Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wamempa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, majukumu ya kuikomboa nchi kwa mara ya pili kama alivyofanya mwalimu Julius Nyerere wakati akiitoa mikononi mwa wakoloni.
Jukumu hilo alipewa jana na wazee hao baada ya kumvisha vazi la uchifu na kumkabidhi vitu mbalimbali vikiwamo kisu, panga, shoka, jembe, nundu na usinga ikiwa ni ishara ya kumtawadha kushika madaraka hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo sasa atatambuliwa kama Chifu Mwinyikambi.
Mzee Ally Mwinyikambi, ambaye alimkabidhi Dk. Slaa uchifu huo kwa niaba ya wazee wa mkoa huo, alisema wanamtaka ahakikishe anakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema kuwa, kilichotokea kimekumbusha enzi za Nyerere wakati akiwa anatoka masomoni.
Alisema kitendo hicho kimekihakikishia chama hicho ushindi wa kuelekea Ikulu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwahakikishia wazee hao na Watanzania kwa ujumla kuwa, uchaguzi huu lazima washinde kwa kishindo.
Alisema licha ya Mwalimu Nyerere kuwataja maadui wa nchi kuwa ni umaskini, ujinga, maradhi lakini CCM katika utawala wake wote imeshindwa kuyaondoa hayo.
“CCM imekuwa ikikusanya wazee wa chama chao pekee kwenye ukumbi na kuwapa Sh. 5,000 bila kuangalia matatizo yao, sisi hatuna ubaguzi na tunawatambua wazee wote wa nchi hii,” alisema.
Alisema licha ya CCM kutawala muda mrefu lakini huduma za jamii kama barabara, afya, elimu utekelezaji wake bado ni hafifu wakati wananchi wamekuwa wakitozwa kodi.
“Tunadai chenji zetu kwenye Richmond, Epa, Escrow kwa sababu hizi ni fedha za watanzania ambao ndio walipakodi,” alisema.
Dk. Slaa alisema watakapoingia madarakani miaka kumi watahakikisha nyumba zilizojengwa kwa nyasi zinatoweka huku huduma za afya zilipungua gharama zake kulingana na kipato cha Mtanzania.
Kuhusu mashine za kuandikisha wapiga kura za Kieletroniki Biometrick Voters Registration, katibu huyo aliwataka wazee kutumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji na kuhakikisha hawatoki vituoni hadi vinafungwa.
Akiongelea migogoro ndani ya nchi ukiwemo ule wa madereva ambao waligoma hivi karibuni, alisema kuwa serikali haipaswi kutafuta mchawi bali itafute muafaka.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, wakili mashuhuri, Mabere Marandu, alisema kuwa Chadema haina tamaa ya madaraka na kwamba wakiingia madarakani muda wake ukiisha na wananchi wakiona hawajafanya kitu, wapo radhi kuondoka.
Naye, mwenyekiti wa Wazee Tanzania, Hashimu Issa Juma, alisema kuwa Chadema ikiingia madarakani itatoa pensheni ambao haitapungua 100,000.
Pia alisema watatoa matibabu bure na huwahakikishia usafiri wa daladala utakuwa bure.
Huko unakoenda siko Dr! Mazindiko waachie CCM wewe mtangulize Mungu!
ReplyDelete