Sunday, October 4, 2015

GOLI LA MKONO - MYIKA ARUSHA KOMBORA JENGINE NEC


NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujibu hoja zinazoibuliwa kuhusiana na Uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Octoba 25 na sio kupotosha kwa makusudi huku ikiacha hoja za msingi zinazotolewa zikielea.
John Mnyika ambaye pia ni Mgombea Ubunge wa Chadema katika jimbo la Kibamba, amezungumza hii leo jijini Dar makao makuu ya UKAWA eneo la Ngome, na kusema Tume ya Uchaguzi mpaka sasa inastahili kutiliwa shaka kwa kuwa inaweza kusababisha utata mkubwa kwa kuendelea kuchelewesha daftari la wapiga kura kwa vyama vya siasa.
“Hatuwezi kuiacha Tume iendelee kufanya ucheleweshaji wa kutoa orodha ya wapiga kura nchi nzima kwa vyama ili wataalamu wetu wa teknolojia ya kompyuta wayahakiki, siku zimeshabaki chache na tukumbuke mwaka jana muda kama huu vyama tulikuwa tumeshapewa ‘soft copy’ ya daftari na kulifanyia uhakiki,” amesema Mnyika.
Mnyika ameitaka NEC kutoa orodha ya wapiga kura wote mpaka kufikia siku ya Jumatatu wiki ijayo (kesho kutwa) ili kuondoa sintofahamu inayoweza kujitokeza kutokana na daftari hilo kucheleweshwa kwa Vyama kwa Vyama vinahitaji kuwapatia nakala ya daftari hilo mawakala wao nchi nzima.
Katika hatua nyingine Mnyika ameiasa NEC kuacha upotoshaji, kwa kusema busara ya wasimamizi wa Uchaguzi inaweza kutumika kuwaruhusu watu wenye vitambulisho vya kupiga kura watapiga kura hata kama wasipokuwepo katika orodha ya wapiga kura, huo ni upotoshaji mkubwa.
“Tumesikia NEC ikifanya upotoshaji ambao unakiuka sheria za uchaguzi kuwa wenye vitambulisho ambao majina yao yatakosekana kwenye daftari busara inaweza kutumika wakapiga kura. Huu ni upotoshaji na sheria inakataa kabisa, busara inaweza kutumika kwa wale wenye utata wa vitambulisho lakini wapo kwenye daftari na si vinginevyo,” amefafanua Mnyika.
Pia Mnyika amewataka watanzania watakaohudhuria tamasha la kuiombea amani ya Tanzania siku ya kesho wamuombee zaidi Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kwani wao ndio watu muhimu wanaotakiwa kutenda haki na kufanya amani iendelee kuwepo hata baada ya matokeo ya uchaguzi.
Mwanahalisi Online ilijaribu kumtafuta Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima kwa njia ya simu ili kutolewa majibu baadhi ya hoja za Mnyika hata hivyo hakupokea licha ya kupigiwa zaidi ya mara tatu na kutumiwa ujumbe mfupi wa simu lakini hakuwa tayari kujibu pia.
Hapo awali Tume iliahidi kubandika orodha ya wapiga kura katika vituo walivyojiandikishia siku nane kabla ya uchaguzi ili kuwawezesha wananchi kuweza kuangalia majina yao na kutoa malalamiko iwapo kuna dosari zozote zilizoonekana.


No comments:

Post a Comment