Thursday, July 9, 2015

Chadema yaonya watakaotumia fedha kusaka uongozi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara, kimewaonya wanachama wake wanaosaka uongozi waepuke kutumia fedha vinginevyo majina yao yatakatwa na kuchukuliwa hatua kulingana na taratibu za chama hicho.

Mbali na hilo, wametakiwa pia kuepuka kupakana matope kwenye kampeni ndani ya chama, kwa vile watakiwa wanakiharibia mbele ya wananchi ambao ndiyo wapigakura.

Mwenyekiti wa Chadema wa mkoa huo, Vicent Nyerere (pichani) alitoa onyo hilo juzi, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mukendo mjini Musoma.

Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), alikuwa akihamasisha wakazi wa mji huo kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.

Alisema kipindi cha uchukuaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge kumekuwapo na taarifa kwamba baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya ugawaji fedha na kuharibiana wenyewe kwa wenyewe.

Alisema kuwa Chadema haina sifa za ulaji rushwa, hivyo atakayebainika kujihusisha na vitendo hivo, jina lake litakatwa mapema sana na kisha hatua nyingine zitachukuliwa dhidi yake.

"Hiki chama siyo cha wala rushwa, kama kweli kuna mtu anatumia fedha kuhonga wananchi ili apenye kwenye mchakato wa kupata mwakilishi kwenye ngazi ya kata na jimbo, basi ahesabu maumivu," alisema Nyerere.

Alisema Chadema ni chama mbadala, hivyo hakina budi kufanya mambo ambayo yanalenga kuleta maendeleo na siyo kama vyama vingine ambavyo ulaji rushwa limekuwa ni jambo la kawaida.

"Nirudie kwamba kama kuna mtu anatumia fedha kuhonga ili apate uongozi, atambue kuwa Chadema hakina utaratibu, akatafute kwingine atawapa wanaoendekeza vitendo hivyo," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema mtu anayetafuta uongozi kwa kuhonga hafai na anaweza kuwa mzigo kwa taifa.

No comments:

Post a Comment