FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa amesema kuwa, Serikali ya Rais John Magufuli inalipeleka taifa kwenye ugaidi, anaandika Moses Mseti.
Amesema, kitendo cha serikali yake kuzuia watu kujieleza, kunaweza kusababisha vitendo vya kigaidi kuibuka na kuenea nchini.
Tarehe 7 Juni mwaka huu, Nsato Mssanzya, Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Makao Makuu jijini Dar es Slaam alitoa taarifa ya kuzuia mikutano ya hadhara nchini kwa madai ya kutokuwepo kwa hali nzuri ya usalama.
“Jeshi la Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini kuwa, mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (Civil disorder),” ilieleza taarifa ya CP Mssanzya kwa vyombo vya habari na kuongeza;
“Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 07/06/2016 hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.”
Chadema chini ya Mbowe, hivi karibuni kilifungua kesi ya kuwashtaki Wakuu wa Polisi wa Wilaya za Geita na Kahama, Kamishna wa Mafunzo na Oparesheni wa Polisi Makao Makuu Dar es Salam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa madai ya kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.
Chadema kilifungua shtaka namba 79 mwaka 2016, baada ya kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa iliyopewa jina la ‘Okoa Demokrasia Nchini’ kitendo ambacho kimeibua mjadala mzito kitaifa.
Lengo la mikutano ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini, lilikuwa kuishitaka Serikali kwa Wananchi kwa maai ya kuendesha nchi bila kufuata kanuni na sheria za nchi pamoja na kuzuia kuoneshwa moja kwa moja vikao vya Bunge.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.
Amesema kuwa, kitendo cha Serikali ya Awamu ya Tano kuzuia Watanzania kupokea mawazo mbadala kutoka kwa vyama vya upinzani nchini, ni sawa na ugaidi hivyo wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kusema.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro amesema kuwa, kuwakataza Watanzania kuzungumza ni jambo wanaloliona linakwenda mrama na hivyo kukaribisha vitendo vibaya ikiwemo ugaidi.
“Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wao wanakataza watu kuzungumza kile ambacho wanaona kinakwenda marama na watu kutoa mawazo yao ili wao wenyewe waendelee kuonekanakwa Wananchi,” amesema Mbowe.
Pia amesema kuwa, chama hicho hakitabadilisha uamuzi wao mpaka pale mwafaka utakapopatikana kortini.
Amesema kuwa, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ambaye anadaiwa kuendesha nchi kidkiteta, inaminya uhuru wa Wananchi wa kujieleza kitendo ambacho amesema hakikubaliki.
No comments:
Post a Comment