Thursday, June 25, 2015

Lema avutana na Polisi, NEC.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) , amemtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, kujiandaa kupokea mkanda wa DVD ya bomu lililorushwa katika mkutano wa Chadema, Juni 15, 2013 kabla ya Bunge kuvunjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lema alidai amechukua hatua hiyo kutokana na Sabas kutuma Jeshi la Polisi toka nje ya mkoa huo kwenda kufanya kazi maalum ya kummaliza nguvu kabla ya uchaguzi.

Alisema umma wa Watanzania anapenda wajionee polisi waliohusika kufanya unyama katika ufungaji wa kampeni za udiwani kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema.

Kuhusu uandikishwaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafanya hujuma ya kusitisha uandikishwaji wakati idadi ya watu ikiwa kubwa kwenye kata zilizoanza kuandikisha.

“Walichofanya ni kuorodhesha majina ya watu waliokuwapo juzi kituoni na jana wanawamalizia hao na wanaokuja ambao ni wengi wanakataliwa kuwa zoezi limefika mwisho maeneo hayo, wakati maeneo mengi wameongeza siku tatu na siyo majiji makubwa kama Arusha,” alisema.

Alisema tayari ameagiza wenyeviti wa mitaa kukusanya idadi ya wapiga kura waliobaki kila mtaa na walioandikishwa, kisha atafanya maandamano makubwa ya kupinga dhambi hiyo.

Hata hivyo, amemwomba Rais Jakaya Kikwete kumwondoa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, katika nafasi hiyo akidai ameshindwa kuendesha vizuri kazi ya uandikishwaji na kuhatarisha amani ya Tanzania katika uchaguzi ujao.

“Huyu Lubuva anasema mimi nasababisha vurugu naingilia Tume, kumwambia watu ni wengi aongeze mashine ni kosa, ameshindwa kuleta watumishi wa Tume, mashine chache na ameweka watu wasio na sifa na kusababisha watu kulala vituoni,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Liberatus Sabas, alisema Lema anatakiwa kuhamasisha wananchi wake kufanya maendeleo, badala ya kuendesha vurugu na maandamano.

“Huyu Lema watu wamemchoka na amebakiza siku chache kumaliza muda wake na kurudi kuwa raia kama wengine, hivyo amalize salama na asitafute shari, ila akileta vurugu na mwingine atakayesababisha uvunjifu wa amani katika zoezi hili, atakumbana na mkono wa dola na jeshi lipo vizuri,” alisema.

1 comment:

  1. Kamanda acha kuwatishabwapiga kura. Wana haki ya kuandikishwa katika daftari sio .kufanya njama.

    ReplyDelete