Friday, December 25, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KAULI YA WAZIRI MKUU MIKUTANO YA HADHARA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU
KAULI YA WAZIRI MKUU MIKUTANO YA HADHARATumeona kupitia vyombo vya habari na njia mbalimbali za upashanaji taarifa kwamba Waziri Mkuu Majaliwa Kassim amenukuliwa akitoa kauli inayoonesha Serikali ya CCM inataka kuzuia shughuli za kisiasa hususan mikutano ya hadhara.

Kupitia kauli hiyo, Waziri Mkuu amenukuliwa zaidi akisema kuwa Uchaguzi umekwisha hivyo sasa si wakati wa siasa bali maendeleo.

Hii ni kauli ya ajabu kutolewa na mtu anayesimamia utendaji wa shughuli za kila siku za serikali inayotaka kuwaaminisha kuwa itakuwa tofauti na serikali zingine zilizopita za CCM.

Kupitia taarifa hii, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tunailaani na kuipinga kwa nguvu zote kauli hiyo yenye chembe za udikteta iliyotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Inaonekana imetolewa na mtu ambae ameanza kulewa madaraka mapema sana huku akisukumwa na utashi wa kisiasa wa kuiokoa CCM kwenye kasi ya kufa kisiasa na kulinda udhaifu wa serikali yao ambao umeshaanza kuonekana wazi kupitia kila hatua wanayochukua na matamko wanayotoa.

Kama wao (CCM) ndiyo walioshinda kama ambavyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema na kwamba wanaendelea kutekeleza wajibu waliokabidhiwa na wananchi, tunahoji hofu yao nini hasa wakiona au wakisikia CHADEMA wanapanga kwenda kuongea na wananchi? Wanaogopa nini?

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa imekuja siku chache tu baada ya kiongozi huyo mwandamizi wa serikali ambaye anatazamiwa kuwa mtumishi wa Watanzania wote bila kuwabagua kwa itikadi za kisiasa, kabila wala dini, kuwa ametoa upendeleo kwa chama kimoja cha siasa ambacho ni CCM kuhutubia na kufanya siasa kwenye mkutano wake mjini Lindi, ambapo Nape Nnauye alitumia jukwaa hilo la kiserikali kuzungumza kama kiongozi wa CCM akiwajibu viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA.

Matukio haya yanaanza kumdhihirisha Waziri Mkuu Majaliwa ni kiongozi mwenye uelekeo wa namna gani hivyo kuanza kuifunua Serikali ya Rais John Magufuli chini ya CCM kwa miaka mitano ijayo itawapeleka wapi Watanzania.

Ni dalili za wazi za watu waliolewa madaraka na
kuchoka kuwa viongozi na sasa wanataka kuwa watawala wenye kudhani kuwa fikra zao ndizo zinazongoza nchi badala ya misingi ya inayokubalika miongoni mwa jamii nzima kupitia Katiba, Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali.

Tunatumia fursa hii kusisitiza kauli yetu kwamba walioko madarakani wanapaswa kutambua kuwa siasa haina msimu wala haianzi na kuishia wakati wa uchaguzi kwa sababu siasa ni mfumo wa maisha ya binadamu kila siku. Si suala la kupenda au kutokupenda.

Uchaguzi pia ni mchakato. Mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine kwa haraka kwa wadau wote, vikiwemo vyama vya siasa na vyombo vingine au taasisi zingine zote zinazohusika. Kuendelezwa kwa fikra za namna hiyo za Waziri Mkuu ndiyo kunasababisha Serikali na taasisi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuvunja sheria za nchi kwa kushindwa kuandikisha wapiga kura kama inavyotakiwa baada ya uchaguzi kumalizika.

Aidha kuheshimu misingi ya demokrasia, ikiwemo ushindani wa (hoja, sera, mikakati, mipango) wa vyama vingi, si suala la utashi wa walioko madarakani bali ni haki ya msingi ya kibinadamu na kikatiba na matakwa ya wanananchi wanaotoa dhamana ya watu kukaa madarakani kuongoza kwa niaba ya wengine.

Je Waziri Mkuu anataka kuwaambia Watanzania kuwa anatofautisha siasa na maendeleo? Je anataka kusema kuwa haki ya vyama vya siasa kukutana na kuzungumza na wananchi itabakia kwa CCM tu kwa miaka mitano ijayo? Anajua hilo halitakubalika.

Ni vyema Waziri Mkuu akatambua kuwa nchi hii haiko kwenye fikra wala mfumo wa chama kimoja tena.

Imetolewa leo Alhamis, Desemba 24, 2015 na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA

No comments:

Post a Comment