Thursday, September 1, 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUHAIRISHA MIKUTANO NA MAANDAMANO YA UKUTA


Ndugu wanahabari,

Tarehe 27 Julai ya mwaka huu Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilitangaza azimio la kuanzisha harakati tulizozipa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA). Pamoja na mengine, azimio hili lilipitishwa kufuatia tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa katika nchi yetu hadi mwaka 2020. Kama mnavyokumbuka, Kamati Kuu yetu iliteua siku ya Septemba Mosi, yaani kesho, kuwa ni siku rasmi ya kuanza kwa harakati za UKUTA ambazo zingejumuisha mikutano ya hadhara na maandamano ya amani nchi nzima.

Kufuatia azimio la Kamati Kuu ya CHADEMA, mambo mengi sana yametokea. Mengi ya mambo haya ni ya ajabu na ya kusikitisha sana. Tumemwona Rais wa Jamhuri ya Muungano, aliyekula kiapo cha ‘kuilinda, kuihifadhi na kuitetea’ Katiba yetu na Sheria zake, ‘akiikanyaga’ Katiba hiyo hadharani kwa kutishia kwamba mtu yeyote atakayefanya mikutano na maandamano ya amani ‘atakiona cha mtema kuni.’

Tumeshuhudia Jeshi la Polisi, ambalo lina wajibu kisheria wa kutoa ‘ulinzi na msaada’ ili kuwezesha mikutano kufanyika kwa amani na utulivu, likizunguka mitaani mijini na vijijini na kutembeza hadharani magari ya deraya na silaha nyingine nzito za kivita kwa lengo la kuwatisha wananchi wanaopanga kutekeleza kile ambacho Katiba na Sheria za Tanzania zinawaruhusu kukifanya, yaani, mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.

Tumeona kwa mshangao mkubwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likitoa tamko la vikosi vyake vyote nchi nzima kufanya usafi siku ya Septemba Mosi, wakati Jeshi hilo lilikwishafanya maadhimisho rasmi ya Sikukuu ya Mashujaa tarehe 25 Julai. Na tangu alfajiri ya leo hadi muda huu, JWTZ imerusha ndege za kivita katika maeneo yote ya Dar es Salaam, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya majeshi yetu.

Na wote tu-mashahidi wa jinsi ambavyo viongozi wa ngazi zote wa CHADEMA na wanachama wa kawaida wamekamatwa, kuteswa na kufunguliwa mashtaka ya uonevu kwa sababu tu ya kutetea au kutekeleza haki na uhuru wao kwa mujibu wa Katiba yetu. Aidha, tumeona matukio mabaya ya kihalifu – ya kweli ama ya kutengenezwa – yakihusishwa kwa makusudi na UKUTA ili kutengeneza mazingira ya kiusalama ya kuhalalisha ukiukwaji wa Katiba na Sheria zetu na vitendo vya kutesa waTanzania na kukiuka haki zao za binadamu.

Vile vile, kila mmoja wetu ameona sio tu mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ambayo imewekewa utaratibu wa kisheria, bali pia mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, ambayo haijawekewa utaratibu wowote wa kisheria, ikikatazwa na Jeshi la Polisi. Mahali pengi katika nchi yetu, mikutano ya CHADEMA ya aina hiyo imevamiwa na kuvunjwa na Jeshi la Polisi na viongozi na wanachama wetu kukamatwa ama kupigwa na kuumizwa vibaya.

Ni juzi tu kikao cha pamoja cha Kamati Kuu yetu na Wabunge wetu kimevamiwa na polisi na viongozi wa ngazi za juu wa Chama kama vile Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mh. Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dkt. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu John Mnyika na wajumbe wa Kamati Kuu Mh. Edward Lowassa na Prof. Mwesiga Baregu kukamatwa na kuhojiwa na polisi.

Na hivyo tunavyozungumza, Naibu Katibu Mkuu wetu Zanzibar, Mheshimiwa Salum Mwalimu na viongozi wengine wa chama chetu, wako rumande Bariadi mkoani Simiyu tangu wiki iliyopita, kwa sababu ya kunyimwa dhamana kwa kosa ambalo sheria iko wazi kwamba lina dhamana.

Sio tu uhai wa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao uko hatarini. Uhuru wa vyombo vya habari umeshambuliwa sana katika kipindi hiki. Ndani ya mwezi huu mmoja, gazeti la Mseto limefungiwa na vituo vya radio vya Radio 5 ya Arusha na Magic FM ya Dar es Salaam vimefungiwa kwa kutangaza habari zinazohusu UKUTA.

Ndugu wanahabari,
Yaliyofanywa na Rais Magufuli mwenyewe na Jeshi la Polisi yamefanywa pia na viongozi wa serikali wa ngazi za chini ya Rais, kama vile mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Hawa nao wametoa matamko ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara na kutoa amri za kuwakamata viongozi na wanachama wetu watakaofanya mikutano hiyo. Taasisi za nchi yetu ambazo zina wajibu wa kulinda haki za vyama vya siasa na haki za binadamu kwa ujumla zimejionyesha wazi wazi kutokuwa na uhuru unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria na kikatiba.

Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ana wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, ameshindwa kabisa kulinda na kutetea haki za vyama vya siasa za kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani. Badala yake, Msajili Francis Mutungi amejidhihirisha kuwa adui mkubwa wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu, kwa kuunga mkono matamko batili ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.

Kwa kifupi, katika kipindi cha takriban mwezi mmoja tangu kutangazwa kwa UKUTA, tumeshuhudia Tanzania yetu ikiserereka kwa kasi kwenye mteremko mkali wa utawala wa kidikteta.



Ndugu wanahabari,
Katika mazingira haya, taifa letu limeingia katika taharuki kubwa. Watanzania wa kila rika na wa kila kundi la kijamii wameingiwa na hofu kubwa ya nchi yetu kuingia katika machafuko ya kisiasa na umwagaji damu mkubwa endapo siku ya Septemba Mosi, yaani kesho, tutatekeleza azimio letu la kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani nchi nzima, na majeshi ya ulinzi na usalama yakatekeleza azma yao ya kutumia mabavu ya kijeshi kuzuia au kuzima mikutano na maandamano hayo ya amani.

Ndugu wanahabari,
Kwa sababu ya taharuki hii na ombwe kubwa la uongozi wa kisiasa lililojitokeza tangu tutangaze UKUTA, viongozi wakuu wa kidini wa madhehebu mbali mbali ya dini zote kubwa hapa nchini, yaani, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste ya Karismatiki, Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Mufti Mkuu wa Zanzibar, wametuomba na kutusihi, katika vikao mbali mbali tulivyofanya pamoja nao, tuwape muda wa wiki mbili au tatu, ili waweze kufanya jitihada za kuonana na Rais Magufuli kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu wa kisiasa, ili kuliepusha taifa letu na machafuko ya kisiasa na umwagaji damu, utakaosababishwa na matumizi ya nguvu za kijeshi yanayotishiwa na Rais Magufuli na majeshi yetu ya ulinzi na usalama.

Aidha, sio viongozi wa kidini tu ambao wametuomba kuahirisha UKUTA kwa muda. Viongozi wa taasisi za kiraia kama vile Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Wahariri na Jukwaa la Katiba nao wametusihi tuahirishe UKUTA kwa muda, ili tutoe fursa kwa jitihada za mazungumzo na majadiliano kufanyika.

Sisi CHADEMA tunatambua na kujali haki zetu za kisiasa kama zilivyofafanuliwa katika Katiba na Sheria za nchi yetu. Hata hivyo, tunajali na kuheshimu kwa kiasi kikubwa zaidi, haki ya waTanzania ya ‘kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yao’ kama ilivyotamkwa na ibara ya 14 ya Katiba. Tunatambua mchango mkubwa ambao umetolewa na dini zote hapa nchini katika kutunza utulivu uliopo Tanzania na katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa waTanzania. Tunaelewa rai ya viongozi wetu wa kiroho juu ya umuhimu wa kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa kwa mazungumzo na majadiliano.

Tofauti na wengine ambao wamekataa hata kuwaona viongozi wetu wakuu wa kidini, sisi tunawaheshimu viongozi wetu wa kidini. Tumekutana nao. Tumesikiliza na kutafakari wito wao wa kuahirisha UKUTA kwa wiki mbili au tatu, ili wapate fursa ya kuzungumza na Rais Magufuli na Serikali yake. Huu ni wito wa busara na wenye kulijali taifa letu na watu wake. Sio wito unaopaswa kupingwa kwa sababu nyepesi nyepesi.

Tofauti na wengine, sisi wa CHADEMA hatuwezi kuwakaidi viongozi wetu wa kidini katika wito wao huu wa busara.

Kwa sababu hizi zote, tunaomba kuwatangazia viongozi wetu wa ngazi zote za CHADEMA, pamoja na wanachama, wafuasi na mashabiki wetu na waTanzania wote popote walipo, kwamba tunaahirisha kwa mwezi mmoja mikutano na maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika nchi nzima kuanzia kesho Septemba Mosi, ili kutoa nafasi kwa viongozi wetu wa kiroho kutafuta suluhu ya jambo hili kwa kukutana na Rais Magufuli na Serikali yake.

Endapo jitihada za viongozi wetu wa kidini hazitazaa matunda katika kipindi hicho, mikutano na maandamano hayo ya amani sasa yatafanyika kuanzia Oktoba Mosi ya mwaka huu. Tunawaomba viongozi na wanachama wetu nchi nzima waendelee na maandalizi mbali mbali kwa ajili ya UKUTA katika maeneo yao.

Aidha, tunarudia wito wetu kwa vyama vingine vya siasa, taasisi na mashirika ya kiraia yasiyokuwa ya kiserikali, taasisi za kitaaluma za aina mbali mbali, vyombo vya habari na waTanzania katika ujumla wao, kujiunga na UKUTA na kutetea Katiba yetu na haki za binadamu. Tunasisitiza tena: hakuna atakayepona endapo Rais Magufuli atafanikiwa kuangamiza mfumo wa vyama vingi vya siasa katika nchi yetu kama alivyodhamiria.

Hakuna atakayekuwa salama endapo Rais Magufuli ataruhusiwa kukanyaga Katiba yetu, kupuuza sheria za nchi yetu na kukiuka haki zetu za binadamu kama anavyotaka. Kama inavyotamka Katiba yetu, ‘kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.’ UKUTA ni sehemu ya hatua hizo za kisheria za kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria zetu. Tujenge UKUTA ili tuokoe nchi yetu.

--------------------------------

FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB)
MWENYEKITI TAIFA

No comments:

Post a Comment