Friday, June 12, 2015

Mbowe: Sheria tata zinalenga kudhibiti upinzani Oktoba.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, (pichani) amesema sheria tatu za makosa ya jinai zilizo mbioni kupitishwa na serikali, zimelenga kuwanyamazisha wapinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao, ili wasiweze kuanika madudu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika taarifa yake iliyopatikana jana jijini Dar es Salaam, Mbowe alizitaja sheria hizo ambazo ama zimesainiwa au zinasubiri saini ya rais kuwa ni pamoja na ile ya Muswada wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015.

Alisema kuna nia moja tu inayoweza ikaeleza ni kwa nini sheria hizi zimepelekwa mbio mbio, nayo ni kutokana na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Uwingi wa sheria hizo mpya kwa pamoja kunaweza kunyamazisha ukosoaji wa kukosekana kwa utawala bora, na kukandamiza kile ambacho kimekuwa ni utamaduni wa vyombo vya habari wa kuchunguza na kuripoti ufisadi, ndani ya serikali,” alisema.

Mbowe alifafanua kwamba, Muswada wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, utawazuia waandishi wote na vyombo vya habari kujiendesha, kuwa na baraza lao la habari, isipokuwa waandishi wenye leseni tu.

Aidha alisema muswada huo unalenga kudhibiti machapisho hadi majarida madogo na blogs, na kutoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makosa, pamoja na kuyafungia magazeti.

Kwa upande wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, alisema itaharamisha machapisho ya mtandaoni yanayoonekana na serikali kuwa na habari za kupotosha, udanganyifu au uongo.

Aidha, alisema sheria hiyo inatoa mamlaka kwa polisi ya kukagua nyumba za watuhumiwa, kukamata kompyuta zao na kutaka takwimu zao kutoka kwa watoa huduma wa mitandaoni

“Itakuwa ni kosa la jinai kutuma barua pepe au mawasiliano mengine ya kielektroniki bila ya idhini,” alisema. Kwa upande wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015, Mbowe alisema inaharamisha uchapishaji wa takwimu ambazo kwa maoni ya serikali zitakuwa ni za uongo, na adhabu yake itakuwa faini ya Dola 6,000, au hukumu ya miaka mitatu jela.

“Mtafiti au mwandishi anaweza kwenda jela kwa kuchapisha takwimu ambazo serikali haikubaliani nazo,” alisema.

Mbowe alizitaka nchi washirika katika maendeleo na jumuiya ya kimataifa kumsisitiza Rais Jakaya Kikwete kutozisaini sheria hizo, na kuzirudisha tena bungeni ili mambo yote yaliyolenga kuvisambaratisha vyombo vya habari na kukandamiza uhuru wa kujieleza yaweze kuondolewa.

No comments:

Post a Comment