Saturday, July 18, 2015

Mbunge Lembeli aondoka CCM

HUYU ameondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anasema, chama hicho kinanuka rushwa na kwamba yeye hawezi kugombea kwenye chama ambacho kimebeba wala rushwa. Ni James Lembeli, mbunge wa Kahama mkoani Shinyanga.

Akizungumza na wanachama wa CCM, wilayani Kahama, Lembeli amesema, “…nimekuja kuwaeleza, kwamba sitagombea ubunge katika jimbo hili kupitia CCM.”

Hii ilikuwa majira ya saa nne asubuhi. Mara baada ya kauli yake hiyo, kuliibuka tahahuri miongoni mwa wanachama wa chama hicho, waliokuwa wamejazana ofisini kumsubiri Lembeli achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Mbunge huyo machachari nchini alikuwa ni miongoni mwa wabunge waliojipambanua kupinga ufisadi, ndani na nje ya Bunge.

Kabla ya uamuzi huo, Lembeli amekuwa akilalamikia chama chake kubeba baadhi ya wagombea; kujenga makundi ya wanamtandao na kuanza kampeni kabla ya muda.

“Sitaki kuwa sehemu ya uchafu huu. Hivyo, nimeamua kutogombea ubunge kupitia CCM, ingawa nitagombea kupitia chama kingine,” ameeleza.

Amesema katika ziara zake jimboni amekuwa akipokea kadi nyingi ambazo zimetolewa na wagombea kinyume cha taratibu na taarifa hizo alizifikisha katika ofisi ya wilaya lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Mara baada ya kutoa shutuma hizo, Lembeli aliondoka katika ofisi hizo bila kusalimiana na katibu wa chama hicho wilayani Kahama ambaye alikuja kumsubiri ili amkabidhi fomu za kuwania ubunge kupitia CCM.

MwanaHALISI Online, lilipoulizwa katibu wa CCM wilaya ya Kahama, Alexandulina Katabi, kuhusu madai ya Lembeli, haraka alisema, “madai hayo yanapaswa kupelekwa ofisini siyo kwenye magazeti.”

Alisema, kamati ya maadili ya chama hicho iliwahi kumuita mbunge huyo ili kuja kutoa ushahidi, lakini amegoma kufanya hivyo.

Alisema, “kadi feki zinajulikana kupitia kwangu kwa kuwa ndiye ninayezitoa.”

Taarifa ambazo zimepatikana baadaye zinasema, Lembeli anatarajiwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), muda wowote kutoka sasa.
Aidha, wabunge wengine wa CCM majina tunayo, wanatarajiwa kujiunga na chama hicho na kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini.

Mwanahalisi Online

1 comment: