimataifa kwa ujumla kama ambavyo umekuwa ni utamaduni wa taifa letu. Aidha, washauri wa Rais hasa wa masuala ya kimataifa wamshauri Rais juu ya umuhimu wa ushiriki wake katika vikao na mikutano hiyo pamoja na kuzingatia itifaki za kimataifa.

44. Mheshimiwa Spika, kuna udhaifu mkubwa sana katika Serikali hii wa kutozingatia itifaki za kimataifa. Wengi walishangazwa wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anakuja nchini na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya nje bila kupata fursa ya kuonana na Rais. Inaweza kuonekana kama ni kawaida tu Rais kutompokea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa; lakini katika jicho la kidiplomasia kuna makosa makubwa sana ya kiitifaki yanayofanywa na Ofisi ya Rais.

45. Mheshimiwa Spika, uhusiano wa kimataifa unaweza kuathiriwa na namna sisi kama taifa tunavyowatendea raia wa nchi nyingine wanaoishi au kufanya kazi katika nchi yetu. Mataifa mengine huwa yanajali sana hali za raia wao wanaoishi au kufanya kazi katika mataifa mengine. Hivyo, mataifa hayo huwa yako tayari hata kupigana vita kwa ajili ya raia wao wanaonyanyaswa au kutendewa visivyo katika nchi nyingine.

46. Mheshimiwa Spika, kitendo cha hivi karibuni cha Rais wetu kuagiza pasi ya kusafiria ya mkandarasi kutoka India ambaye anajenga mradi wa maji wa Ngapa huko Lindi kutokana na makosa aliyoyafanya katika mradi huo unaweza kuingiza nchi yetu katika mgogoro wa kidiplomasia kwa sababu pasi ya kusafiria ni mali ya taifa ambalo limetoa pasi hiyo. Na katika pasi hiyo kuna tamko la Rais wa nchi husika linaloomba raia huyo apewe ulinzi na msaada wowote atakaohitaji katika nchi atakayokuwa ameingia kuishi au kufanya kazi.

47. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa utamaduni duniani ni kuwa pasi ya kusafiria hutolewa na Rais wa nchi husika kwenda kwa mamlaka ya nchi ambayo mtu anasafiri kwa ajili kupata msaada wowote anaohitaji kulingana na malengo ya safari yake na taratibu za nchi aliyopo. Hata Sheria yetu inayosimamia utoaji wa pasi na nyaraka nyingine za kusafiri kifungu cha nne kinatamka kuwa pasi inatolewa na Rais kwa ajili ya kumtambulisha Mtanzania katika mamlaka ya nchi nyingine na kupatiwa msaada na usaidizi wowote atakaohitaji kwa mujibu wa taratibu za nchi husika. Hivyo, kuagiza pasi hiyo kushikiliwa ni kuidhalilisha mamlaka iliyotoa pasi hiyo kwa maana ya Rais wa nchi husika jambo ambalo linaiingiza nchi yetu katika mgogoro wa kidiplomasia moja kwa moja.

48. Mheshimiwa Spika, agizo la Rais la kushikilia passport ya mkandarasi huyo tayari limeripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa ambavyo kwa vyovyote vile vinasomwa na watu mbalimbali duniani wakiwemo wawekezaji.

49. Mheshimiwa Spika, serikali ina vyombo vya ulinzi na usalama mpaka mipakani, kama mwekezaji au mkandarasi kutoka nje amepewa maelekezo ya kumaliza mradi kwa muda fulani, ni vema akapewa nafasi ya kufanya hivyo bila kuchukua pasi yake ya kusafiria. Mambo yote hayo yanafanyika kwa mujibu wa mikataba ambayo serikali imeingia na wawekezaji au wakandarasi na hivyo ni vema mikataba ikazingatiwa na au maelekezo/makubaliano mengine kuliko kuanza kuchukua pasi za kusafiria za mataifa mengine.

50. Mheshimiwa Spika, athari za maamuzi au amri za Rais zinaweza zisionekane leo lakini kwa utafiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kuwa agizo la Rais la kuamuru pasi ya raia mwingine kuchukuliwa liliripotiwa katika vyombo vya habari vingi duniani pamoja na nchi ya India yenyewe. Jambo hili si tu linatia doa nchi yetu katika masuala ya uhusiano wa kimataifa lakini pia linaweza kuleta athari katika sekta ya uwekezaji.


*HALI YA UTUMISHI WA UMMA NCHINI*



*Utumbuaji Holela wa Watumishi Usiozingatia Sheria na Taratibu za Utumishi wa Umma*

51. Mheshimiwa Spika, sekta ya utumishi wa umma imeghubikwa na hofu kubwa hivi sasa kutokana na utumbuaji holela wa watumishi usiozingatia sheria za nchi. Watu wachache wanaamini wao wana mamlaka ya kuamua vile wanavyoona inafaa wao kwa utashi wao bila kuzingatia sheria za nchi. Ifahamike kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeti haipuuzi hata kidogo jitihada zinazofanywa na kila mmoja wetu katika kuhakikisha sekta ya umma inafanya kazi kwa weledi ili kuleta tija katika taifa. Lakini, jitihada hizi ni lazima zizingatie sheria na taratibu tulizojiwekea kama taifa ili kuepusha uonevu na matumizi mabaya ya madaraka kwa waliopewa dhamana.

52. Mheshimiwa Spika, ifahamike kuwa hakuna mtu yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliye juu ya sheria au mwenye mamlaka ya kutumia cheo chake kinyume na sheria. Nayasema haya kwa kuwa; kumeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kutumia mamlaka yao kuwawajibisha watumishi wa umma bila kuzingatia sheria kwa kuwatumbua hadharani bila kupewa haki ya kusikilizwa na hata kutumia lugha za kejeli na udhalilishaji. Hii imechangiwa pia na ‘umwamba’ ambao kila mwenye dhamana anataka kuuonyesha ili kufurahisha mamlaka zao za uteuzi au kwa hofu tu ya wao kutumbuliwa hata bila sababu za msingi. 

53. Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa katika Ibara ya 13 (6) (a) na (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatao haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya sheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, na katika kipengele (b) kinasema ni marufuku kwa mtu anayeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. Hivyo, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuacha mara moja tabia hii inayokiuka haki za watumishi wa umma, inayodhalilisha sekta ya umma na inayojenga hofu na itakayo iletea hasara kubwa serikali katika kulipa fidia.

*Uhakiki wa Vyeti na Watumishi Hewa*

54. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendesha zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na vyeti vya taaluma zao ili kukabiliana na tatizo la watumishi hewa pamoja na watumishi wasio na sifa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina tatizo na zoezi la namna hiyo kwa kuwa linalenga kuokoa fedha za umma zinazopotea kutokana na watumishi hewa na kudhibiti ubora wa huduma zinazotolewa katika sekta ya umma kwa kuhakikisha watumishi wote wana taaluma au sifa stahiki katika kazi wanazozifanya. 

55. Mheshimiwa Spika, Pamoja na dhamira hiyo njema ya serikali ni muhimu kazi hii ikafanywa kwa weledi bila kuathiri masharti ya Ibara ya 13 (1) ya Katiba ya nchi inayoonya ubaguzi wa aina yoyote kwa mtu yoyote bila kujali cheo chake, kabila lake ,dini yake ,elimu yake na hata jinsia yake. 

56. Mheshimiwa Spika, wapo Watanzania wengi waliochukuliwa hatua baada ya kukutwa na vyeti feki lakini cha ajabu ni kuwa kitendo cha Mheshimiwa Rais kuendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, ambaye anashutumiwa kutumia cheti ambacho sio chake na kushindwa hata kuamuru uchunguzi wa jambo hilo ufanyike, ni kitendo cha kufedhehesha sana kwani kinawagawa Watanzania. Ubaguzi wa namna hiyo unalifanya kundi fulani kujisikia wanyonge na hawana haki na kundi jingine kujisikia wao wana haki zaidi ya wengine. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutenda haki katika zoezi hili la uhakiki kwani limeshaanza kuonyesha dalili za ubaguzi na upendeleo jambo ambalo linasababisha matabaka ya watu katika taifa.

*KAZI NA AJIRA KWA VIJANA*

57. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2011 ni kwamba; asilimia 68 ya watanzania ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35. Nyaraka zinaonesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na nguvu kazi ya watu zaidi ya 22,152,320 na kati ya hao watu 19,783,648 hawana ajira iliyo rasmi. Kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kati ya umri wa miaka 15-34 ni asilimia 13.4. 

58. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa tovuti “youthemployement” (www. youthemployementdecade.org), nguvu kazi mpya inayoingia kwenye soko la ajira kila mwaka ni zaidi ya watu 800,000 na kati ya hao ni vijana 40,000 tu sawa na asilimia 5.7 ndio wanaopata ajira katika sekta rasmi. Ikumbukwe kwamba takriban vijana 700,000 wanamaliza vyuo na shule katika ngazi mbalimbali kila mwaka na wengine 100,000 wanahamia mijini kutoka vijijini na wote hawa wanahitaji ajira.

59. Mheshimiwa Spika, ukosefu wa ajira hasa vijana ni janga la taifa na serikali isipochukua hatua za makusudi yamkini nchi hii inaweza kuja kuingia kwenye mgogoro mkubwa kutokana na hali ngumu ya maisha itakayokuwa imesababishwa na ukosefu wa ajira. Ili taifa lisifike huko, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwa serikali kwamba, itoe maagizo kwa wakurugenzi wote wa Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti wakati Waziri mwenye dhamana na TAMISEMA atakapokuwa anawasilisha bajeti ya wizara yake.

60. Mheshimiwa Spika, kukiwa na dhamira ya kutekeleza ushauri huu, tutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira nchini. 

*SAKATA LA DAWA ZA KULEVYA*

61. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutambua jitihada za Serikali, Waheshimiwa Wabunge na jamii kwa ujumla kwa kushirikiana kwa pamoja katika kupambana na biashara ya madawa ya kulevya pamoja na matumizi ya aina yoyote ya madawa ya kulevya. Sote tunatambua madhara makubwa ya madawa haya kwa kuwa tumepoteza ndugu, jamaa , marafiki na nguvu kazi ya taifa kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. 

62. Mheshimiwa Spika, kihistoria vita ya dawa ya kulevya nchini imeanza muda mrefu. Jitihada za kupambana na madawa haya zilizaa matunda yaliyopelekea kutungwa kwa Sheria ya madawa na Uzuiaji wa Usafirishaji wa Madawa Haramu tangu mwaka 1995 ambayo ilifutwa na baadaye kutungwa sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015. Aidha, iliundwa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mfuko wa Udhibiti wa Dawa za Kulevya na uwepo wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) pamoja na kampeni mbalimbali zinazoendeshwa na serikali, taasisi binafsi, wanasiasa na hata viongozi wa dini katika kupambana na madawa hayo. 

63. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni harakati hizi zilichukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya. Jambo hili lilizua mtanzuko mkubwa kwa wanajamii huku kila mmoja akilipokea kwa namna yake. 

64. Mheshimiwa Spika, Kitendo cha kuwataja watu hadharani bila kuwa na ushahidi wowote kilifanywa kibabe kwa kuwakejeli, kuwadhihaki na kwa uonevu mkubwa kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wowote na pia mahakama haikuhusishwa katika hatua za awali. Hii ina maana kwamba Mkuu huyo wa Mkoa aliamua kuwa hakimu kwa kutumia cheo chake kuchafua majina ya watu na haiba walioitengeza kwa muda mrefu na gharama kubwa.

65. Mheshimiwa Spika, tabia ya viongozi wa namna hii wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kuvunja sheria kwa makusudi ni lazima ipingwe kwa nguvu zote na hatua kali zichukuliwe dhidi yao bila kujali nafasi zao au vyeo vyao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa sana na kitendo cha Rais Magufuli kuendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam katika matukio tofauti tofauti huku ushahidi wa wazi ukionyesha matumazi mabaya ya madaraka pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, umiliki wa mali ulio wa mashaka ikiwemo magari ya anasa ya wafanyabiashara aliowatuhumu kujihusisha na madawa ya kulevya, vitisho kwa vyombo vya habari , kuingilia uhuru wa habari nchini ,matumizi mabaya ya rasilimali za nchi ikiwa ni pamoja na kufanya tafrija ya kutimiza mwaka mmoja kazini kwa kivuli cha kampeni ya kutokomeza dawa za kulevya. 

66. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana kuona Mheshimiwa Rais akimtoa kafara Waziri wake kwa gharama ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.Tunajiuliza kuna jambo gani lililojificha baina ya Rais na Mkuu huyu wa Mkoa? Tatizo la madawa ya kulevya sio tatizo la mtu mmoja na wala halihitaji kufwanywa kama vita ya mtu binafsi. 

67. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua Rais ana mamlaka ya kuteua na kutengua uteuzi lakini hana mamlaka ya kumkingia kifua mtu yoyote pale anapovunja sheria za nchi hata kama Rais ndie aliyempa dhamana. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka viongozi wote waliopewa dhamana kuheshimu ‘utu’ na haki za kila raia. Ugomvi binafsi, kutofautiana kiitikadi, kiimani na hata kimtazamo kusimfanye yoyote mwenye dhamana kutumia mamlaka yake katika kumuonea mtu yoyote. Kama taifa tuna jukumu la kusimamia misingi ya utu na kuheshiminiana.

68. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mheshimiwa Rais kumchukulia mara moja hatua za kinidhamu Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam. Aidha, Rais aache ubaguzi katika maamuzi ya kinidhamu kwa baadhi viongozi wa umma kwani hii ni kuwa na double standard katika utekelezaji wa majukumu yake.

*MAMLAKA ZA KISHERIA ZA JIJI LA DAR ES SALAAM KATIKA KUSIMAMIA NA KUENDESHA USAFIRI WA UMMA*

69. Mheshimiwa Spika, majiji makubwa duniani yanakabiliwa na changamoto za kuongezeka kwa wakazi wake, jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na za kiuchumi kama vile, afya, elimu, maji, huduma za uokozi, usalama wa raia na huduma za usafiri. Kutokana na ukweli huo, sheria za majiji hayo, zimetoa mwongozo na mamlaka kwa majiji hayo kushughulikia baadhi ya masuala yenye athari za moja kwa moja kwa wananchi wa eneo husika ili kukabiliana na changamoto hizo. Kwa sababu hiyo, Mameya na kamati zao wamepewa mamlaka makubwa ya kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo katika majiji wanayoyaongoza.

*Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Umma Katika Majiji*

70. Mheshimiwa Spika, Ipo Mifumo tofauti ya umiliki na uendeshaji wa usafiri wa umma katika mabara ya Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini. Katika Bara la Asia, nchi nyingi hutumia mfumo wa ushirika kati ya sekta ya umma na sekta binafsi – yaani PPP. Mfumo huo ni tofauti na ule unaotumika na nchi za Bara la Amerika ya Kaskazini ambapo umiliki na uendeshaji upo chini ya mamlaka za manispaa za miji husika. Nchi nyingi za bara la Ulaya huduma ya usafiri kwenye majiji hutolewa na makampuni ya umma na makampuni machache ya watu binafsi.

*Mifano ya baadhi ya Majiji na Mamlaka ya Usimamizi na Uendeshaji wa Usafiri wa Umma*

71. Mheshimiwa Spika, Jiji la London: Jiji hili limeanzisha mamlaka inayoitwa “Great London Authority”. Mamlaka hii iko chini ya Meya wa London. Katika mamlaka hii ya Great London Authoriy, kuna idara maalumu inayoshughulikia usafiri wa wakazi wa London (Transport for Londoners). Kwa kifupi, mfumo mzima wa usafiri wa Umma katika Jiji la London, unaratibiwa na kusimamiwa na mamlaka ya jiji la London na msimamizi mkuu akiwa ni Meya wa Jiji la London.

72. Mheshimiwa Spika, Jiji la Cape Town - Afrika ya Kusini: katika Jiji hili, usafiri wa abiria upo chini ya Ofisi ya Meya. Mamlaka ya Jiji hili imeanzisha chombo kinachoitwa Transport for Cape Town, (TCT) ambacho kinasimamia na kuendesha mradi wa mabasi yaendayo kasi wa “My CiTi Bus Service”. Chombo hiki kina mamlaka ya kupanga, kusimamia, kudhibiti, kutoa mikataba kwa makampuni, na kukarabati miundo mbinu yote ya barabara katika Jiji la Capetown. “The TCT has full mandate and autonomy over issues pertaining, planning, costing, contracting, regulating, monitoring, evaluating, communicating, managing and maintaining the city of Cape Town’s Transport infrastructure, systems, operations, facilities and network”

73. Mheshimiwa Spika, Jiji la Johannesburg –Afrika ya Kusini: Mamlaka ya jiji hili iliunda chombo kinachoitwa Rea-Vaya “the City of Johannesburg's Revolutionary Bus Rapid Transit system. “REA VAYA, which means “we are going”, offers fast, safe and affordable public transport on a network of bus routes across Johannesburg”. Rea-Vaya kwa sasa inaendeshwa kwa pamoja na ushirika wa wenye taxi ambao walikuwa ni wahanga baada ya mfumo huo kuanzishwa na Jiji hilo.

*UANZISHWAJI WA HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM NA MAMLAKA YAKE YA KISHERIA*

75. Mheshimiwa Spika, Jiji la Dar es salaam limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji ) namba 8 kifungu cha 5 (1) na (4) ya mwaka 1982 ambapo Waziri mwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa hutangaza kwenye gazeti la serikali kuanzisha Mamalaka ya Jiji. Majukumu ya Jiji yameainishwa katika kifungu cha 55 (1)(2) cha sheria namba 8 ya mwaka 1982 pamoja na majukumu mengine yaliyoainishwa kwenye jedwali la sheria kama ifuatavyo;
• Kuhakikisha barabara kuu zote ndani ya Jiji Zinakuwa katika hali ya usafi.
• Kusimamia matumizi ya usafiri wa umma kwenye masuala ya gharama za ukodishaji/nauli, njia za magari hayo pamoja na maegesho.
• Mamalaka za Jiji kulingana na majukumu ya Jiji yameainishwa katika kifungu cha 59(h)(i)(l) kuwa kwa ruhusa ya Waziri mamlaka ya Jiji inaweza kuanzisha huduma ya usafiri, kutoza kodi kwenye huduma za Jiji na kuelekeza njia za magari/routes, mitaa ambayo magari yanayotoa usafiri wa umma yatapita bila kuathiri mwenendo mzima wa usafiri wa magari mengine.


76. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine kwa mujibu wa jedwali la sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) ni kama ifuatavyo; 
 kusimamia na kupanga makazi
 kuanzisha na kuendesha masuala ya zimamoto kwenye Jiji
 kuanzisha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya taa katika maeneo ya umma ndani ya Jiji
 kuanzisha na kuendesha usafiri wa umma ndani ya Jiji
 kuanzisha na kuendesha usafiri wa feri au boti
 kujihusisha na biashara au kuanzisha viwanda. 

*MAMLAKA YA JIJI LA DAR ES SALAAM KATIKA KUMILIKI, KUENDESHA NA KUSIMAMIA SHIRIKA LA USAFIRI DAR ES SALAAM (UDA)*

77. Mheshimiwa Spika, Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilianzishwa Mei 1974 chini ya Sheria ya Makampuni (Companies Ordinance, Cap 212) ikiwa na hisa zilizoidhinishwa (Authorised Shares) 15,000,000. Kati ya hiza hizo, hisa 7,119,697 zilizolipiwa (allotted) zilitolewa kwa Serikali kwa asilimia 100 na hisa zilizobaki 7,880,303 zilibaki kama hisa zisizogawiwa (unalloted shares) kwa shirika. Lengo kuu la kuanzisha shirika hilo lilikuwa ni kutoa huduma ya usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam.

78. Mheshimiwa Spika, Ili kuongeza tija na ufanisi wa uendeshaji wa shirika la UDA, mwaka 1985, Serikali iligawa hiza zake 3,631,046 zilizolipiwa sawa na asilimia 51 kwa jiji la Dar es Salaam na hivyo kubakia na hisa 3,488,651 sawa na asilimia 49. Hata hivyo, UDA ilishindwa kujiendesha kutokana na upungufu wa mtaji na udhaifu wa uendeshaji (management) uliochagizwa na ushindani wa kibiashara baada ya Serikali kuruhusu sekta binafsi kutoa huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

79. Mheshimiwa Spika, kutokana na UDA kushindwa kujiendesha, iliwekwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) mwaka 1997 kwa lengo la kuibinafsisha. Ili kutekeleza lengo hilo la kubinafsisha UDA, PSRC ilitangaza uuzaji wa asilimia 49 ya UDA kwa mwekezaji aliyekuwa na nia ya kununua. Hatimaye, Kampuni ya Simon Group Limited ilinunua hisa hizo. Hata hivyo hakukuwa na uwazi katika mchakato wa kuiuzia Kampuni ya SGL hisa hizo na pia mwanahisa mkubwa ambaye ni Msajili wa Hazina hakushirikishwa jambo ambalo lilizua mgogoro juu ya uhalali wa umiliki wa hisa za UDA na hasa ushiriki wa Kampuni ya SGL.


80. Mheshimiwa Spika, pamoja na mchakato wa uuzaji wa hisa za UDA kwa Kampuni ya Simon Group kugubikwa na utata kwa kutozingatiwa kwa utaratibu wa uuzwaji wa hisa za serikali, na pia utata kuhusu uuzwaji wa hisa za Jiji, bado kuna haja ya wadau wa Jiji kukaa pamoja kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinanzani Bungeni inashauri wadau wa UDA wakae na kuweka msimamo wa pamoja kutafuta suluhisho la sakata la UDA kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam. 

81. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa inafahamika duniani kuwa suala la usafiri ndani ya Majiji husimamiwa na Jiji husika na au kwa kushirikiana na sekta binafsi;
Na kwa kuwa ilivyo sasa pamoja na makosa yaliyofanyika tayari Simon Group ndiyo kampuni pekee inayoendesha shirika la UDA bila Halmashauri ya Jiji kuhusika katika kusimamia na kuendesha usafiri wa Dar es Salaam;
Na kwa kuwa hapa nchini vipo vitega uchumi vingi ambavyo vimebinafsishwa bila kuzingatia utaratibu;
Na kwa kuwa imetolewa kauli na Rais kupoka sehemu ya miliki ya hisa za Jiji kama suala la UDA halitapewa ufumbuzi;
HIVYO BASI, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kuwa wadau wa Dar es Salaam kwa maana ya Mameya, Madiwani wakubaliane masuala yafuatayo;
(i) Kuwa, Jiji lipewe hisa na haki ya kuwa sehemu ya kuendesha na kusimamia usafiri wa Dar es Salaam kama ilivyo katika majiji mengine duniani.
(ii) Kuwa, Halmashauri ya Jiji iwe na mamlaka ya kutoa leseni kwa mwekezaji mwingine ambaye atapewa kuwa sehemu ya kutoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam kuliko ilivyo sasa ambapo ni Simon Group Limited pekee wanaoendesha usafiri wa Jiji lote la Dar es Salaam.
(iii) Serikali kuu ibaki na jukumu la kutoa miongozo ya kisera na kusimamia hisa zake katika vikao vya wanahisa na sio kama ilivyo sasa ambapo kwa sasa DART ipo chini ya TAMISEMI ambayo ni ofisi ya Rais.
(iv) Kuwa kuisimamisha kampuni ya Simon Group ambayo inajulikana kuwa ilipata hisa na miliki ya kuendesha usafiri wa Jiji bila kuzingatia utaratibu na njia zilizowazi, na pia ikijulikana kuwa tayari kampuni hiyo imeshakopa fedha kwa kutumia mali za Jiji na pia tayari kampuni hiyo ikiwa tayari inatoa huduma kwa wananchi wa Dar es Salaam, hautakuwa uamuzi wenye maslahi mapana kwa wananchi. 

82. Mheshimiwa Spika, jambo muhimu hapa ni ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na say/stake katika kupanga na kuendesha mradi wa usafiri wa umma kwa kuwa Halmashauri ya Jiji ndio wawakilishi wa wananchi. Kwa maneno mengine, mamlaka za kisheria za Jiji la Dar es Salaam za kupanga na kusimamia usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) 1982 zilindwe na zitekelezwe.

*UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17 NA UCHAMBUZI WA BAJETI INAYOPENDEKEZWA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18*

83. Mheshimiwa Spika, wajibu wa Serikali katika bajeti ni kukusanya mapato na kutumia mapato hayo katika matumizi ya kawaida na maendeleo kwa kadiri itakavyokuwa imeidhinishwa na Bunge. Kwa maneno mengine, ni wajibu wa Serikali kutekeleza Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

84. Mheshimiwa Spika, licha ya Serikali kuwa na wajibu huo, kumeanza kuwa na utamaduni wa utekelezaji mbaya wa bajeti inayoidhinishwa na Bunge. Utekelezaji huu mbaya unatokana na kukosekana kwa umakini tangu bajeti ya serikali inapoandaliwa na pia kuingiza matashi ya kisiasa katika bajeti, jambo ambalo linaifanya bajeti yote kuwa ‘unrealistic’.

85. Mheshimiwa Spika, mfano mzuri wa ukosefu wa umakini, ni katika uandaaji wa bajeti ya 2016/17 inayomaliza muda wake, ambapo kulikuwa na tofauti ya kati ya takwimu zilizokuwa katika vitabu vya mapato, na vile vya matumizi. Kwa mfano, wakati kitabu cha mapato ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaonza tarehe 1 Julai, 2016 hadi tarehe 30 Juni 2017 kinaonyesha kuwa jumla ya mapato yote ya Serikali ni shilingi trilioni 22.063; vitabu vya matumizi ya kawaida na maendeleo vinaonyesha kuwa jumla ya matumizi yote ya Serikali kwa kipindi hicho ni shilingi trilioni 23.847; kwa mchanganuo kwamba: Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) ni shilingi 13,336,042,030,510 na fedha za Miradi ya Maendeleo (Volume IV) ni shilingi 10,511,945,288,575.

86. Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ni kwamba; kwa mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 22.063 ila ikapanga kutumia shilingi trilioni 23.847, kiasi ambacho ni zaidi ya mapato yake kwa shilingi trilioni 1.783. Swali hapa ni kwamba hii shilingi trilioni 1.783 iliyoongezeka kwenye matumizi itapatikana wapi wakati haipo katika kitabu cha mapato? Huku ni kukosekana kwa umakini na ndio chanzo cha utekelezaji mbaya wa bajeti.

87. Mheshimiwa Spika, chanzo kingine cha utekelezaji duni wa bajeti ni kuingiza matashi au maslahi ya kisiasa katika uandaaji wa bajeti. Nasema hivi kwa sababu bajetiya Serikali iliyopitishwa hapa Bungeni kwa mwaka wa fedha 2016/17 ililenga kupata umaarufu wa kisiasa na sio kutatua kero za watanzania. Hii ni kwa sababu ukisoma sura ya bajeti iliyowasilishwa katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango utaona kwamba jumla ya makusanyo yote yalitakiwa kuwa shilingi trilioni 29.539 na matumizi yote shilingi trilioni 29.539 lakini takwimu zilizoandikwa kwenye vitabu vya mapato na matumizi ni tofauti kama nilivyoonyesha hapo juu. Hii ni kuwarubuni wananchi kwamba Serikali imekuja na bajeti kubwa hivyo wategemee unafuu katika huduma za kijamii kumbe ni usanii mtupu.

88. Mheshimiwa Spika, mkanganyiko huo wa takwimu za bajeti: kwamba; Serikali ingekusanya shilingi trilioni 29.5 na kutumia shilingi trilioni 29.5 wakati kwenye vitabu inaonekana ingekusanya trilioni 22.063 na kutumia trilioni 23.8 ndio kunaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani kuiita bajeti hiyo kuwa ni ‘bajeti hewa’ na kwamba mkanganyiko huo ndio kiashiria cha kwanza kikubwa; kwamba bajeti hiyo haikutekelezeka ipasavyo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliita bajeti inayomaliza muda wake kuwa ni hewa kwa sababu iliainisha vyanzo hewa vya mapato. Kwa mfano, kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kukifanya kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa fedha 2016/17, hakuna jina lingine la kukiita chanzo hicho cha mapato isipokuwa ni ‘chanzo hewa cha mapato’ kwa kuwa fedha hiyo itapatika mwaka 2020 wakati wabunge watakapolipwa kiinua mgongo hicho. 

89. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na vyanzo hewa vya mapato, ambavyo vimepelekea kuwa na bajeti hewa, basi hata utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo umekuwa hewa.
90. Mheshimiwa Spika, naomba nitoe takwimu za utaoji wa fedha kutoka hazina kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika wizara mbalmbali hadi kufikia mwezi Machi, 2017 ili kuthibitisha jambo hili. Hadi kufikia mwezi March, 2017 serikali ilikuwa imetumia jumla ya shilingi bilioni 4,168.009 sawa na asilimia 35.26 ya bajeti nzima ya maendeleo ya shilingi 11,820.503 iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge.

91. Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa matumizi ya fedha za maendeleo katika baadhi ya wizara zenye athari ya moja kwa moja kwenye uchumi ni kama ifuatavyo: 
i. Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipewa shilingi 2,251,881,250/= sawa na asilimia 2.22 ya shilingi 101,527,497,000/= zilizoidhinishwa na Bunge.
ii. Wizara ya Viwanda na Biashara ilipewa shilingi 7,200,000,000/= sawa na asilimia 8 ya shilingi 40,000,000,000/= zilizoidhinishwa na Bunge.
iii. Wizara ya Miundombinu ilipewa:
a) Ujenzi wamepewa jumla ya Tshs trillion 1.075 sawa na asilimia 58.71 ya shilingi trilioni 2.176 zilizoidhinishwa na Bunge.
b) Uchukuzi wamepewa jumla ya shilingi bilioni 761.5 sawa na asilimia 30.51 ya shilingi trilioni 2.496 zilizoidhinishwa na Bunge.
iv. Wizara ya Nishati na Madini wamepewa shilingi bilioni 372.877 sawa na asilimia 36 ya shilingi trilioni 1.056 zilizoidhinishwa na Bunge.
v. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wamepewa shilingi 133,872,272,755/= sawa na asilimia 25 ya shilingi bilioni 518.5/= zilizoidhinishwa na Bunge.
vi. Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wamepewa shilingi bilioni 500.452 sawa na asilimia 55.75 ya shilingi bilioni 897.658 zilizoidhinishwa na Bunge.

92. Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo, ni kwamba, Serikali imeshindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2016/17 kwa takriban asilimia 70. Kambi Rasmi haioni muujiza unaoweza kufanyika ili asilimia hiyo 70 ya bajeti ambayo haijatekelezwa iweze kutekelezwa kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha.

93. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini pia kwamba; Bajeti ya Serikali inayopendekezwa kwa mwaka 2017/18 haikuandaliwa kwa umakini. Hii ni kwa sababu kuna tofauti kati ya ukomo wa bajeti ulioainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano na ukomo wa bajeti ulioainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18 

94. Mheshimiwa Spika, Ukomo wa bajeti ulioainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni shilingi trilioni 30.4 wakati ukomo wa bajeti ulioanishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni shilingi trilioni 31.6.

95. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuwa makini katika suala zima la uandaaji wa bajeti kwa kuwa, utekelezaji duni wa bajeti zilizotangulia unatokana kwa kiasi kikubwa na maadalizi dhaifu ya bajeti husika.

*URATIBU USIO WAZI WA MATUMIZI YA BILIONI 6.2 FEDHA ZA MAAFA YA WAHANGA WA TETEMEKO LA ARDHI – KAGERA*

96. Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba tarehe 10 Septemba, 2016 kulitokea tetemeko la ardhi huko Mkoani Kagera – tetemeko ambalo lilisababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Kagera. Kutokana na maafa hayo, wadau na wananchi mbalimbali walioguswa walijitoa kwa hali na mali kwa kuchanga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa maafa hayo.

97. Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza ni kwamba Serikali ilikataza wadau kutoa michango ya moja kwa moja kwa wahanga na badala yake ikaunda kamati maalum ya maafa ambapo ilielekeza watu waliotaka kutoa michango kwa ajili ya maafa hayo wachangie kupitia akaunti maalum ya maafa ya kamati hiyo.

98. Mheshimiwa Spika, Serikali imeripoti kupitia randama ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, kwamba iliratibu upatikanaji wa shilingi bilioni 6.2 (6,235,930,095.04/=) kwa ajili ya maafa hayo ila haitoi maelezo yoyote juu ya namna fedha hizo zilivyotumika jambo linalozua hofu kuwa fedha hizo zilitumika tofauti na ilivyokusudiwa. 

99. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa bado kuna wahanga wa tetemeko ambao bado hali zao ni mbaya kutokana na kukosa misaada; na kwa kuwa Serikali inakiri kuwa ilikusanya shilingi bilioni 6.2 kwa ajili ya maafa hayo, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalumu (Forensic Audit) wa matumizi ya fedha hizo, ili wahanga waweze kujuwa matumizi ya fedha za msaada kwa ajili yao.

*BAJETI YA KUKUZA DEMOKRASIA NCHINI*

100. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/17, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliidhinishiwa na Bunge shilingi bilioni 1.6 (1,684,723,167/=) ikiwa ni fedha za Mradi wa Kukuza Demokrasia Nchini (Democratic Empowerment Project). Hata hivyo, fedha iliyotolewa na hazina hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2017 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ni shilingi milioni 29 (29,085,278/=) sawa na asilimia 2 tu ya bajeti yote iliyoidhinishwa. 

102. Mheshimiwa Spika, kutotekelezwa kwa mradi huu ni uthibitisho kwamba Serikali ya awamu ya tano imedhamira kukandamiza demokrasia hapa nchini. Makatazo ya kufanya mikutano ya siasa, ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari, udhibiti wa watumiaji wa mitandao ya jamii kupitia Sheria kandamizi za Makosa ya Mitandao (Cyber Crime Act), Sheria ya Huduma za vyombo vya habari na Sheria ya Takwimu ni sehemu endelevu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano inayovuta hisia za kuwepo mpango wa kufuta mfumo wa vyama vingi vya upinzani hapa nchini, jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalikemea kwa nguvu zote. Aidha, vitendo hivyo vyenye lengo la kukandamiza demokrasia vinakwenda kinyume na ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema kwamba “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa” 

103. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imefanya jitihada zipi za kukuza demokrasia hapa nchini ikiwa imeshindwa kutekeleza bajeti iliyotengwa na bunge kwa ajili ya mradi wa kukuza demorasia hapa nchini? 

*HITIMISHO*
104. Mheshimiwa Spika, wanazuoni wa Sayansi ya Siasa (Political Science) wanasema kwamba; huwezi kutenganisha siasa na maendeleo. Uhusiano kati ya siasa na maendeleo ni sawa na uhusiano kati ya yai na kuku. Huwezi kuwa na kimoja bila uwepo wa kingine. Kwa sababu hiyo, ili taifa liweze kuwa na maendeleo endelevu ni lazima taifa hilo liwe na mfumo mzuri wa siasa – siasa ambayo inaheshimu misingi ya katiba na utawala wa sheria, siasa ambayo inaliunganisha taifa na sio kulisambaratisha kwa misingi ya tofauti za kiitikadi, kidini, kikabila na mambo yanayofanana na hayo.

105. Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza hapo awali, ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kumfikia kila mwananchi ni lazima uchumi huo uwe shirikishi. Uchumi huo hauwezi kuwa shirikishi ikiwa tunabaguana kwa misingi ya tofauti za kisiasa au tofauti nyinginezo. Uchumi wa nchi yetu hauwezi kujengwa na kundi moja la jamii na kulibagua lingine. Hali kadhalika uchumi wan chi yetu hautajengwa na chama kimoja cha siasa kwa kukibagua kingine au kuchochea migogoro ndani ya vyama vingine. Mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana katika kujenga uchumi ulio imara. Ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda haiwezi kufikiwa tukiwa na msigano wa namna hii.

106. Mheshimiwa Spika, wanazuoni wanasema: “kutofautiana kifikra ni afya ya akili”; na ili uvumbuzi utokee lazime kuwe na fikra mbadala - ‘alternative thinking’. Nilidhani kuwa Serikali na Chama cha Mapinduzi wangetambua kuwa uwepo wa watu wenye fikra mbadala katika taifa hili ni tunu na zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu; lakini badala yake Serikali wameona kuwa uwepo wa watu hao ni kama mwiba na kikwazo. 

107. Mheshimiwa Spika, Nihitimishe kwa kuwashukuru Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia kama kiongozi wao. Naishukuru sana Sekretariat ya KUB kwa namna wanavyokesha kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia uandaaji wa hotuba za Kambi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Freeman Aikaeli Mbowe (Mb)

KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI NA
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU
6 Aprili, 2017

No comments:

Post a Comment