Thursday, July 21, 2016

Lowassa: Tulieni, njia nyeupe 2020

EDWARD Lowassa, aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema safari ya upinzani kushika dola 2020 njia yake ni nyeupe, anaandika Faki Sosi.

Lowassa ambaye aligombea urais kupitia chama hicho na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesema kuwa, serikali ya Rais John Magufuli inarahisisha upinzani kushika dola kwenye uchaguzi mkuu ujao kutokana na kushindwa kuwatumikia wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Lowassa amesema kuwa, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inawanyima maisha ya raha na amani Watanzania kutokana na maisha kuwa magumu.

“Hakuna anayependa maisha haya, kwa namna yoyote hakuna anayependa kushinda njaa. Maisha haya hakuna anayeyatamani.

“CCM inawaonjesha maisha magumu Watanzania, pesa imekuwa ngumu kupatikana,” amesema Lowassa.

Amesema kuwa, ili Chadema kishinde 2020 ni lazima washirikiane na kwamba, wasikubali kufitinishwa.

“Kuna watu maalum wameajiriwa na serikalai kwa ajili ya kutugombanisha, watu hao ni maofisa usalama. Mfumo huu si wa hapa nchini tu, hata huko nje huwa hivyo hivyo,” amesema Lowassa.

Pia Lowassa amekosoa uteuzi wa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika halmashauri mbalimbali nchi.

Amesema, uteuzi huo umefanywa kibaguzi na kuwa haukuzingatia vijana kutoka katika vyama vingine ambavyo vina vijana wenye uwezo na utashi wa uongozi.

“Serikali inasera ya kuongeza ajira kwa vijana, ni kwanini wanabagua? kwanini nyinyi hamjasoma?” amewahoji vijana wa Bavicha.

Hata hivyo, amewapongeza vijana hao kwa kutii katazo liliotolewa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa kutokana na dhamira yao ya kutaka kuzuia mkutano wa CCM unaotarajia kufanyika mkoani Dodoma.

Lowassa amewaambia kuwa, hata yeye alipokuwa kijana alishiriki katika kupinga mambo mbalimbali ambayo yangeweza kuathiri maslahi ya nchi na kwamba, Mwl. Julias Nyerere aliwapongeza.

Lowassa amewasisitiza vijana hao kuwa na mshikamano wa kujenga chama kuanzia ngazi za vjijini.

Hamis Mgeja, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa, nguvu ya mabadiliko imewashtua CCM na kwamba, wamekuwa wakihangaika kutumbuana.

Amesema kuwa, serkaili imekuwa ikiteleza na kuogopa kukoselewa na kuwa “wamekuwa wakiwafunga midomo wapinzani ili wanyamaze.”

No comments:

Post a Comment