Wednesday, August 10, 2016

TUMECHOKA KUVUMILIA!

TUMECHOKA kuvumilia! Ni kauli ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kudai kusakamwa na Serikali ya Rais John Magufuli, anaandika Pendo Omary.

Chama hicho kimetoa kauli hiyo leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya Jaji Mstaafu, Salome Kaganda ambaye ni Kamishna wa Maadili na Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwaandikia barua viongozi wa chama hicho akiwatuhumu “kukiuka masharti ya Hati ya Ahadi ya Uadilifu wa Viongozi wa Umma.”

Jaji Kaganda aliwaandikia barua viongozi hao tarehe 4 mwezi huu ambapo Chadema wameitaka sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kuacha vitisho kwa viongozi wa chama hicho.

Walioandikiwa barua hiyo ni Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.

Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema amesema, kwa mujibu wa barua ya Jaji Kaganda, katika tarehe, muda na siku ambayo haijulikani, viongozi hao wa Chadema walitoa matamshi ambayo yanachochea wananchi kutotii sheria, kufanya vurugu, kudharau misingi ya demokrasia iliyopo nchini na kutishia usalama wa nchi.

“Hata hivyo, Jaji Kaganda hakuyataja matamshi hayo wala kuyafafanua. Aidha, alidai kwamba matamshi hayo yanatokana na maazimio yaliyofikiwa na kikundi cha watu wachache nje ya Bunge,” amesema Dk. Mashinji.

Licha ya kudai kwamba, maazimio ya kikundi hicho yanapuuza utangamano, utulivu na usalama wa wananchi wengine kinyume na dhana ya maslahi mapana ya umma, Jaji Kaganda hakukitaja kikundi hicho cha watu wachache nje ya bunge huku pia akidai matamshi ya viongozi hao yalilenga ‘kushamirisha ‘ maslahi yao binafsi na maslahi ya Chadema.

“Mheshimiwa Mbowe ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama kikuu cha upinzani hapa nchini. Ni kiongozi wa chama ambacho mgombea urais wake alipata zaidi ya kura milioni sita kati ya kura 15 milioni zilizopigwa kwenye uchaguzi mkuu wa urais mwaka jana.

“Ni mbunge wa kuchaguliwa na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Katika Bunge. Ni mtu na kiongozi anayejulikana na kuheshimika ndani na nje ya Tanzania. Kusema kuwa kiongozi huyo anaongoza kikundi cha watu wachache nje ya Bunge kwenyewe ni kuonesha maadili yenye mashaka kwa mwandishi wa barua hiyo,” amesema Dk. Mashinji.

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki ameeleza kushangazwa na barua ya Jaji Kaganda akisema;

“Ni vigumu kuamini kwamba, barua hii imeandikwa na mwanasheria na mtu ambaye amewahi kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Barua ambayo haina maelezo yoyote ya kile kinachodaiwa kuwa kosa; haitaji tarehe, siku, muda au mahali kosa hilo lilipotendeka.

“Haitaji vifungu vya sheria yoyote iliyokiukwa na wala kuonyesha kama sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma ina mamlaka kisheria ya kushughulikia kosa hilo, in onyesha mapungufu makubwa ya kitaaluma na kiuandishi ya kamishna wa maadili na katika mazingira ya kawaida, ingestahili kupuuzwa,” amesema Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama hicho, Chadema haiwezi kuipuuza barua hiyo na kwamba, inaashiria kuwepo kwa njama za kuwafungulia mashtaka katika Mahakama ya Maadili Viongozi hao ambao ni wabunge kwa lengo la kuwavua ubunge.

Aidha, mojawapo ya vigezo vya kikatiba vya mtu kukosa sifa ya kuwa mbunge ni pamoja na kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kamishna wa maadili ana mamlaka ya kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuunda mahakama (Tribunal) ya kusikiliza tuhuma hizo na kupeleka taarifa ya mashauri hayo kwa kamishna ambaye atapaswa kuwasilisha nakala za taarifa hiyo kwa rais na spika wa Bunge.

“Rais Magufuli na washauri wake wanafahamu ugumu wa kutumia mahakama za kawaida kwa lengo la kukandamiza wapinzani.

“Licha ya matatizo yake mengi, Mahakama ya Tanzania imedhihirisha mara nyingi uwezo wa kulinda uhuru wake na kutokuwa tayari kutumika kwa malengo ya kisiasa ya watawala.

“Sasa Magufuli (Rais John Magufuli) na washauri wake wanaandaa mazingira ya kuitisha Mahakama ya Kangaroo watakayoidhibiti wao ili kuhakikisha wanawakandamiza viongozi wakuu wa chama chetu.

“Kama ambavyo tumethibitisha mara kwa mara chama chetu hakitakuwa tayari kuona viongozi wake wakikandamizwa kwa kutumia kivuli cha maadili ya viongozi wa umma. Tutapambana na njama hizo. Kwa uthabiti na kwa weledi ule ule ambao tumepambana na njama nyingine za aina hiyo katika siku za nyuma,” ameeleza Lissu.

Aidha Jaji Kaganda amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo akikana kujua kuhusu barua hiyo huku akisema “mimi sifahamu kuhusu suala hilo, sina taarifa.”


MwanaHalisiOnline

No comments:

Post a Comment