Sunday, March 6, 2016

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA ILIYOKUTANA MACHI 1, 2006, JIJINI DAR ES SALAAM

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO



TAARIFA KWA UMMA KUHUSU
MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA ILIYOKUTANA MACHI 1, 2006, JIJINI DAR ES SALAAM


Kamati Kuu ya Chama imesema kuwa tangu utawala wa awamu ya tano chini ya Serikali ya CCM ikiongozwa na Rais John Magufuli uingie madarakani, misingi ya uongozi bora na demokrasia ya vyama vingi imeyumba, kiasi cha kuiingiza nchi katika sintofahamu kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala na kutishia mstakabali wa nchi.

Akitoa maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe ametaja masuala kadhaa ambayo yameanza kuharibu sifa Tanzania kwa kuvunja misingi ya demokrasia kuwa ni pamoja na ‘uhuni’ wa kisiasa unaofanywa na Serikali, vyombo vya dola kwa kushirikiana na CCM kupora haki ya wananchi katika uchaguzi wa mameya na wenyeviti wa halmashauri hasa maeneo ambako vyama vinavyounda UKAWA vimeshinda.

Katika muktadha huo, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa Kamati Kuu katika kikao chake hicho kilichoketi Machi 1, mwaka huu, imazimia kwa kauli moja kuwa Chadema haitaendelea tena ‘kuomba’ haki ya kufanyika uchaguzi na hatimaye kuongoza Jiji la Dar es Salaam kupitia Meya na Naibu wake, wanaotokana na UKAWA, bali itaidai haki hiyo, ambayo imepatikana kutokana na mapenzi ya wananchi wa jiji hilo kwa vyama vinavyounda UKAWA.

Mwenyekiti Mbowe amewaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu katika kikao hicho cha siku moja, ilijadili na kutafakari kwa kina, pamoja na masuala mengine, mambo yafuatayo:

1. Hali ya kisiasa nchini.

2. Kutathmini uhai na nguvu ya chama.

Kwa kuanzia, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa kwa Mamlaka ya Kikatiba, ibara ya 6.1.3 inayopewa nguvu na ibara ya 7.5.1, Chama kimeamua kuimarisha uongozi wa kichama mkoani Dar es Salaam, kwa kuanzisha Kamati Maalum itakayosimamia eneo linalojulikana Dar es Salaam Kuu (Greater Dar es Salaam) ambayo pamoja na mambo mengine, wajibu wa awali itahusika katika kuratibu upatikanaji wa haraka wa kikatiba, kisheria na kikanuni wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mbowe, Kamati hiyo Maalum itakayokuwa chini ya Uenyekiti wa Mwita Waitara (Mb), Makamu Mwenyekiti Bernard Mwakyembe (Diwani) na Katibu Henry Kilewo ikiwa na wajumbe 25, pia itahusika katika mambo mengine yanayohusu uimarishaji wa chama na usimamizi wa shughuli zote zinazohusu utendaji wa wawakilishi wa chama katika vyombo vya serikali hususan katika eneo la Dar es Salaam Kuu.

Suala jingine lililodhihirisha kuyumba kwa misingi ya uongozi bora na demokrasia ya vyama vingi ni uchaguzi wa Zanzibar ambao Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa washindi halali wa nafasi ya Rais na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamenyimwa haki yao hali ambayo hadi sasa imesababisha sintofahamu kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala Zanzibar, akisisitiza kuwa msimamo wa Chama cha CUF ndiyo msimamo wa CHADEMA kuhusu hali tete inayoendelea visiwani humo.

Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza masuala mengine ambayo yameiharibia sifa nchi katika kusimamia misingi ya demokrasia na uongozi bora, kuwa ni pamoja na namna Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya dola vilivyosimamia Uchaguzi Mkuu na kutumika kupora haki ya wananchi ya kuchagua na kupata viongozi wanaowataka.

Suala jingine ni juhudi za makusudi zinavyofanywa na watawala wa awamu ya tano kudhibiti mhimili wa Bunge usitekeleze wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia serikali, akitolea mifano kadhaa ikiwemo kuzuia TBC kurusha vikao vya bunge moja kwa moja, Serikali ya CCM kuingilia uundwaji wa uongozi wa Kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma (PAC na LAAC).

“Pia serikali hii hii ya CCM imeingilia mhimili wa bunge na kudhibiti uundwaji wa Kamati mbalimbali za bunge kwa kutumia visivyo au nje ya taaluma, uzoefu na uwezo wao wabunge wa kutoka vyama vyote ambao walionesha ujasiri wa kuikosoa Serikali katika mabunge yaliyopita…jambo ambalo kwa upande wa Kamati za PAC na LAAC tumekataa CCM watuamulie kinyume na sheria na kanuni za bunge.

“Jeshi la Polisi kwa maelekezo ya Serikali limeendelea kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya upinzani, ilihali CCM, viongozi wao, wanachama na wafuasi wao wakifanya maandamano na mikutano maeneo mbalimbali ya nchi bila kuzuia na polisi. Yote haya yanafanyika, Magufuli anajua, Majaliwa anajua.
“Viongozi wetu, wanachama, wafuasi na hata mashabiki wa vyama vya upinzani wanafunguliwa mashtaka yasiyokuwa na msingi pale wanapodai haki za kikatiba za kutekeleza wajibu wao wa kisiasa katika mazingira huru yenye uhakika. Wameamua hata kudhibiti kwa kuvitisha na hata kuvifuta vyombo vya habari ambavyo vinatimiza wajibu kikamilifu kwa jamii na havifungamani na CCM moja kwa moja. Yote haya yanafanyika Magufuli anajua, Majaliwa anajua,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;

“Ni vyema kuelewa kuwa hatua ya misingi ya utawala bora na demokrasia ya vyama vingi ambayo kama nchi tulikuwa tumeifikia kiasi cha Tanzania kujipambanua miongoni mwa nchi za Afrika hasa Kusini mwa Sahara yalikuwa ni matokeo ya mapambano ya zaidi ya miaka 20 kupigania demokrasia katika taifa hili. Leo watu wanataka nchi iongozwe kwa kauli za mtu au watu badala ya misingi ya katiba, sheria na taratibu ambazo nchi imejiwekea.”

Mwenyekiti Mbowe amehitimisha kwa kusema, Kamati Kuu imeazimia kwamba namna ya kukabiliana na hila, njama, mipango ovu ya CCM dhidi ya wapinzani, hali ya kisiasa nchini kwa kina pamoja na Mkakati wa Chama wa Miaka 5 ijayo, itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika kikao cha Baraza Kuu kitakachofanyika jijini Mwanza, Machi 12 mwaka huu ambalo pia litaweka dira na mwelekezo wa chama kuelekea mwaka 2020.

Imetolewa leo Machi 5, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment