Saturday, January 23, 2016

Mahakama yafuta kesi ya Tundu Lissu

Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, jana ilifuta kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Mdai katika kesi hiyo, ambaye pia alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jonathan Njau, aliamua kuiondoa kesi hiyo kwa madai kuwa inampotezea muda wa kufanya shughuli zingine ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa gharama za kuendesha kesi, Sh. milioni 15.

Katika shauri hilo Njau alikuwa akilalamikia utaratibu uliotumika katika kuhesabu kura zilizompa ushindi Lissu, hivyo akataka kura hizo zirudiwe kuhesabiwa upya, jambo lililopingwa na mhusika.

Mbele ya Jaji Barker Sahel, Wakili wa Njau, Geofrey Wasonga, alisema mteja wake ameamua kuifuta kesi hiyo ili kumpa nafasi ya kufanya majukumu mengine pamoja na kumpa uhuru Lissu wa kutekeleza majukumu yake ya kibunge.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Lissu alisema alikuwa na uhakika wa kushinda kesi hiyo kwa kuwa ilikuwa na makosa mengi ya kisheria yanayolingana na ile ya kipindi kilichopita.

Lissu alisema kabla ya kufutwa kwa shauri hilo, mdai alishawasilisha mara mbili maombi ya kutaka kupunguziwa gaharama za kesi na imepita zaidi ya miezi miwili ameshindwa kulipa.

Alisema latika kesi hiyo aliweka mapingamizi sita na hata kama angelipa gharama hizo asingeweza kuyavuka kwa kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kwa ushabiki wa kisiasa.

Wakili aliyekuwa akisaidiana na Lissu, Fred Kalonga alisema walijiandaa kikamilifu katika kesi hiyo na kwamba wangeshinda mapema kuliko ilivyokuwa mwaka 2010, katika kesi iliyofunguliwa na wananchama watatu wa CCM.

No comments:

Post a Comment