Friday, August 5, 2016

Polisi wamnyima Lissu dhamana

JESHI la Polisi, kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemnyima dhamana, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya kumaliza kuhojiwa katika kituo kikuu cha polisi, anandika Shabani Matutu.

Pamoja na jitihada za viongozi mbalimbali wa Chadema kuhangaikia dhamana lakini polisi wamekataa, badala yake walitimua kila mtu aliyekuwepo eneo hilo wakiwamo waandishi wa habari.

Baadhi ya viongozi waliofika ni pamoja na Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema, Edward Lowassa Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu wa Chama hicho, aliyefika saa 12:14 jioni akiungana na viongozi na wanachama wa chama hicho.

Baada ya kufika Lowassa wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya ofisi hizo za polisi walianza kuimba wimbo wa kumuita rais, rais, rais ikiwemo na kauli mbiu ya maarufu ya Peoles power.

Mara baada ya kufika alipokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa amepanda gari moja na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob waliokuwa nje ya geti.

Viongozi hao waliokuwa nje baada ya kuzuiwa kuingia ndani polisi waliongozana na Lowassa kuomba kuingia walizuiwa hali iliyofanya wachukue uamuzi wa kuondoka.

Kiongozi aliyeruhusiwa kuingia alikuwa ni Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Akizungumzia kuhusu hilo, Peter Kibatala mwanasheria wa Lissu amesema kwamba mahojiano kati ya jeshi hilo na mtuhumiwa yalianza saa 9:30 hadi saa 12:30.

“Katika maelezo ya polisi wanasema kwamba eti wakati Lissu akitoka mahakamani juzi kwenye kesi yake eti alitamka maneno ya uchochezi, lakini haya yote yanahitaji ushahidi,” amesema Kibatala.

Wakili huyo anasema kwamba polisi baada ya kumaliza mahojiano na wao wakiwa wameandaa utaratibu wa dhamana walikataliwa hadi kesho atakapofikishwa mahakamani.

“Ninavyojua kesho lazima atafikishwa mahakamani na hapo ndipo tutakuwa tumefanya mipango ya kumpatia dhamana,” alisema Kibatala.

No comments:

Post a Comment