Sunday, October 25, 2015

Taarifa Rasmi Kutoka UKAWA Kuhusu Uchaguzi Mkuu Unaoendelea Leo- 25/10/2015


1. Hali ya vitisho vya jeshi la polisi na kamata kamata iliyoanza jana usiku hadi leo asubuhi. Wawaache wananchi watumie haki yao ya kikatiba kumchagua kiongozi wanayemtaka.

2. Suala la watu wenye kadi lakini majina yao hayapo, ambapo kisheria inatakiwa msimamizi awape fomu namba 19 kisha waijaze na kupiga kura. Tumewataka wananchi kutokuondoka vituoni hadi wapate haki hiyo ya kujaza fomu hizo na kupiga kura.

Vifaa vya kupigia kura kuchelewa kufika vituoni ambapo baadhi ya vituo kama Kimara Temboni Dar es salaam, msimamizi amefungua kituo saa mbili kisha akasema karatasi za mgombea urais zimekwisha. Tumewataka wananchi katika maeneo kama hayo kutokuondoka vituoni, wakae kwa utulivu wahakikishe wanapiga kura.

Tumewataka NEC ambao wanapigiwa simu lakini hawapokei kutoa msaada wa haraka, wahakikishe suala hilo linatatuliwa haraka. Uchaguzi huu haukuwa ajali au suala la kushtukiza.

3. Idadi ya wapiga kura kwenye kituo kimoja kuwa kubwa tofauti na matakwa ya kisheria, kuna vituo tumebaini vinawapiga kura zaidi ya 800. Hairuhusiwi. Wapiga kura hawapaswi kuzidi 450 kwa kila kituo.

4. Madai ya kuwepo kwa kura feki kukamatwa katika maeneo mbalimbali zikiwa tayari zimepigwa, mfano tunazo taarifa za kukamatwa huko, Vunjo, Njombe na maeneo mengine ya nchi.

Hili tulitarajia tume ilizungumzie kwa udharura lakini mpaka sasa tunawatafuta watu wa tume hawapatikani.
Tunawahimiza watu wawe watulivu wasiondoke vituoni mpaka wapige kura ambayo ni haki yao kikatiba.

Tumaini Makene
Mkuu wa idara ya mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment