Saturday, November 21, 2015

WABUNGE WA UKAWA WATOKA NJE YA UKUMBI WA BUNGE


Wabunge wanaounda "Umoja wa Katiba Ya Wananchi", UKAWA wametolewa nje ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Ijumaa, Novemba 20, 2015 baada ya kusisitiza kutokutambua ujio wa Dk Shein bungeni na kuanza kuzomea huku wakisema kwa kurudia, "Maalim Seif. Maalim Seif. ..."

Wabunge hao awali walitoa msimamo wao wa kutokubali Dk Ali Shein kuhudhuria Bunge hilo wakati rais John Magufuli atakapoingia bungeni kulihutubia kwa kuwa hawamtambui kama rais wa Zanzibar wakishikilia kuwa, kwa mujibu wa Katiba, muda wake wa uongozi umekwisha.

Kelele za kuzomea zomea ziliibuka ghafla wakati Rais Dk Shein alipoingia bungeni hali iliyoondoa utulivu Bungeni.

Hata hivyo, Mbunge pekee wa upinzani, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) alibaki ndani ya Bunge kwa na kuendelea kusikiliza hotuba ya Rais Magufuli, ambaye naye alimsifu kwa msimamo wake.

Awali, wabunge hao walimuandikia barua Spika wa Bunge wakihoji uhalali wa hotuba ya Rais bungeni endapo Dk Shein atahudhuria Bunge hilo kama Rais wa Zanzibar.

UKAWA wameendelea kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (NEC) kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, huku mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi akidai kuwa ameshinda kutokana na kura halali alizokusanya kwenye vituo vyote.

Spika wa bunge, Job Ndugai aliwataka wabunge hao waache kuzomea na badala yake wakae chini lakini baada ya agizo lake kutokuitikiwa alivyotaka, alitoa amri ya kuwaamuru watoke nje kwa hiari yao kabla nguvu ya dola haijatumika kuwatoa.


wavuti

No comments:

Post a Comment