Saturday, October 3, 2015

MGOMBEA UBUNGE WA MBINGA MAGHARIBI KUPITIA CHADEMA APATA AJALI MBAYA YA GARI

Pichani Gari alilopatia ajali mgombea ubunge wa jimbo la mbinga Magharibi Ndugu Cuthbert Ngwata

Mgombea Ubunge Kupitia Chadema Jimbo la Mbinga Magharibi ndugu Cuthbert Ngwata amepata ajali mbaya ya gari usiku alipokuwa akielekea kwenye kampeni ya Ubunge. Kulingana na Mtoa taarifa Mgombea Ubunge huyo wa Chadema alipata ajali baada ya gari yao waliyokuwa wanasafiria kuvamiwa na watu waliokuwa wanataka kuwateka ndipo dereva wa gari hilo katika harakati za kuwakimbia ndipo gari likayumba na kuingia Korongoni na kusababisha ajali hiyo mbaya. Kulingana na mtoa taarifa ndani ya gari hiyo kulikuwa na mtu mwingine anayejulikana kama kamanda Pompi anayetokea Mbozi Mkoani Mbeya ambaye amefariki dunia katika ajali hiyo.

Awali mgombea ubunge huyo ndugu Cuthbert Ngwata pamoja na dereva wake walikimbiziwa katika hospitali ya Nyasa kwa matibabu lakini kutokana na hali zao kuwa mbaya sana wamehamishiwa kwenye hospitali ya Litembo kwa matibabu zaidi.

Hili ni tukio la pili kuwapata wagombea Ubunge wa Chadema katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja. Ikumbukwe tukio kama hili liligharimu maisha ya mgombea Ubunge wa Lushoto ndugu Mohamed Mtoi wiki chache zilizopita. Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi zinazoelezea mazingira ya kifo kilichompata Ndugu Mohamed Mtoi.

Kutokana na mfululizo wa matukio haya tunaliomba jeshi la Polisi lifanye Uchunguzi kujua namna gani kumekuwa na matukio kama haya yanayowapata wagombea Ubunge katika kipindi hiki cha kampeni. Pia wagombea Ubunge wote wachukue Tahadhari za kiusalama wanapokuwa katika harakati za kampeni kwa kuepuka kutembea safari za Usiku wanapokuwa katika kampeni, na pia kuwa na Ulinzi wa kutosha ili kuepuka matukio kama haya kuwakumba.
Pichani Gari la aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Marehemu Mohamed Mtoi 


No comments:

Post a Comment