HAIKUWA kazi rahisi kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam,anaandika Happyness Lidwino.
Wafuasi na wanachama wa Ukawa leo mapema walifika katika Ukumbi wa Kareemje kushugudia uchaguzi wa Meya.
Ulinzi ulikuwa mkali getini huku wananchi wakizuiwa kuingia ukumbuni, viongozi na wajumbe waliotakiwa kupiga kura waliingia kwa kukaguliwa na polisi.
Mara baada ya wajumbe wa pande zote kuwasili ukumbini humo, mkutano ulifunguliwa saa 4:37 asubuhi na kura zilianza kupigwa huku Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Ukawa akishuhudia tukio hilo.
Mara baada ya wajumbe kumaliza kupiga kura kabla ya kuhesabiwa, wajumbe wa CCM walianza walinyanyuka na kutoka nje.
Hali hiyo iliwashangaza wengi waliokuwa ukumbini humo, walipofika nje ya ukumbi walianza kuzomewa na wafuasi wa Ukawa.
Safari hiyo ikahitimishwa kwa Isaya Mwita Charles (Chadema) kutwaa nafasi hiyo kwa kura 84 na kumbwaga mpinzani wake Yusuph Omary Yenga (CCM) aliyepata kura 67.
Safari ya mafanikio ya Ukawa katika Jiji la Dar es Salaam ilitawaliwa na vuta nikuvute. Kulikuwa na michezo michafu.
Jeshi la Polisi pamoja na Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam vililaumiwa kwa madai ya kushiriki katika hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM kutaka kushinda kwa hila nafasi hiyo.
Jumla ya wajumbe wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji ni 163. Kwa upande wa Kinondoni kulikuwa na wajumbe 58; CCM wakiwa 20 na Ukawa 38. Temeke jumla ya wajumbe 49, CCM wakiwa 31 na Ukawa 18 na Ilala jumla ya wajumbe 54 huku CCM wakiwa 23 Ukawa 31.
Umoja na mshikamano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) ndio umeiangusha CCM.
Safari ya Ukawa kusaka nafasi ya Umeya katika Jiji la Dar es Salaam ilianza tarehe 23 Januari wakati Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipoitisha uchaguzi huo kwa mara ya kwanza.
Kwa mara ya kwanza uchaguzi huo uliitishwa tarehe 23 Januari na kusindwa kufanyika kutokana na kuwepo kwa mvutano wa wajumbe halali wa uchagzi huo.
Mzozo huo uliibuka baada ya CCM kuingiza wajumbe kutoka Zanzibar na kutaka kuwa sehemu ya wapiga kura, hatua hiyo iligomewa na Ukawa na kusababisha kuanza kwa mnyukano.
Hatua hiyo ilimlazimu Sarah Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kughairisha uchaguzi huo ambapo alipanga kufanyika tarehe 8 Februari mwaka huu.
Licha ya Sarah kuitisha uchaguzi huo tarehe 8 Februari mwaka huu, Sarah alighairisha uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa zuio la mahakama
lililopelekwa katika Mahakama ya Kisutu Februari 5 na mwanachama wa CCM.
Sarah kwa nafasi yake, aliitisha uchaguzi huo tarehe tarehe 27 Februari mwaka huu na baada ya taratibu zote kufuatwa, alisimama na kughairisha uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa zuio kutoka mahakamani jambo ambalo liliibua vurugu.
Wabunge, madiwani kukamatwa
Tuhuma ziliibuka kwa wajumbe wa Ukawa kwamba walishiriki kumshambulia Terresia Mmbando, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kughairishwa kwa uchaguzi huo wa tarehe 27 Februari mwaka huu.
Tuhuma hizo zilisababisha baadhi ya wabunge na madiwani wa Ukawa kukamatwa na Jeshi la Polisi na baadaye kufikishwa mahakama kujibu tuhuma hizo.
Kundi la kwanza kukamatwa lilikuwa ni Halima Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, Mwita Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga na madiwani watatu na kisha kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu.
Jeshi la Polisi kisha lilimkamata Saed Kubenea, Mbunge wa Ubunge kwa tuhuma zile zile za kumshambulia Mmbando, watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Hatua ya vuta nikuvute iliyofanywa na jiji ilionywa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa kwamba ina madhara na kwamba, hawatoomba ila watachukua nafasi hiyo.
George Simbachawene, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alichoshwa na hali hiyo ambapo alimtaka Sarah kuitisha uchaguzi huo kabla ya tarehe 23 mwezi huu.
Katika hali ya kuonesha kuelemewa, Rais John Magufuli alishauri ‘walioshindwa washindwe na walioshinda washinde.”Mafanikio ya Ukawa leo katika Jiji la Dar es Salaam alianza siku nyingi.
No comments:
Post a Comment