Saturday, November 21, 2015

TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA TANZANIA (AZAKI) KUHUSU HALI YA KISIASA VISIWANI ZANZIBAR 20/11/2015

TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA TANZANIA (AZAKI) KUHUSU HALI YA KISIASA VISIWANI ZANZIBAR 20/11/2015

Sisi Wanaasasi za Kiraia nchini - AZAKI, tumekutana tarehe 17 Novemba 2015, ambapo ni zaidi ya wiki tatu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika na kutathimini mwenendo wa uchaguzi mkuu na hali ya kisisasa vizisiwani Zanzibar. Awali ya yote tunapenda kuwapongeza watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani katika uchaguzi huo. Hata hivyo tathmini yetu imeonyesha kuna mambo mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi mara baada ya uchaguzi kwisha tarehe 25/10/2015 ili kurudisha imani kwa Watanzania ambao wanaonekana kukata tamaa na zoezi la upigaji kura mara baada ya uchaguzi huu.

Asasi za Tanzania tumeendelea kufuatilia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 katika hatua zote toka uandikishaji wa wapiga kura, kampeni, upigaji wa kura, ujumlishaji na hatimaye utangazaji wa matokeo kwa umakini mkubwa. AZAKI tumefanya hivyo tukiamini kuwa uchaguzi ni sehemu muhimu ya michakato ya kidemokrasia hapa nchini kama ilivyo duniani kote. Sisi asasi za kiraia Tanzania, tukiwa watetezi na wasimamizi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu, hatuegemei upande wa mgombea yeyote wala chama chochote cha siasa kinachotafuta kuingia madarakani wala hatulengi kuchukua dola.

Uchanguzi huu umeonekana kuwa na kasoro nyingi zinazohitaji ufumbuzi wa haraka kabla ya kuelekea kwenye chaguzi zinazofuata. Katika makubaliano ya mkutano wa AZAKI tumekubaliana kuitisha mkutano mwingine mkubwa wa AZAKI mapema mwakani ili kuweka wazi mapungufu yote yalijitokeza kwenye uchaguzi huu ili kuitaka Serikali kuyafanyia kazi kabla ya chaguzi zinazofuata.

Kwa ujumla , wanaasasi tumebaini kuwa kuna kila sababu ya kususia kwenda kwenye chaguzi zijazo endapo changamoto ambazo zitawekwa wazi kwenye mkutano ujao hazitafanyiwa kazi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kukosekana kwa Katiba bora, kuwa na sheria za uchaguzi ambazo haziakisi mfumo wa vyama vingi na kukosekana kwa Tume huru za uchaguzi pande zote mbili za Muungano Tanzania.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar, AZAKI tunatambua hali isiyoridhisha ya kisiasa ambayo imetokana na kukwamishwa kwa sababu zisizokuwa na tija kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar, uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. Tunaona kumeibuka mgogoro mkubwa wa kisiasa kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Bw. JECHA SALIM JECHA wa kufuta uchaguzi mkuu wote wa Zanzibar, kwa maana ya uchaguzi wa kumchagua Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar.

Uamuzi huo wa kufuta uchaguzi siyo sahihi kisheria na haukubaliki kwa sababu umevunja katiba na kwamba umefanywa kwa msukomo wa maslahi binafsi ya kisiasa kwa kuwa si Mwenyekiti wala Tume ya Uchaguzi yenye mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi. Kwa ufupi, hakuna kifungu chochote cha sheria wala Katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 kinachompa uwezo Mwenyekiti au Tume kuchukua uamuzi kama huo.

Uamuzi huo umezusha mtafaruku mkubwa huko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, umeibua malumbano na mivutano katika jamii na hiyo kwenda mbali zaidi kwa kuibua upya mvutano wa kisiasa kati ya vyama vikuu viwili vya siasa vya CCM (Chama Cha Mapinduzi) na CUF (Chama cha Wananchi).

Hali hii ya malumbano na mivutano imesababisha matatizo zaidi hasa kutokana na kuongezeka kwa ukali wa maisha na ukimya katika hali ambayo wananchi hawajui ni nini hasa kinachoendelea kuhusu hatima ya nchi yao. Hata hivyo, wanachi wanajua kumekuwa na vikao vya majadiliano vya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa uliopo, lakini taarifa za maendeleo ya mazungumzo imekuwa siri kubwa.

Wakati hali hiyo ikiendelea Zanzibar, Tanzania Bara taratibu zote za kuunda serikali ya Muungano, baada ya uchaguzi Mkuu zinaendelea zikiwemo za Rais wa Jamhuri ya Muungano kuliitisha Bunge, kuchaguliwa kwa Spika na makamu wake napia kupitishwa kwa jina la Waziri Mkuu. Kikubwa zaidi Wabunge waliochaguliwa kutoka Zanzibar nao waliapishwa na ambao kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa ZEC uchaguzi wao ulifutwa.

Tunachukua nafasi hii kuwapa moyo viongozi wa ngazi ya juu nchini wanaokutana na kuendeleza majadiliano kwa matumaini kwamba wanatafuta njia za kuiondolea nchi hatari ya kuchafuka kisiasa, hatua itakayohatarisha Usalama, Amani na Utengamano katika nchi.

Huku tukitambua kwamba kukutana na kujadiliana kwa viongozi wa ngazi ya juu, wakiwemo marais wastaafu wa Zanzibar, ni njia muafaka ya kutafuta suluhu ya mgogoro, tunataka ieleweke wazi kuwa vikao visivyokuwa na mwisho wala taarifa inayotolewa kwa umma kuhusu maendeleo yake, havileti matumaini kwa wananchi. Ni haki ya msingi na ya kikatiba kwa wananchi kupewa taarifa ya maendeleo ya vikao hivyo; waelezwe vinalenga nini; na kwa muda gani viongozi wanaweza kumaliza majadiliano. Wananchi wanayo haki ya kujua yote hayo kwa vile ndio dhana ya utawala bora inavyotaka.

Hofu kubwa tuliyonayo sisi Wanaasasi za Kiraia ni kwamba kuendelea kwa ukimya mkubwa kunaongeza minong'ono katika jamii, hali inayoweza kuzusha migongano na kusababisha haki na amani kuchezewa na wasiokuwa na nia njema ya kuiona Zanzibar inaishi katika amani na kuendeleza utengamano kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa - Government of National Unity (GNU). Kwa sasa kuna hali ya utata kuhusu uongozi uliopo madarakani Zanzibar kutokana na Sababu Mbalimbali;

A. Muda wa Kushika Madaraka ya Urais Kikatiba

Ibara ya 28(2) ya Katiba ya Zanzibar inaeleza wazi kuwa "Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula Kiapo cha Uaminifu na Kiapo cha kuwa Rais. Tafsiri ya maneno hayo ni kuwa tangu Rais wa Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais siku ya tarehe 3 Novemba 2010, atakuwa ametimiza miaka mitano siku ya tarehe 2 Novemba 2015. Kwa hivyo basi, Rais kuendelea kushika madaraka ya urais zaidi ya tarehe hiyo ni kinyume na Katiba ya Zanzibar ya 1984. Upo mjadala katika jamii kuwa Rais anao uhalali wa kuendelea kushika madaraka ya urais kupitia mamlaka ya Ibara ya 28(1)(a), lakini maoni ya wanasheria walioko chini ya Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) na Wale wa Tanganyika Law Society (TLS) ambayo tunayaunga mkono ni kwamba maudhui ya Ibara hiyo ni kumpa uwezo wa kikatiba Rais kuendelea kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo cha uaminifu kwa Rais mpya (anayefuata) tu na sio kuendelea kukaa madarakani pasina kufanyika kwa uchaguzi au kwa sababu ya kufutwa uchaguzi.

B. Nchi kuendeshwa Bila kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi (BLW):

Katika mazingira ya uongozi wa Zanzibar yaliyopo kwa sasa, ni wazi kuwa nchi inaendeshwa kwa muda mrefu bila ya kuwepo chombo cha kutunga sheria ambacho ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa Serikali. Katiba ya Zanzibar imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW kwa muda usiozidi Siku Tisini (90) kuanzia Baraza lilipovunjwa. Kipindi hicho kikatiba kilikwisha toka tarehe 12 Novemba 2015, kwa kuwa Baraza lilivunjwa rasmi tarehe 13 Agosti 2015.

Wito Wetu

Kutokana na yote hayo tuliyoyaeleza hapo juu, sasa tunapendekeza hatua zifuatazo zizingatiwe ili kuendeleza amani na utengamano nchini:

1. Uwepo utaratibu wa kutolewa taarifa ya maendeleo ya majadiliano yanayofanywa na viongozi wanaokutana kuhusu suala la Zanzibar, ikieleza lengo la majadiliano na muda wake; ikumbukwe kikatiba, wananchi wana haki ya kujua na kushirikishwa katika masuala yoyote yanayohusu maslahi yao na nchi yao.

2. Wakati majadiliano yakiendelea, (i) Vyombo vya Ulinzi na Usalama viendelee kulinda wananchi kwa mujibu wa Sheria za Nchi na kusiwe na utaratibu wa kuwanyanyasa wananchi kama inavyolalamikiwa na baadhi ya watu kuhusu manyanyaso yanayofanywa na wanausalama maeneo ya Bandarini mjini Zanzibar.

3. Vyombo vya Habari hasa vya Serikali visitumike vibaya, mfano hai ukiwa unaoendelea kwa muda sasa wa matangazo ya hutuba za viongozi zinazoeneza siasa za chuki na propaganda zisizofaa. Matumizi mabaya ya vyombo hivi vya habari yadhibitiwe. Sambamba na hili tutahitaji kuona sheria na sera zote zinazosimamia vyombo vya umma zinabadilishwa ili kuleta mfumo usio na upendeleo kabla ya kuelekea kwenye chaguzi zijazo.

4. Tunakumbusha Viongozi wanaojadiliana na watu wengine wote wenye mchango katika kuiona Zanzibar inaishi kwa amani na salama, wajikite sana katika mazingatio ya Sheria na Katiba wanapokusudia kufanya maamuzi ya utatuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar, kwa sababu kinyume na hivyo, watazusha machafuko kwa kufikia maamuzi yasiyofuata au yanayokinzana na sheria na katiba. Kila mtu na kwa kila hatua, kutii misingi ya Sheria na Katiba ni muhimu na kutaepusha migongano na machafuko.

5. Tunapenda kuwakumbushia Wanaasasi wenzetu kuwa uchaguzi sio tendo la mara moja au siku moja. Watambue kuwa uchaguzi ni mchakato na sasa tupo kwenye uchaguzi bado ila katika ngwe ya baada ya kupiga kura ( Post Election Periodn). Tuendelee kufuatilia maswala yote yanayohusu uchaguzi ili kuendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwa na chaguzi bora na zenye kuzingatia haki na usawa siku za usoni.

6. Pia tunawakumbusha watanzania kuwa, kama AZAKI tumeona sababu nyingi za kisheria kwenda mahakamani kupinga yaliyotokea Zanzibar, lakini kwa sababu mahususi tumeridhia kutokwenda kwenye mahakama yoyote. Moja ya sababu kubwa iliyotushawishi kutokwenda mahakamani kwa kesi za kisiasa, kwa maoni yetu, ni kukosekana kwa uhuru wa kutosha wa vyombo vya kutoa haki kama mahakama. Tunahistoria ya mashauri kadhaa kama ya mgombea binafsi na ile ya Mita 200 kuamuliwa sio kwa mujibu wa sheria bali kwa matakwa ya kisiasa zaidi na baadaye baadhi ya wahusika kuonekana katika majukwaa ya kisiasa kama wanachama wa muda mrefu wa vyama vya siasa.

Mwisho

Sisi ni Asasi za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zilizoundwa na kutambulika kisheria na zinazofanya kazi katika masuala mbalimbali ya kisheria, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kwa umoja wetu tunasimamia na kuhimiza utawala wa sheria na haki za binadamu na masuala yote ya kimaendeleo ili kuhakikisha maisha ya watanzania yanakuwa bora katika nyanja zote. Kwa sababu hiyo, tunajiona tukiwa na jukumu kubwa la kukemea na kuvitaka vyombo husika kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka uvunjifu wa amani na hivyo kulinusuru Taifa letu.

Imetolewa kwa niaba ya AZAKI zote nchini na asasi miavuli zilizofanya Mkutano Jijijini Dar es Salaam Tarehe 17/11/2015 :

Kwa niaba ya Asasi zote, inaletwa kwenu na:

Ismail Suleiman

Katibu Mkuu- Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia

Onesmo Ole Ngurumwa

Mratibu wa Kitaifa- Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania

Deus M Kibamba

Mwenyekiti Taifa -JUKWAA LA KATIBA TANZANIA

Martina Kabisama-Mratibu Taifa

Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini Mwa Afrika(SAHRINGON)

Stepheni Msechu

Mwakilishi- Chama cha Wanasheria Tanganyika

Omary Said- Katibu

Chama cha Wanasheria Zanzibar

Salma Said

Mwenyekiti WAHAMAZA

Alan Lawa

Mwakilishi Baraza la Habari Tanzania

No comments:

Post a Comment