Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016, ilifunguliwa jana na kusimamiwa na mawakili watatu Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.
Licha ya kuwepo na ulinzi mkali wa jeshi la polisi uliowekwa katika barabara zote za kuelekea Mahakama Kuu, viongozi na wafuasi wa Chedema walifanikiwa kuvuka vizuizi hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka mahakamani jana jioni, Mbowe alisema sababu za kufunguliwa kwa kesi hiyo ni baada ya kuona demokrasia ya vyama vingi "inabakwa nchini."
Mbowe alisema watu wanne waliotajwa katika kesi hiyo ya madai ni Kamanda wa Polisi wilayani Geita, Kamanda wa Polisi wilayani Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema wadaiwa hao wamefunguliwa kesi kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa nchini, kwa kuchukua maamuzi ambayo hayaendani na demokrasia.
“Tunaiomba mahakama itangaze amri ya jeshi la polisi ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni batili, utekelezaji unaofanywa ni batili, polisi wapewe tangazo la kutowanyanyasa wapinzani na pia itoe amri ya vyama vya siasa kufanya mikutano yake na polisi wawe walinzi wa mikutano hiyo,” alisema Mbowe.
Alisema pamoja na polisi kuwabana hawataondoka jijini Mwanza, na wataongezeka zaidi mpaka kieleweke.
Alisema upo mkakati wa makusudi kuhakikisha Chadema inafutika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na baadhi ya viongozi wake kutekwa na kunyanyaswa na polisi.
Mkutano huo na waandishi wa habari ulihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Saidi Issa Mohamed, Dk. Vincent Mashinji (Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Zanzibar), Halima Mdee (Mwenyekiti Bawacha) na Pastrobass Katambi (Mwenyekiti Bavicha) na baadhi ya wabunge wa chama hicho.
Kesi hiyo ya madai inatarajiwa kupangiwa Jaji Jumatatu ijayo.
Polisi ilisambaratisha mkutano wa Chadema uliokuwa ufanyike Kahama katikati ya wiki, ambapo mabomu ya machozi na magari ya 'washawasha' vilitumika kuondoa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wasikilize hotuba za viongozi wa kitaifa.
Chadema imepanga kufanya mikutano nchi nzima kulaani inachodai uonevu unaofanywa dhidi ya wabunge wake Bungeni.
No comments:
Post a Comment