Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ametangaza vita mpya na serikali ya kuanza safari ndefu ya kuelekea Ikulu mwaka 2020.
Moja ya kati vita yake hiyo na serikali ni kuanza kwa msukumo mkubwa wa kudai tume huru ya uchaguzi.
Lowassa alisema hayo wakati akizungumza na wafanyabishara wanaotaka mabadiliko wanaofanya shughuli zao Kariakoo, jijini Dar es Slamaa jana.
Alisema ili safari ya 2020 iwe na mafanikio, lazima chama chake kupitia kwa wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) washinikize kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
Alisema ana amini kwamba bila kupatikana tume huru hakuna haki itakayopatikana wakati wa uchaguzi, kusimamia matokeo na kumtangaza mshindi.
Harakati za kudai tume huru ya uchagzi ziliwahi kufanywa na wadau mbalimbali vikiwamo vyama vya upinzani, lakini kilio chao hakijawahi kusikilizwa.
Miongoni mwa wadau waliojitolea kudai tume huru ya uchaguzi ni marehemu, Christopher Mtikila, ambaye tangu kuanzishwa vyama vingi hapa nchini aliipigania mpaka anafariki dunia mwaka jana.
Wengine waliopigania na kudai kwa nguvu kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi ni viongozi wa Chama cha Wananchi Cuf, upande wa Zanzibar kabla ya mwaka 2010.
Hata hivyo, nguvu za CUF zilipungua nguvu baada ya mwaka 2009 baada ya kubadilishwa Katiba ya Zanzibar iliyoruhusu serikali ya umoja wa kitafa.
Lakini pia Katiba Mpya iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, iliweka kipengele cha kuuundwa tume huru ya uchaguzi pamoja na kuruhusu mgombea binafsi.
Hata hivyo, Bunge la Katiba ambalo wajumbe wake wengi walitoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliondoa vipengele hivyo, hatua ambayo imeendelea kufanya jambo hilo kuwa gumu japo limekuwa likilalamikiwa na wadau wengi.
Aidha, katika kikao hicho na wafanyabiashara, Lowassa aliendelea kudai kuwa alishinda nafasi ya urais lakini aliamua kukubali yaishe ili kuepusha machafuko na kwamba hakuwa tayari kuingia Ikulu mikono yake ikinuka damu.
Alidai baada ya kushinda na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukataa kumtangaza, angesema watu waingie barabarani wangechinjana jambo ambalo hakutaka kuona linatokea hapa nchini.
"Sijakata tamaa kwa sababu naamini nilishinda katika uchaguzi uliopita, Watanzania wanajua na dunia inajua, lakini niliamua yaishe ili kulinda amani tuliyonayo," alidai na kuongeza:
"Nipo salama, nipo fiti na morali yangu katika kuelekea Ikulu ipo juu sana zaidi ya mwaka jana."
Alisema ili kufikia malengo yake ya kisiasa yeye na chama chake wanajipanga kwa nguvu nyingi ili kushiriki uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Alitoa mfano kuwa kuna Rais mmoja wa Marekani aliwahi kugombea mara tano na hakukata tamaa na hatimaye alifanikiwa kuingia Ikulu.
Lowassa ambaye alitoa upinzani mkali kwa Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, alisema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi huo, lakini anachoshukuru nchi ni salama na wananchi wanaishi kwa amani.
Aliwataka wanamadiliko na wananchi wote waliompigia kura mwaka jana wasikate tamaa kwa kuwa uchaguzi mkuu ujao hataibiwa tena kura.
UBAGUZI
Kuhusu sakata la wanachama wa CCM kupita na mabango yenye lugha za ubaguzi katika sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, Lowassa alikitaka chama hicho kukemea suala hilo.
''Lazima ajitokeze mtu mzito na mwenye heshima ambaye anaweza kulielezea vizuri hili na watu wakalielewa kwamba siyo msimamo wa chama badala ya kumuachia mtu mwenye mipasho kulisemea,'' alisema.
Alisema kuna kiongozi ndani ya CCM ambaye alimuita mtu wa mipasho (hakumtaja jina), kwamba hana uwezo wala nguvu za kulisemea jambo hilo kama alivyofanya.
Katika sherehe hizo, kulikuwa na bango lililoandikwa 'Machotara wa Hizbu Zanzibar ni nchi ya Waafrika' na bango hilo kupitishwa mbele ya viongozi wa serikali katika sherehe hizo.
MKWAMO WA KISIASA Z’BAR
Kuhusu mkwamo wa kisiasa Zanzibar, Lowassa aliitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kumtangaza mshindi ambaye alidai ni Maalim Seif Shariff Hammad.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa wanamabadiliko wafanyabishara hao wa Kariakoo, Sevelin Mushi, alisema wako nyuma ya Lowassa licha ya kuwapo vitisho mbalimbali.
Alisema wao kama wafanyabishara wapenda mabadiliko walifika ofisini kwa Lowassa kumpongeza kwa kura nyingi alizopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Alimuita Lowassa kuwa ni Rais wa mioyo ya Watanzania na kwamba walikuwa naye katika safari ndefu ya kutafuta mabadiliko ya kweli.
No comments:
Post a Comment