Friday, March 18, 2016

Uchaguzi wa Meya Dar waota mbawa

UCHAGUZI wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam bado ni kitendawili licha ya Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa na idadi kubwa ya wajumbe kuliko Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini bado hawaishi vikwazo, anaandika Happyness Lidwino.

Wajumbe halali walioshiriki katika uchaguzi wa mameya wa Halmashauri za Manispaa Jijini ni 163 huku CCM wakiwa 76 na Ukawa 87, kwa hivyo Ukawa kuwazidi CCM wajumbe 11.

Akizungumza na waandishi leo Jijini Mwita Waitara Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam Kuu ‘’The Great Dar’’ amesema wanashangazwa na mbinu zinazotumiwa na CCM kwa kuwashirikisha watumishi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema CCM wanafanya kila mbinu ili kulipoka Jiji licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiga kura. Mbinu hizo pia wamemshirikisha Willson Kabwe Mkurugenzi wa Jiji kuvunja sheria katika majukumu yake.

Mbinu nyingine waliyoitumia ni kuwaandaa wanachama feki wa CCM wakiongozwa na wakili Elias Nawela kufungua kesi ya madai huku wakitaka wajumbe 9 toka Zanzibar na 11 kutoka mikoa mingine kushiriki uchaguzi wa meya.

Waitara amesema, kesi hiyo yenye jarada namba 39 ya mwaka 2016 wameshaomba kujiunga na kesi hiyo huku wakiwa na mawakili wa kutosha ambapo inatarajiwa kusomwa Machi 21 mwaka huu katika Mahakama ya Kisutu.

‘’CCM haina ujanja kwa sasa kwani tunapambana nao, na hatutakubali wajumbe wasiohusika kupiga kura wakati ni kinyume cha sheria ya Serikali za Mitaa za mwaka 1982 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2006,’’ amesema Waitara.

‘’Juzi tumepokea barua kutoka kwa Mkurugenzi ya mwaliko wa ushiriki katika uchaguzi wa meya wa Jiji lakini ndani ya barua hiyo kuna kitu hatujakubaliana nacho. Barua inaeleza uchaguzi utafanyika Machi 22 mwaka huu ukumbi wa Kareemjee lakini wanaotakiwa kuingia ni wajumbe tu,.

Wananchi na wafuasi wa vyama hawataruhusiwa kushuhudia ucha guzi huo. Tunajua hizo ni mbinu za CCM kwa kuwa kuna uovu umepagwa kufanyika siku hiyo.

Kufuatia hali hiyo Waitara amesema Ukawa umemwandikia barua Mkurugenzi huyo ya kutokubaliana na matakwa yake ya kuzuia wafuasi wa vyama kuingia ukumbini wakati wa uchaguzi kwani ni uvunjifu wa sheria na kwamba hawatakubali, bali watawapigania na kuhakikisha wananchi wanaingia ukumbini.

Aidha, kuhusu kesi iliyopo mahakamani watahakikisha sheria inafutwa hata kama uchaguzi utapelekwa mbele lakini hawatakubali kuruhusu mamluki wa CCM kuingia ukumbini kwani wao hawatashiriki uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment