Friday, July 17, 2015

VIJANA 32 WA CCM wajiunga na CHADEMA

Vijana 32 waliokuwa wanachama wa CCM wakiwawakilisha wenzao 100 walipowasili katika Ofisi ya CHADEMA Mkoa wa Kinondoni kujiunga na ‘people’s power’ , kulia ni Diwani wa Kata ya Makumbusho, Ulole Ulole akiambatana nao kuwapeleka ofisini ambako walipokelewa na kupewa kadi za uanachama wa CHADEMA rasmi na viongozi wa chama mkoa.
Viongozi wa Chama waliowapokea vijana hao ni majira ya saa 6 mchana leo ni Mwenyekiti wa Mkoa Waziri Muhunzi, Ester Semanya (Makamu Mwenyekiti), Suzan Lyimo (Mbunge Viti Maalum CHADEMA), Rose Mushi (Diwani Viti Maalum Kinondoni) pamoja na wanachama wengine.
Vijana hao ambao wengi wao ni wanafunzi wakiongozwa na Michael Litanga wamesema kuwa wameamua kukimbia CCM kutokana na ubovu wa chama hicho na kwamba kadri siku zinavyokwenda kinajiweka mbali katika kuwatumikia wananchi huku kikionesha kushindwa kuendelea kuongoza akisema kuwa CHADEMA ndiyo chama mbadala wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Mbunge wa Viti Maalum Lyimo aliwaambia vijana hao kuwa wamejiunga na chama katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo vijana wa CHADEMA wamepewa majukumu makubwa ya kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na wimbi la mabadiliko kwa ajili ya kwenda kuiondoa CCM madarakani.
Aidha, Lyimo aliwasisitiza kuisoma Katiba CHADEMA ili kuelewa misingi ya chama hiki kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kuwashawishi wengine.

No comments:

Post a Comment