Thursday, June 4, 2015

Ukawa wawaponda waliotangaza nia CCM

Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.

Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na mgombea safi.

Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo.

Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.

Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili.

“Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere, vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo.


“Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru) anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.

Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje.

Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi.

“Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.

No comments:

Post a Comment