Friday, July 17, 2015

UCHUKUAJI NA UREJESHAJI WA FOMU KUWANIA UTEUZI WA UDIWANI NA UBUNGE NA UTARATIBU WA KURA YA MAONI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIUCHUKUAJI NA UREJESHAJI WA FOMU KUWANIA UTEUZI WA UDIWANI NA UBUNGE NA UTARATIBU WA KURA YA MAONI

Kuanzia jana Julai 15 hadi 19 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefungulia rasmi milango kwa watu wenye nia na sifa kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge kwenye majimbo yenye wabunge wa chama hicho.

Aidha, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi, CHADEMA pia kimelazimika kupangua ratiba ya awali na sasa kimeruhusu wanachama wote wenye sifa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi wa ndani ya chama katika nafasi za udiwani na ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima.

Kupitia Waraka wa Katibu Mkuu Namba 5 wa mwaka 2015, uliosainiwa na Katibu Mkuu Dk. Willibroad Slaa, chama kimesema kuwa wananchi wote wenye nia na sifa za kuchukua fomu za ubunge kwenye majimbo yote yakiwemo mapya wanaruhusiwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 15/07/2015 hadi saa 10 jioni tarehe 19/07/2015.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Dk. Slaa, kwa nafasi za udiwani , zoezi la kuchukua na kurejesha fomu katika kata zote nchi nzima limeongezwa muda kuanzia Julai 15, 2015 hadi 29/07/2015 saa 10 jioni.

Itakumbukwa kuwa hapo awali CHADEMA ilitoa ratiba yake ya uteuzi wa ndani ambapo ilionesha kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge katika kata na majimbo yenye madiwani au wabunge wa chama hicho ulitakiwa kusubiri hadi halmashauri zitakapokoma au bunge litakapokuwa limevunjwa.

Katibu Mkuu pia ameelekeza kuwa baada ya NEC kutangaza majimbo mapya 26 kwa upande wa Tanganyika, fomu za kuwania uteuzi katika majimbo hayo zitaendelea kutolewa katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na jimbo kwa utaratibu ule ule ambapo makatibu wa majimbo mama (yale ya zamani) wataendelea kutoa fomu kwa ajili ya majimbo mapya.

“Wagombea ambao walishachukua na kurejesha fomu wana haki ya kuamua jimbo lipi wanaenda kugombea na hawalazimiki kuchukua fomu upya…watatakiwa kuujulisha uongozi wa chama ngazi ya jimbo kwa barua rasmi kuonesha kuwa fomu yake iwe ni ya jimbo lipi kati ya jimbo mama ama jipya na nakala ya barua hiyo inakiliwe ngazi ya wilaya, mkoa, kanda na taifa,” ameelekeza Katibu Mkuu Dk. Slaa.

Kuhusu zoezi la kura ya maoni

Kupitia waraka huo ambao umetumwa kwa Waratibu wa Kanda, Wenyeviti na Makatibu wa majimbo, Katibu Mkuu Dk. Slaa ameagiza kuwa majimbo yote yanatakiwa kuanza zoezi la kura ya maoni tarehe 20-25 Julai mwaka huu kwa kuzingatia Mwongozo wa Taratibu za Kura ya Maoni ambao umeshatumwa nchi nzima.

“Kwa majimbo ya yaliyogawanywa kila jimbo litafanya mchakato wake wa kura ya maoni kwa kusimamiwa na mamlaka zilizotajwa katika mwongozo husika. Hii maana yake ni kwamba zoezi la kura ya maoni litafanyika kwa siku 6 mfululizo. Kila kanda inapaswa kuweka ratiba yake ya ndani katika muda huo na kuhakikisha kuwa majimbo yote, ya zamani na mapya, katika kanda husika yakamilishe kura za maoni ndani ya tarehe hizo.

“Kamati Kuu iliazimia pia kuwa kura za maoni nafasi ya udiwani zitaanza kufanyika kuanzia tarehe 30 Julai hadi 5 Agosti, 2015. Hii maana yake ni kuwa zoezi la kura za maoni kwa nafasi ya udiwani litaanza baada ya kumalizika kwa zoezi la kura za maoni nafasi ya ubunge,” ameagiza Katibu Mkuu Dk. Slaa kupitia waraka huo.

Aidha Katibu Mkuu amewaagiza Waratibu wa Kanda za CHADEMA kusimamia utaratibu wa kuwatangazia wananchi katika majimbo yote kwa njia anuai ikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, matangazo kwenye mbao na nafasi mbalimbali za hadhara ili Watanzania wote wapate fursa ya taarifa hiyo muhimu.

Imetolewa leo Alhamis, Julai 16, 2015 na
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:

Post a Comment