Friday, August 14, 2015

MWENYEKITI WA CCM SHINYANGA AHAMIA CHADEMA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ametangaza rasmi kuachana na chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Pamoja naye katika kutangaza hayo ni kada maarufu wa chama hicho, John Guninita.

Mgeja ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, leo ametangaza rasmi kujiunga na CHADEMA mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo ametumia kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa mwaka 1995 alipozungumzia haja ya chama hicho kujisahihisha kwamba, Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.

Makada hao wamesema kuwa wamechoka kuona chama kinatumia ubabe na mabavu kuwasimika watu wasio na uwezo wa kuiongoza nchi na kuacha viongozi wenye uwezo jambo ambalo wamesema hawawezi kulivumilia milele.

Mgeja amesema kuwa hali iliyotokea Dodoma katika mkutano wa kufanya uteuzi hali ya Mwenyekiti kuingia na majina yake matano mfukoni na kukataa ushauri wa viongozi na wanachama ni jambo ambalo lilionyesha udhaifu mkubwa ndani ya chama hicho hasa pale walipoamua kutumia silaha na vyombo vya usalama kuwatawanya wanachama waliokuwa wanaihitaji haki itendeke.


Mgeja ni mmoja wa wanachama waliokuwa mstari wa mbele katika kumuunga mkono Edward Lowassa katika mbio za kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa Tanzanai 2015.

Akizungumzia mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, John Mgeja amesema kiongozi huyo ni sawa na "learner" anayejifunza kuongoza nchi kwani hajawahi hata kuwa balozi wa nyumba kumi kupitia chama hicho, hivyo watanzania hawako tayari kuwajaribu watu katika nafasi kubwa kama ya Urais.

Mgeja amesema kuwa kama viongozi wa CCM wanahitaji kukijenga chama lazima watengue maamuzi hayo na kuwaomba radhi wanachama wa chama hicho na kisha kuchagua mtu ambaye anaweza kukivusha chama hicho tofauti na hapo chama hicho kinakwenda kufa.

Mgeja amesema kuwa kama wana CCM watahitaji mambo mengine waite mdahalo na viongozi hao wakaseme yale yote yaliyotokea Dodoma.

No comments:

Post a Comment