Sunday, November 22, 2015

Ukawa kuchanga Mil 33.9 kusaidia familia ya Mawazo

WABUNGE wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamepanga kuchanga Sh. 33.9 milioni kwa ajili ya kusaidia familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoani wa Geita, Alfonce Mawazo. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Fedha, hizo zimepatika baada ya wabunge 113 wa Ukawa kuchangishana kiasi Sh. 300,000 kila mmoja ambazo zitakabidhiwa familia ya Mawazo ambaye ameuawa kikatili na watu ambao mpaka sasa hawajabainishwa.

Mwenyekiti wa Chadema – Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema hayo wakati akizungumza na mwanahalisionline mjini hapa Dodoma kuhusu maandalizi ya mazishi ya kada huyo ambaye anatajwa kuwa shujaa katika mapambado ya kutafuta ukombozi Ukawa.

Mbowe amesema licha ya kwamba Mawazo alikuwa mwanachama wa Chadema lakini pia alishiriki vyema katika ukombozi ndani ya Ukawa kwa kutetea masilahi ya Watanzania kwenye mkoa wake wa Geita pamoja na mikoa mingine nchini.

“Kwa ujumla wetu wabunge takribani 113 tumekubaliana kuchanga kiasi cha Sh. 300,000 kila mmoja kwa ajili ya kuiwezesha familia yake ambayo ameiacha.

“Kumbuka kwamba Mawazo amepigania masilahi ya Watanzania wengi katika mkoa wake wa Geita lakini pia katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Hivyo tunalazimika kumuenzi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wetu wa Ukawa na ikumbukwe kuwa, kwa sasa seriali ya CCM inaonesha wazi kutumia vyombo vyake vya dola kudidimiza upinzani,” amesema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe amesema inasikitisha kuona jeshi la polisi linavyotumiwa vibaya na kujikuta linafanya kazi za siasa badala ya kusimamia ulinzi na usalama wa raia.

“Leo (juzi), baada ya viongozi wa Mji wa Mwanza kupambana vikali na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, aliwaambia viongozi wa Chadema kuwa intelejensia imeonesha kuwa, iwapo watafanya mkusanyiko wa ibada kuna uwezekano wa kuzuka machafuko.

“Baada ya kupata taarifa hizo nilipata kuzungunza na IGP na kuniahaidi kunipatia majibu lakini hadi sasa sijafanikiwa kupata majibu lakini jambo lingine na la ajabu ni pale ambapo wamegeuza kibao na kusema hakuna kufanya ibada kwani kwa sasa kuna ugonjwa wa kipindupindu hivyo hakuna mkusanyiko,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema lazima Watanzania watambue kuwa serikali inatumia vibaya vyombo vyake vya dola kuzuia wapinzania wasifikishe ujumbe wao kwa jamii, imekifia hatua ya kuzuia hata watu kuwazika wafuasi wao.

“Sasa angalia kutuuwa wanatuuwa lakini hatua ya kutunyanyasa na kukataa hata tusimzike mtu wetu jambo hilo ni la ajabu sana lakini najua tutafikisha ujumbe kwa njia nyingine ambayo inafaa na kwa ustaarabu,” amesema Mbowe.

Mwanahalisi Online

No comments:

Post a Comment