Thursday, March 10, 2016

Waitara: Ukawa hatutalala umeya Dar hadi kieleweke.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaendelea kupambana dhidi ya mbinu chafu zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Alizitaja mbinu hizo kuwa ni kuahirisha uchaguzi huo mara tatu bila sababu za msingi ikiwamo kisingizio cha zuio la Mahakama kwa ajili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 26 ambalo limebainika kuwa halikuwa halali.

Waitara aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kivule mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuwashukuru wananchi hao kwa kumchangua kwa kura nyingi, hivyo kuwa miongoni mwa wabunge 10 nchini waliopata kura nyingi.

Alisema iwapo juhudi zao za kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam zitafanikiwa, kazi ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha wanafuta sheria ya kuwazuia bodaboda wasiingie mjini na kutumbua jipu la mradi wa mabasi yaendayo haraka (Darts) kusuasua.

“Hatuwezi kuachia nafasi hiyo kwani CCM wakiipata utekelezaji wa majukumu ya kuleta maendeleo kwa jamii kupitia Ukawa utakuwa mgumu, hivyo lazima tuvuke vikwazo vyote,” alisema.

Alisema nafasi ya meya wa Jiji ni muhimu kwa kuwa ndiyo nafasi pekee inayoratibu itifaki za viongozi wa nchi, hivyo CCM hawapendi mpinzani apewe jukumu hilo na ndiyo sababu wanatafuta kila sababu kupunguza kasi ya Ukawa.

Aliongeza kuwa itakuwa ndoto kwa CCM kushinda kwa kura kwenye uchaguzi wa meya wa Jiji kwa kuwa ina wajumbe 76 wakati Ukawa ina wajumbe 87, hivyo ipo tofauti ya wajumbe 11.

Aidha, Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule, alisema wananchi wakiona Mbunge wa upinzania anapigiwa makofi na chama tawala wafahamu ni msaliti na anapaswa kufukuzwa.

“Nyote mtakuwa mashahidi, nilivyokamatwa na polisi kisha kuwekwa lupango kwenye sakafu aliyolala Masamaki, lakini nilipofika mahakamani nilijidhamini mwenyewe, kiukweli sijampiga RAC (Katibu Tawala wa Mkoa),” alisema.

Mmoja wa wakazi hao, Juma Hamis, alisema wanashukuru kupata taarifa kutoka kwa mbunge wao, lakini wao wanahitaji maendeleo ya kuboreshewa miundombinu ya barabara, maji na umeme.

“Tumechoka na ahadi za wanasiasa, tunahitaji vitendo kuliko maneno,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment