Thursday, August 27, 2015

Chadema yawakatia rufaa waliopita 'kiulaini'.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekata rufani katika majimbo matatu ya Bumbuli, Mlalo na Ludewa baada ya pingamizi zake kutupiliwa mbali.

Pingamizi hizo zilitupiliwa mbali na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo hayo na hivyo kuwatangaza wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepita bila kupingwa. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala, alisema tayari wamewasilisha rufani na wanasubiri uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na wanaamini haki itatendeka.

Alisema Jimbo la Ludewa, Msimamizi wa Uchaguzi, alidai kwamba katika fomu ya mgombea wa Chadema haikuwa na fomu namba 10, huku mgombea akisema aliwasilisha kila kitu kinachohitajika ikiwamo fomu hiyo.

Kibatala alisema baada ya kufuatilia, ofisi ya msimamizi ilibaini kwamba wao ndiyo walifanya uzembe katika kuihifadhi. Alisema sababu za kutupiliwa mbali pingamizi katika majimbo mengine, hazikuwa na msingi hususan Majimbo ya Bumbuli, Mlalo, Peramiho, Handeni Mjini na Chalinze na hivyo kulazimika kukata rufani.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema sababu za wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo hayo kutupa pingamizi hizo, siyo za msingi na inaonekana wamepanga kuwabeba wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi wa Uchaguzi Nec, Ramadhani Kailima, alisema hakuwapo ofisini wakati rufani hizo zinapelekwa, lakini alisema anaamini zitafanyiwa kazi.

“...lakini kama wamesema wameleta, yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Nec ndiye muamuzi wa mwisho katika suala hilo na ikishatoa uamuzi hauwezi kupingwa popote ikiwamo mahakamani labda yawe ni jinai yanayohusisha matusi au rushwa,” alisema.

KUZINDUA KAMPENI JUMAMOSI
Na katika hatua nyingine, Mwalimu alisema Ukawa watazindua kampeni zake Agosti 29, mwaka huu katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia sababu za awali kutaka kuutumia Uwanja wa Taifa katika uzinduzi huo, alisema ni za kiusalama, idadi kubwa ya wafuasi wao.

Hata hivyo, alisema wameshangazwa na serikali kuwanyima uwanja huo kwa kutumia kigezo ya mihemko mikubwa ya kisiasa na kwamba kitendo hicho ni muendelezo wa kuminya demokrasia nchini.

1 comment:

  1. WATANZANIA WAPENDA MABADILIKO TUMECHOKA NA UNYANYASAJI WA WAZIWAZI UNAOONESHWA NA CHAMA CHA MAPINDUZI(CCM). TUNACHOOMBA VIONGOZI WETU KUWENI IMARA NA KAMA IKIBIDI HAMASISHENI WANACHAMA NA WAPENZI WA UKAWA-CHADEMA WAANDAMANE KUSAKA HAKI.

    CCM WAMEZOWEA KUMINYA HAKI YA USHIRIKI WA VYAMA VINGINE VYA SIASA KWA KUJIONA WAO NDIYO WANA HAKI KUPITA WENGINE. KAMA NI VIWANJA NI VYA TANZANIA SIYO VYA CCM HIVYO KILA MMOJA AKIHITAJI ANA UHURU WA KUKITUMIA.

    VIONGOZI WA UKAWA NA CHADEMA KWA UJUMLA TANGAZENI MAPEMA KUHUSU KAMA UZINDUZI UTAFANYIKA JUMAMOSI YA TAREHE 29/08/2015 ILI TUJIANDAE MAPEMA.

    KUTOKA MOYONI NAPENDA KUSEMA WAZI NIMEICHOKA NA TUMEICHOKA CCM KWA SERA ZAKE ZA KIBAGUZI. VIONGOZI WAKE WAMEJAA MAJIVUNO YA AJABU MPAKA WANAFIKIA KUTUTUKANA KATIKA MAJUKWAA KUWA SISI WATANZANIA TUNAOUNGA MKONO HARAKATI ZA MABADILIKO KUWA NI WAPUMBAVU NA MALOFA...!!!

    MUNGU ATAKUWA AMESIKIA MAUMIVU YETU MIOYONI YA KUTUKANWA NA KUKANDAMIZWA KATIKA KILA NYANJA YA MAISHA.

    HEBU TAZAMA CCM WALIVYO WANAFIKI, SASA HIVI MADEREVA WA BODABODA HAWAKAMATWI NA KUBUGUDHIWA KISA UCHAGUZI ILA UKIISHA WANAWAFUKUZA TENA , MAMA NTILIE NAO KWA SASA HAWASUMBULIWI ILA UCHAGUZI UKIPITA WANALO, WAFANYA BIASHARA WANAOTANDAZA BIASHARA ZAO MAENEO YA HIFADHI ZA BARABARA NAO KWA SASA HAWASUMBULIWI KISA UCHAGUZI LAKINI BAADA YA HAPO WANACHEZEA VIRUNGU. JE HUU SI NI UNAFIKI MKUBWA??????

    MAGUFULI NAE KASEMA AKIWA RAIS MGAMBO WATAFUTE KAZI NYINGINE YA KUFANYA ANA MAANA GANI?? INA MAANA HAPO KABLA ALIKUWA HAONI KERO WANAYOSABABISHIA WANANCHI??

    HUU NI WAKATI WA MABADILIKO TWENDE NA LOWASSA TWENDE NA UKAWA. TANZANIA BILA CCM INAWEZEKANA TENA ASUBUHI KWEUPE.

    ReplyDelete