TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kuhusu picha zinazoashiria shari
Jioni hii zimeonekana picha za mtu ambaye anadhaniwa kuwa ni mwanamke ameshika silaha za jadi mikononi mwake, panga, upinde na mishale huku akiwa amevalia nguo zenye rangi na nembo za CHADEMA.
Mtu huyo ameonekana pia akifanya mazoezi huku nyuma yake kukiwa na bendera ya CHADEMA ambayo imeshikwa na watu 'wanaoficha' sura zao nyuma ya bendera hiyo.
Kwa mtazamo wa haraka picha hizo zinamuonesha mtu huyo akijiandaa kwa 'shari' ambayo bila shaka anaijua mwenyewe au na wenzake walioshirikiana naye kupiga hizo picha.
Tungependa kutaarifu umma kuwa picha hizo zisihusishwe kwa namna yoyote ile na Operesheni UKUTA na maandalizi ya Septemba 1 kwa ajili ya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani kwa mujibu wa Sheria za Nchi, ambayo inatarajiwa kufanyika katika kutimiza wajibu na haki za kikatiba za Watanzania.
Tumeona ni vyema kuweka sawa jambo hili baada ya watu mbalimbali wapenda haki ambao wangependa kuona Operesheni UKUTA na Septemba 1, zikifanyika na kuendelea kwa amani ili kufikisha ujumbe mzito na muhimu unaokusudiwa kwa maslahi na matakwa ya Watanzania, kuanza kuhoji kuhusu picha hizo.
Lakini pia tumeamua kutozipuuzia picha hizo baada ya kuona dalili za maadui wa demokrasia na watetezi wa uvunjifu wa Katiba na Sheria za Nchi unaoendelea kufanywa na watawala kupitia kauli, matamko na vitendo, wakilenga kuzitumia picha hizo kuwatisha watu na bila shaka kujazia jazia vinyama kwenye vihoja vyao na propaganda nyepesi za kupindisha maudhui na madhumuni ya Septemba 1 na UKUTA kwa ujumla.
Chama kinalaani vikali matumizi ya nembo za chama yaliyofanywa na watu hao kwa namna inayoashiria shari na vurugu huku ikihusishwa na Operesheni UKUTA na Septemba 1. Waliozipiga na kuzisambaza mitandaoni wanajua makusudi yaliyowatuma kufanya hivyo na bila shaka watapaswa kuwajibika kwa walichofanya.
Tunapenda kusisitiza tena, kama ambavyo Chama kupitia kwa viongozi wakuu kimesema mara kadhaa sasa, Operesheni UKUTA na maandalizi ya Septemba 1, vitatekelezwa kwa misingi inayothamini na kuzingatia uwajibikaji kwa maslahi mapana ya Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na kudai HAKI na KUPINGA UVUNJAJI WA KATIBA na SHERIA za Nchi kwa njia za AMANI.
Tumaini Makene
Mkuu wa Habari na Mawasiliano CHADEMA
No comments:
Post a Comment