Sunday, February 14, 2016

Siku 200 za kishindo cha Lowassa Ukawa

Wakati jana Rais John Magufuli akitimiza jana siku 100 tangu aingie Ikulu, aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, Edward Lowassa, leo anafikisha siku ya 200 tangu alipohama rasmi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani, alitangaza kuachana na CCM Julai 28, 2015, baada ya kile kilichoelezwa kuwa ni kuondolewa ‘kimizengwe’ katika orodha ya ‘tano bora’ kutoka katika makada 38 waliojitokeza kuwania urais ndani ya chama hicho tawala.

Hata hivyo, baadaye Lowassa alitimiza ndoto yake ya kugombea urais baada ya kupitishwa na Chadema kuwania nafasi hiyo, huku akiungwa mkono pia na NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF) ambavyo, pamoja na Chadema, vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwa kila nafasi kupitia muungano wao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Lowassa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo baada ya kupata asilimia 39.97 ya kura halali zilizopigwa huku Magufuli akiibuka kidedea kwa kupata asilimia 58.46 ya kura hizo.

Wakizungumza na Nipashe kuhusiana na siku 200 za Lowassa ndani ya Ukawa, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa walisema kuwa uwepo wa mwanasiasa huyo katika kambi ya upinzani umeongeza changamoto kubwa kwa chama tawala (CCM), pengine kuliko wakati wowote ule tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

“Kishindo cha kutua kwa Lowassa kwa kambi ya Ukawa kimeipa changamoto kubwa CCM… makada wake kadhaa muhimu wakiwamo wenyeviti wa mikoa, walihama na kumfuata Lowassa.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alifanya uamuzi kama wa Lowassa,” mmoja wachambuzi wa masuala ya siasa aliiambia Nipashe. “Wapo pia mawaziri walimfuata Lowassa na kuipa nguvu Chadema na Ukawa kwa ujumla. Halikuwa jambo dogo.
“Kuna watu wamehamasika zaidi na kupata matumaini mapya kuhusiana na jitihada za upinzani katika kutwaa madaraka na kuleta mageuzi ya kweli.

“Ameongeza wafuasi kwa Ukawa, ushahidi ni idadi ya watu waliokuwa wakijitokeza kwenye mikutano wakati wa kampeni, kuongezeka kwa idadi ya kura za urais na pia kuongezeka kwa idadi ya wabunge na madiwani wanaotoka Ukawa. Amechangia sana katika kuupa nguvu upinzani.”

Akieleza zaidi, mchambuzi mwingine alisema kutokana na athari za kuhama kwa Lowassa katika kipindi kifupi kabla ya uchaguzi, CCM ilionekana wazi ikitumia nguvu zaidi katika kampeni zake ili kuhakikisha kwamba inarejea madarakni.

“Hakuna asiyejua kuwa CCM ililazimika kufanya kazi ya ziada ili kuendelea kuongoza. Kampeni zilikuwa kubwa ziadi, ahadi nzito zikatolewa zikiwamo zile zilizoonekana wazi kuwa utekelezaji wake ndani ya miaka mitano hautakuwa rahisi,” alisema mchambuzi huyo.

Kadhalika, inaelezwa kuwa kujiunga kwa Lowassa katika kambi ya Ukawa kumefuta mtazamo potofu uliokuwapo awali kuwa watu wazito na waliowahi kushika nafasi za juu serikalini kama ile ya uwaziri mkuu hawawezi kuhamia upinzani.

“Ilizoeleka kwamba mara nyingi, watu wanaohamia upinzani ni wale tu waliopata misukosuko na kutimuliwa ndani ya chama tawala (CCM),” alisema mchambuzi mwingine mzoefu wa siasa za Tanzania.

“Lakini Lowassa alihamia Ukawa kwa hiari yake na siyo kutimuliwa. Uamuzi wake umeleta mtazamo mpya kuhusu upinzani na ndiyo maana haikushangaza kuona vigogo kama Sumaye wakihamia pia upinzani. Kwa ufupi, Ukawa wamenufaika zaidi na ujio wa Lowassa.”

Mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya diplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Israel Sosthenes, alisema kuondoka kwa Lowassa CCM kulitikisa chama hicho tawala na kwamba, kisiasa, hiyo ni faida kwa kambi ya upinzani ambayo ilipata wafuasi kadhaa kutoka upande huo.

“Tangu siku aliyotangaza kuondoka CCM, umoja ndani ya chama hicho katika baadhi ya maeneo uliyumba… na ushahidi ni kwamba tangu siku hiyo, matamko mbalimbali yalisikika kutoka kwa viongozi wakubwa ndani ya chama hicho,” alisema Sosthenes.

Hata hivyo, alisema kazi kubwa inayofanywa sasa na Rais Magufuli katika uongozi wa nchi inaweza kusaidia katika kuijenga upya CCM ambayo iliyumbishwa kwa kiasi kikubwa na kishindo cha Lowassa akiwa Ukawa.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atik, alisema kwake yeye, Lowassa anamfananisha na kazi ya mbolea shambani, kwani ujio wake umeiongezea nguvu kambi ya upinzani na kukuza demkorasia.

Alisema siyo jambo dogo kwa nchi za Afrika kuona mawaziri wakuu wastaafu wakibaki na heshima zao nje ya mfumo wa chama tawala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk. Benson Bana, alisema kuondoka kwa Lowassa kunatoa mwanya kwa CCM kujitathmini na kurekebisha kanuni za chama chao ili kuzingatia matakwa ya wapiga kura.

“Kwa chama chochote, kuondokewa na kada wa siku nyingi lazima mtatetereka. Na hakuondoka peke yake bali aliondoka na makada wengi,” alisema Dk. Bana.

Alisema katika siku zote za kuwa Ukawa, Lowassa amechangia kuuimarisha upinzani na kuijenga Chadema huku naye akiimarika zaidi kisiasa kwani tangu alipojiuzulu uwaziri mkuu, hakuwahi kupata umaarufu kama alipojiunga Ukawa.

Kabla ya hapo, alisema Dk. Bana, jina lake lilikuwa likihusishwa zaidi na tuhuma za ufisadi.

Mara baada ya kutua Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Ukawa, aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alipinga na mwishowe kuwa kando, sawa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ambaye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake.

WASEMAVYO MBOWE, MAGDALENA SAKAYA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema katika kipindi cha siku 200 zinazotimia leo za kuwapo kwa Lowassa upinzani, wameimarika zaidi na kupata nguvu kwa kiasi kikubwa kulinganisha na awali.

Alisema Lowassa amekuwa mfano wa wanasiasa mahiri na mtendaji na ndiyo maana hata Rais Magufuli na CCM wamekuwa wakitekeleza kwa vitendo baadhi ya ahadi alizotoa kupitia kauli mbiu ya ‘mabadiliko’.

“Nataka kusema jambo moja, Lowassa ameongeza nguvu ndani ya chama… hivi sasa tumeimarika zaidi na hatuwezi kutikisika kwa jambo lolote,” alisema Mbowe.

Akitolea mfano wa kile anachoeleza kuwa ni kuigwa kwa fikra za Lowassa na Ukawa, Mbowe alisema Rais Magufuli amekuwa akitumia falsafa ya Lowassa ya kutaka Tanzania inayolenga kujitegemea kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake yenyewe pamoja na kuongeza uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.

“Hata kauli ya utendaji kazi ya Dk. Magufuli kwa kauli mbiu ya Hapa Kazi tu ni matokeo ya kile alichokianzisha Lowassa,” alisema Mbowe.
“Kinachofanyika sasa ni kwamba, CCM imeichukua na kutekeleza. Hata hivyo, siyo vibaya.”

Akizungumzia siku 200 za Lowassa ndani ya Ukawa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, alisema ujio wa Lowassa katika kambi hiyo umewanufaisha kwa mengi ikiwamo kuongezeka kwa viti vya udiwani na ubunge kulinganisha na miaka iliyopita.

Akieleza zaidi, Prof. Safari alisema Lowassa amekuwa kiongozi shupavu na hodari, tena asiyependa vurugu na ndiyo maana amekuwa kimya na kuhimiza utulivu licha ya kutambua wazi kuwa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) hayakuwaridhisha wengi wapendao mabadiliko kwani yalikuwa na kila dalili za kuchakachuliwa.

“Kwa upande wetu (Ukawa), tumeimarika zaidi kwa ujio wa Lowassa. Na tuna imani tutaimarika zaidi siku zijazo. Kama hivi sasa anatimiza siku 200, basi atatimiza siku nyingi zaidi akiwa upinzani na hivyo kutuletea mafanikio mengi,” alisema Prof. Safari.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema tangu Lowassa ajiunge Ukawa, amekuwa ni chachu ya mafanikio kwao na taifa kwa ujumla kutokana na changamoto mbalimbali anazoziibua.

“Kwa nafasi yake, ni wazi kwamba Lowassa hakuangalia chama wala maslahi binafsi wakati akiihama CCM… aliangalia maslahi ya taifa, hivyo maamuzi yake yalikuwa yana manufaa kwa taifa,” alisema Sakaya.

Alisema hata CUF imenufaika vya kutosha kupitia Lowassa kwani kwa kiasi kikubwa, hamasa yake imesaidia jitihada za kuongeza idadi ya wabunge wao upande wa Bara kutoka wawili wa kuchaguliwa waliokuwapo awali kutokana na uchaguzi uliopita hadi kufikia 10.

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema mara baada ya jina la Lowassa kukatwa na kutokuwamo katika majina ya wagombea watano, minong’ono mingi ilianza na kuhamia kwake upinzani akitokea CCM kumedhihirisha kuwa inawezekana kwa makada wa hadhi yake kuhama bila shida yoyote.

Alisema anachokiona ni kwamba katika siku 200 anazotimiza tangu ahamie upinzani, Lowassa amefanikiwa kuwabadili fikra wafuasi wengi waliokuwa CCM ambao sasa wanaunga mkono upinzani.

SIKU 200 ZA KISHINDO
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa ni kweli, kutua kwa Lowassa Ukawa kulifuatana na mambo kadhaa mazuri kwa umoja huo.

Baadhi ya mambo hayo ni kuwavuta makada wazito wa CCM ndani ya Ukawa, kuongeza wafuasi katika mikutano yao, kuwezesha Ukawa kupata kura nyingi za urais, kuongeza idadi ya wabunge na madiwani na pia kuongeza idadi ya halmashauri zinazoongozwa na Ukawa.

ONGEZEKO KURA ZA URAIS
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chadema iliyomsimamisha Dk. Slaa ilipata kura 2,271,941 (asilimia 26.34), CUF iliyomsimaisha Prof.

Lipumba ilipata kura 695,667 (asilimia 8.067) na NCCR iliyowakilishwa na Hashim Rungwe (hivi sasa yuko Chaumma) ilipata kura 26,388 (asilimia 0.31), hivyo jumla ya kura zao kuwa 2,993,996, sawa na asilimia 34.72 ya kura zote halali zilizopigwa.

Katika uchaguzi uliopita, Lowassa aliyekuwa akipeperusha bendera za vyama hivyo kupitia Ukawa, alipata kura 6,072,848 (asilimia 39.97), sawa na ongezeko la kura 3,078,852 kulinganisha na jumla ya kura za wagombea wote wa vyama vinavyounda Ukawa mwaka 2010.

AWAVUTIA SUMAYE, KINGUNGE, MAHANGA
Baada ya Lowassa kutangaza uamuzi mzito wa kuihama CCM aliyosisitiza kuwa ‘imemlea’ lakini analazimika kuondoka baada ya kubaini kuwa haiwezi kuleta mabadiliko yanayotakiwa na Watanzania walio wengi, makada wengine kadhaa vigogo wa CCM wakafuata nyayo zake kwa kuhamia pia Chadema.

Miongoni mwao ni mmoja wa waasisi wa CCM aliyewahi pia kuwa waziri na pia kushika nyadhifa kadhaa za chama, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru.

Wengine ni aliyekuwa Waziri Mkuu kwa vipindi vyote vya utawala wa serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa, Frederick Sumaye na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga.

Aidha, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye pia alimfuata Lowassa.

Vigogo wengine walioungana na Lowassa Chadema ni waliokuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa, Mgana Msindai (Singida) na Hamis Mgeja (Shinyanga), na pia waliokuwa wabunge kwa tiketi ya CCM, James Lembeli na Ester Bulaya.

‘MAFURIKO’ MIKUTANO UKAWA
Mara baada ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi Agosti 21, joto la uchaguzi la Uchaguzi Mkuu lilipanda maradufu. Ukawa walianza kampeni zao Agosti 29 na kwa namna ya kushangaza, jina la Lowassa lilitosha kujaza maelfu ya watu karibu katika kila mkutano aliohutubia.

Wakati fulani, hasa pale palipokuwa na jitihada za baadhi ya mamlaka kudhibiti mikutano yake kutokana na hofu ya usalama iliyotokana na wingi wa watu, mwenyewe aliibuka na kusema:”siwezi kuzuia mafuriko kwa mkono”.

Hali hiyo ya ‘mafuriko’ kwenye kila mkutano ilikuwa ni faraja tosha kwa Ukawa kwani mbali na Lowassa mwenyewe, wagombea wengine kwa nafasi za ubunge na udiwani walipata nafasi nzuri ya kunadi sera zao.

ONGEZEKO LA WABUNGE, MADIWANI
Kwa pamoja, katika Bunge la 10, idadi ya wabunge waliokuwa wakitoka vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF na NCCR ilikuwa ni chini ya 100.

Idadi hiyo imeongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya matokeo ya uchaguzi uliopita wakiwa na Lowassa ambapo sasa, kwa ujumla, Ukawa ina wabunge 116; mgawanyo wake ukiwa ni Chadema 71, CUF 44 na mmoja wa NCCR.

Ijapokuwa hakuna uthibitisho wa kiutafiti, lakini inadaiwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kuongezeka kwa idadi hiyo ya wabunge wa Ukawa ni hamasa iliyotokana na ujio wa Lowassa.

Kwamba, katika baadhi ya maeneo, jina lake lilisaidia kuvutia wapiga kura wapya, hasa vijana wasiokuwa na ajira rasmi kama machinga na madereva wa bodaboda ambao kwa muda mrefu amekuwa akiwaunga mkono.

ONGEZEKO LA HALMASHAURI CHINI YA UKAWA
Mbali na Lowassa kuchangia ongezeko la wabunge wa Ukawa, pia ‘mafuriko’ ya mikutano yake yanatajwa kuwezesha wagombea udiwani wengi zaidi wa kambi hiyo kushinda kwenye kata zao.

Matokeo yake, idadi ya halmashauri zinazoongozwa na Ukawa zimeongezeka kutoka tano (zilizokuwa chini ya Chadema) hadi kufikia 28 ambazo 23 ziko chini ya Chadema na 5 chini ya CUF ambayo awali haikuwa ikiongoza halmashauri yoyote Tanzania Bara.

Baadhi ya halmashauri zilizotua upinzani chini ya Ukawa kwa mara ya kwanza katika historia ni pamoja na Kinondoni na Ilala za jijini Dar es Salaam.

SIASA ZA UTULIVU
Inaelezwa kuwa miongoni mwa mambo chanya aliyoyafikisha Lowassa kwa Ukawa ni juu ya namna ya kuyaendea mambo panapokuwa na msuguano dhidi ya vyombo vya serikali.

Kwamba, badala ya kufanya maandamano katika kupigania kile wanachoamini kuwa ni haki yao, sasa Ukawa wamekuwa na utaratibu mwingine kabisa wa kutanguliza mazungumzo na mijadala na hilo limechangia kuwapo kwa utulivu hata pale wafuasi wao wanapokuja juu kwa nia ya kupinga kile wanachoamini kuwa ni dhulma ya wazi dhidi yao.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa mwenendo huo mpya wa siasa za utulivu katika kambi ya upinzani, ndiyo uliochangia kwa kiasi kikubwa kutokuwapo kwa matukio yanayohusisha polisi kutumia mabomu ya machozi na silaha za moto dhidi ya wafuasi wa Ukawa.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum wiki iliyopita, Lowassa alisema anawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwa watulivu licha ya kwamba wengi wao walitaka mabadiliko kupitia Ukawa, lakini wakatii rai yake ya kutaka wawe watulivu ili kudumisha amani ya nchi licha ya kutambua kuwa kura zao zimechakachuliwa.

“Baada ya matokeo, watu wengi, hasa vijana, walitarajia niwaambie waingie barabarani, sikufanya hivyo, bali nikawaambia tulieni… ni kwa sababu tu ya kutunza amani. Lugha hiyo kwa wanasiasa wengi wa nchi za Afrika siyo ya kawaida. Nawashukuru zaidi Watanzania kwa kunielewa japo hawakukubaliana na matokeo,” alisema Lowassa.

No comments:

Post a Comment