Monday, October 24, 2016

Ukawa: Hatutavumilia upuuzi huu

UCHAGUZI wa Meya katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam leo umevurugwa licha ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijitangazia ushindi, anaandika Faki Sosi.

Pamoja na CCM kujitangazia ushindi, Ukawa wameeleza kuwa, hawatovumilia tena kile walichokiita upuuzi unaopangwa na CCM kwa kushirikiana na serikali kuwahujumu.

Kauli hiyo imetolewa baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutibua mkakati wa CCM kisha kususia uchaguzi huo.

“Kuanzia leo hatutakuwa chama cha kulalamika tena, tutafuata taratibu za kupambana na uonevu unaoendelea kufanyika nchini,” amesema Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho.

Hata hivyo, baada ya Ukawa kususa uchaguzi huo, wajumbe wa CCM walijikusanya na kumchagua mmoja wao kuwa Meya wa Kinondoni, waliomtunuku nafasi hiyo kinyume na utaratibu ni Benjamin Sitta, Diwani wa Kata ya Msasani.

CCM kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali katika Wilaya ya Kinondoni wamekuwa wakipanga namna ya kuiangusha Ukawa kwenye uchaguzi huo jambo ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa jicho la karibu na Ukawa na hata kubaini baadhi ya mbinu hizo.

Ukawa unaowakilishwa na Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) kwenye Manispaa ya Kinondoni, wamegomea uchaguzi huo kutokana na CCM kuongeza idadi ya wajumbe baada ya wajumbe wa Ukawa kuwa wengi.

Kabla ya kugawanywa kwa Manispaa ya Kinondoni na kuwa manispaa mbili (Kinondoni na Ubungo), Meya wa Kinondoni alikuwa Boniface Jacob kutoka Chadema huku naibu wake akiwa Jumanne Amir Mbunju wa CUF.

Baada ya kugawanywa kwa manispaa hiyo, kumeendelea kuwepo na hekaheka zinazofanywa na vyama vya siasa katika kuhakikisha vinatwaa manispaa hiyo.

Kutokana na kuibuka kwa sintofahamu kwenye uchaguzi huo, Ukawa leo wamesusia uchuguzi wa Meya wa Kinondoni kwa madai ya kuondolewa wajumbe halali wa Ukawa na kuingizwa wajube feki wa CCM.

Uchaguzi huo umevurugwa baada ya wajumbe wa Ukawa kutoka nje kwa madai kwamba, uchaguzi huo kuwa kinyume na taratibu. Hata hivyo CCM waling’ang’ania kuendelea.

Halima Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe lilipo kwenye Halmashauri ya Kinondoni ambaye pia ni mjumbe katika Baraza la Halmshauri hiyo amesema kuwa, kilichofanyika katika uchaguzi huo ni ukiukwaji wa sheria.

Mdee amesema kuwa, wajumbe halali wamezuiwa kupiga kura akiwataja kuwa ni Suzani Limo na Salma Mwasa.

Na kwamba, wajumbe wasio halali akiwemo Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi wamejumuishwa.

Amesema, Prof. Ndalichako sio Mkazi wa Kinondoni aliyewahi kushiriki uchaguzi wa Meya wa Ilala pia Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika sio mjumbe halali katika manispaa hiyo.

“Hata hivyo, sheria inaeleza wazi kuwa katika halmshauri moja ni lazima kuwepo na wateuzi wa rais wasiozidi watatu ambapo katika manspaa hii wapo wanne,”amesema Mdee.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa amesema kuwa, awamu hii ya utawala imetupa mazingatio ya sheria na kwamba, demokrasia ipo gizani.

Mbowe amelituhumu Jeshi la Polisi kuwa wakala wa Serikali ya CCM, kutokana na utekelezaji wa majukumu yao kwa upande wa siasa na kwamba chama hicho kina kila sababu ya kuendeleza operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikitekta (Ukuta).

Hata hivyo, ameeleza jinsi uhuru wa vyombo vya habari unavyoanza kuminywa kutokana na kutozuiliwa kwa vyombo vya habari vya wananchi kuripoti tukio hilo.

“Magazeti ya Mwananchi, Mtanzania, Tanzania Daima na MwanaHALISI hayakuruhusiwa kushuhudia mwenendo wa uchaguzi, inaonesha wazi kuwa wanajua kuwa watafanya dhuluma,”amesema.

Amesema kuwa, vyombo vya habari vilivyoruhusiwa ni Telvisheni ya Taifa (TBC1) Daily News, Habari Leo vinayomilikiwa na serikali na Gazeti la Uhuru linalomilikiwa na CCM.

Hata hivyo Dk. Mashinji amesema kuwa, Jeshi la Polisi linatumika kusaidia Serikali ya CCM kupora haki na kuwa, idadi ya polisi leo ilikuwa kubwa kuliko wajumbe wa manispaa hiyo ambao ndio wapiga kura.

Dk. Mashinji amesema kuwa, chama hicho kitaaenda mahakamani kesho kufungua kesi kupinga uchaguzi huo.

Hali ilivyokuwa

Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi za manispaa hiyo mapema asubuhi na kushuhudia Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha ulinzi.

Upande wa kutokea Kituo cha Mabasi cha Magomeni Hospitali, kulifurika wananchi waliokuwa wanasuburi matokeo ya uchaguzi huo huku wakiwekewa uzio.

No comments:

Post a Comment